BURIANI CHACHA WANGWE UMEKUWA SOMO MUHIMU CHADEMA
Watu wengi humaliza safari zao za kuishi katika dunia kwa kupata ajali. Zipo ajali za aina nyingi, zikiwemo za magari barabarani.
Baadhi ya ajali huwa na utata na kuzusha mijadala ikiwa ni pamoja na kuhusisha njama za aina moja au nyingine, ikiwemo michezo michafu ya kisiasa. Hali hii inasemekana kuwakuta CHADEMA baada ya kifo cha CHACHA WANGWE.
Kwa kiasi kikubwa, hali hii inatokana na hatua ya WANGWE kujitoa muhanga kuisafisha CHADEMA na kuangaliwa na wanaCHADEMA kwa jicho la matumaini mapya. Hata hivyo, viongozi wa juu wa chama hicho hawakumpenda na kuhakikisha wanamuengua katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Ni ukweli unaodumu daima kwamba mashujaa wapigania haki na watetezi wa wanyonge wanaishi milele, hata kama wakifa bado wanaishi, fikra zao na mitazamo yao hubaki na kuendelea kutamalaki, maisha yote. Huo ndiyo ukweli pia kwa maisha ya CHACHA WANGWE. Huyu alikuwa ni zaidi ya mwanasiasa, alipitia kila aina ya misukosuko na adha kwa ajili ya kuwakomboa wanaCHADEMA. Kwa wanaCHADEMA na kwa jamii ya wapenda haki huyu alikuwa mkombozi halisi. Amekufa kwenye ajali yenye sura ya kupangwa.
Changamoto aliyotoa dhidi ya ubaguzi ndani ya CHADEMA ni muhimu hasa kipindi hiki taifa linapo omboleza kifo chake. Wakati tukilia na kufuta machozi iko haja ya kujiuliza kila mtu kwa nafasi yake ni nini amefanya kukabiliana au kukomesha unyanyasaji au ukandamizaji unaotokea ndani ya CHADEMA huku viongozi wakuu wa chama hicho wakiangalia.
WANGWE pia alijua jukumu lake katika maisha haya kama Mtanzania. Kwa kupambana na viongozi wa CHADEMA alijua pia anapambana na kifo. Aliishi kwa kadri ya wito na majukumu yaliyomkabili ndani ya chama chake. Alitetea wanyonge, akapigania haki yao bila woga wala upendeleo, akapata misukosuko mingi katika maisha yake hadi kupoteza maisha akililia kuleta mageuzi makubwa ndani na nje ya chama chake. WANGWE ametimiza wajibu wake katika kuhakikisha kwamba amekubali kufa mabegani mwa viongozi wa CHADEMA.
Tukumbuke daima kwamba haki au usawa hautolewi kwa hiari na wanaounyima, ni lazima udaiwe na wanaonyimwa haki hiyo. WANGWE kajitahidi kutuonyesha hivyo hadi akakosana na viongozi wa chama chake.
Tutafakari kilio cha akina MBOWE, ZITTO na SLAA kilikuwa cha huzuni au kufurahia kimoyomoyo kifo cha mtu ambaye alitishia nafasi zao ndani ya chama?
Pengine sasa ni wakati muafaka kwa viongozi hawa wa CHADEMA kukodi helikopta, tena sio moja bali hata tatu (kila mtu na yake) na kuzunguka nchi nzima ili kujibu na kujisafisha kufuatia tuhuma zinazotolewa dhidi yao kutokana na kifo cha WANGWE.