Huyu mtu ametajwa katika mambo mengi ya kishetani.
Shetani siku zote wapo, si ajabu. Maajabu makubwa ni kwa kiongozi mkuu kumkumbatia shetani. Na maajabu ya kushangaza zaidi ni pale nilipomsikia kadinali akimsifia. Siku zote nimejitahidi kuwa mwaminifu kwa imani yangu Katoliki lakini kauli za kadinali kumsifia mtu ambaye mikono yake imejaa damu, iliisumbua sana nafsi yangu.
Tuliomba siku zote viongozi wa dini wakemee uovu utendwao na watawala lakini zilisikika sauti chache sana za maaskofu wa KKKT na Askofu Mwamakula wa Morovian. Wengine wote kimya.
Lakini nimeuona ukuu wa Mungu. Aliwafanya maaskofu kuwa mabubu lakini kilio na maombi ya wenye haki yalipokelewa mbele ya Bwana wetu. Bwana aliye asili ya ukuu na hekima, akatutafutia sauti yenye nguvu zaidi kuliko ya Maaskofu.
Je, watawala watakuwa kama Farao? Watafanywa mioyo yao kuwa migumu? Watamkatalia Musa kuwaondoa wana wa nchi kwenye utumwa wa kugandamizwa uhuru wao? Au watawala watasubiri mpaka malaika wa Bwana apite kuangamiza kila mzaliwa wao wa kwanza?
Ukuu na utukufu wa Mungu haudhihakiwi. Kila tunapoenda kwenye madhabahu ya Bwana, tukalia kwa unafiki, tukakariri vifungu vya biblia ili kuwahadaa watu tuonekane watu wa haki, tukatoka na kuendelea kudhulumu wanadamu wenzetu, tunavuna laana na hukumu.
Enyi watawala kama mtajaliwa japo chembe ndogo ya hekima ya ukubwa wa umbile la punje ya ufuta, mtamsogelea Bwana kwa moyo wa toba, mtairarua mioyo yenu iliyojaa ushetani, na kumlilia Mungu wa kweli awatenge na uovu. Lakini kwa kuwa mmekosa hekima, mtajikweza na kutaka kuonesha ukuu wenu. Hakika ndipo mtakapoujutia uovu wenu.
Neno la Mungu lasema, Mungu wetu si kiziwi, na maamuzi yake hayakawii, bali huja kwa wakati wake.
Wenye uwezo wa kuomba kuondokana na viongozi waonevu na wauaji, waombe. Wenye uwezo wa kukemea dhuluma ya watawala kwa watu wao, wakemee. Wenye uwezo wa kupinga dhuluma, wapinge kwa nguvu zote. Ili kila mmoja atumie karama yake kulinda na kupigania haki, haki ile tuliyopewa toka tulipoumbwa. Sote tuliumbwa na roho moja na idadi ya viungo vifananavyo ili kutuonesha kuwa hakuna aliye na ubinadamu zaidi ya mwingine.
Mungu wetu Mkuu, ushindaye wakuu wote wa Dunia hii, tunaomba utujalie ujasiri wa kuinena na kuiishi kweli yako. Maana wewe Bwana si mwoga na wala si tepetepe mbele ya ibilisi.