Makamu Mwenyekiti wa CCM BARA ataongea na umma juu ya msimamo wa chama na diplomasia ya kimataifa kutokea Ofisi ndogo za CCM - Lumumba.
UPDATE
Itakumbukwa kwamba Mkutano wa 10 wa Vyama vya Ukombozi vya Kusini mwa Afrika uliofanyika Zimbabwe tarehe9-12 Septemba 2019 uliazimia Vyama kupaza sauti kwa pamoja kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuondoa mara moja vikwazo dhidi ya Zimbabwe
Kwa kutambua Jukumu letu ktk kuimarisha Umoja, Mshikamano wa Waafrika na kuendeleza mapambano dhidi ya Ukoloni Mamboleo, kupiga vita Ubeberu na Ubaguzi wa aina yoyote pamoja na kuimarisha uhusiano mwema na Vyama vyote vya Siasa vya Nchi nyingine vyenye itikadi kama ya CCM
CCM kinaamini kuwa vikwazo dhidi ya watu wa Zimbabwe ni muendelezo wa fikra na matendo ya uonevu na unyonyaji kwa Waafrika. Watu wa Zimbabwe wameonewa kiasi cha kutosha, na sasa tunaazimia kuwa uonevu huo ufike mwisho
Vikwazo dhidi ya Zimbabwe vimewekwa takribani miaka 19 sasa tangu mwaka 2000. Wanaadhibiwa wananchi ambao wengine hata walikuwa hawajazaliwa wala kusababisha kwa namna yeyote kuwekwa kwa vikwazo hivyo
CCM kama sehemu ya Vyama vya Ukombozi ktk Bara la Afrika na hasa kwa nafasi yake ya kuwa Chama Kiongozi wakati wote wa mapambano ya kulikomboa Bara la Afrika Kisiasa na sasa mapambano yanayoendelea ya kuikomboa Afrika na Tanzania Kiuchumi
CCM inatumia nafasi hii kupaza sauti na kushinikiza mataifa yote ambayo yameiwekea vikwazo Zimbabwe, kuhakikisha yanaondoa vikwazo hivyo bila masharti yoyote ili nchi hiyo iweze kupiga hatua za haraka za Kimaendeleo, Kiuchumi na Kijamii kwa watu wake
Tunatambua na kupongeza Serikali za Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) chini ya Uenyekiti wa Rais Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania kwa kutoa kauli moja kulaani vikwazo dhidi ya Zimbabwe na kutaka vikwazo hivyo kuondolewa maramoja.
Kwa tamko hili tunaweka msisitizo, kupitia kwa Serikali ya Tanzania, Serikali za Nchi wanachama wa Jumuiya ya SADC
na Nchi wanachama wa Jumuiya ya EAC kwamba ufike wakati Umoja wa Afrika uchukue nafasi yake na kusimamia haki za Nchi wanachama.
CCM inatambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Zimbabwe ikiwemo kuimarisha demokrasia na uongozi bora pamoja na kujitegemea kiuchumi; lakini kutokana na vikwazo hivyo nchi hiyo inashindwa kupiga hatua za maendeleo kiuchumi na kijamii kwa kasi inayostahili
Ustawi wa watoto, akina mama na vijana ndio ulioathirika vibaya zaidi, hawa wote wanaumizwa na vikwazo ambavyo vinaathiri Taifa lao
Mapinduzi ya Afrika ambayo lengo lake ni Ukombozi kamili wa Mwafrika yanapingana na Siasa za Kimataifa za kinyonyaji, za ukoloni-mamboleo na ubeberu ambazo kwa muda mrefu zimekwapua utajiri wa Afrika na kuutumia utajiri huo kwa maslahi ya Nchi zao badala ya kuwanufaisha waafrika
Kwa kuzingatia ukweli huo, kushiriki katika Mapinduzi ya Afrika na kushiriki katika ukombozi uliobaki, ukombozi wa kiuchumi ni jambo la msingi kwa Chama chetu
CCM kinaamini na kutambua kwamba Watanzania tunathamini sana uhuru wa Taifa letu, maana hapo ndipo ulipoanzia ukombozi wa wananchi wengi wa Afrika. Kwasababu hii tuna wajibu wa kuchukua hatua zote muhimu zitakazotuwezesha kulinda uhuru wetu
Chama Cha Mapinduzi, Vyama vya Ukombozi vya Kusini mwa Afrika na watu wote wenye mapenzi mema na watu wa Zimbabwe tutaendelea kupaza sauti hadi hapo Jamhuri ya Zimbabwe itakapoondolewa vikwazo hivyo vya kiuchumi