Wangwe kuishitaki CHADEMA
na Mwandishi Wetu, Dodoma
ALIYEKUWA Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chacha Wangwe, ambaye alisimamishwa uongozi juzi, amesema atakifikisha chama hicho mahakamani iwapo kitamzushia kashfa ambazo si za kweli.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, baada ya CHADEMA kutoa taarifa rasmi kuelezea kusimamishwa kwake katika nafasi ya makamu mwenyekiti, Wangwe aliwataka viongozi wa chama hicho wanaomtuhumu kwa mambo mbalimbali, kuyathibitisha madai yao, huku akionya na kusisitiza kuwa, iwapo watamzulia jambo lolote, atakwenda mahakamani.
Hawawezi kunituhumu kwa masuala ya uongo. Inabidi wa-prove (wathibitishe) tuhuma wanazotoa dhidi yangu
kama wanasema nimevujisha nyaraka wathibitishe hivyo, kama wanasema nakihujumu chama wathibitishe pia, alisema Wangwe.
Hata hivyo, alikiri kusimamishwa uongozi, lakini akasema kusimamishwa kwake kumetokana na hila za Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ambaye juzi katika mkutano wa Kamati Kuu alieleza kuwa hawezi na hataki kufanya kazi na yeye.
Alisema kuwa ni kweli uamuzi wa kusimamishwa kwake ulifikiwa kwa mujibu wa katiba ya chama hicho baada ya wajumbe wa Kamati Kuu kupiga kura ya kuafiki uamuzi huo, lakini alidai kuwa maamuzi hayo yalichagizwa na msimamo wa Mbowe.