Kasheshe na wengine, hoja zilizomo humo ni za msingi na madai yanayotolewa ni mazito na yanayohitaji majibu. Hilo halina ubishi. Binafsi nitaangalia madai ambayo yanahusiana na "facts" kuliko yanayohusiana na "mitizamo na hisia". Hayo mengine ni vigumu kuyafuatilia kwani anayedaiwa kuwa mhusika hayupo tena (nitalirudia hili mwisho).
Madai yanayodai Ukweli wa takwimu na vidhibiti.
HOJA YA KWANZA YA WARAKA:
Si kweli kwamba matatizo yote yatamalizwa na fedha hizi lakini basi hata ofisi za chama zinaweza kuwa hai nchi nzima kitu ambacho kwa sasa hakipo. Mahesabu yanaonesha kuwa mtaji wa laki moja (Tshs.100,000/=) kwa wilaya moja nchini inatosha, hivyo kwa Wilaya 126 kwa mwezi jumla yake ni Tshs. milioni 12 (Tshs. 12,600,000/= ) zinahitajika ( Wilaya 126 x 100,000 kila wilaya = 12,000,000/=)
Hata tukisema tupeleke kiasi hicho kwa kila jimbo la uchaguzi jumla yake ni Tshs. Milioni 23 (Tshs. 23,000,000/=) kwa maana ya majimbo 213 x 100,000 = 23,000,000/=. Mhe. MBOWE anasema hizo ni pesa nyingi sana kwa uimarishaji wa chama. Mimi nasema hapana, kiwango hiki kwa kila Wilaya au Jimbo la uchaguzi ni muafaka kwani haba na haba hujaza kibaba.
MAJIBU YANAYOHITAJIKA:
Je ni kweli Chadema inapata ruzuku ya milioni 66 kwa mwezi? Na kama ni hivyo je ni kwa sababu gani wameshindwa kutumia kiasi (kama kilichopendekezwa na waraka au vinginevyo) kugawa fedha kila jimbo au kila wilaya ili kukiimarisha chama chao? Kwa maneno mengine, kinachohitajika kuoneshwa ni uhalalishaji wa matumizi ya fedha hiyo ukiondoa shughuli za kuimarisha chama wilani au majimboni. Yaani, ni kitu gani kinahalalisha matumizi ya fedha hizo nje ya kuimarrisha chama majimboni au wilayani. Je kati ya milioni 66 yawezekana kutoa milioni 12 au 23 kila mwezi kwa shughuli za kuimairisha chama wilayani/majimboni, kama haiwezekani ni KWANINI?.
HOJA YA PILI YA WARAKA:
Chini ya uongozi wa Mhe. MBOWE na wafuasi wake hawastaajabu kuwa kati ya Tshs. 374,144,000.40 zilizopatikana kama ruzuku katika ya Januari 1 na Juni, 30, 2008, Tshs. 350,000,000/= zilitumika Makao Makuu ya CHADEMA na Tshs. 25,000,000/= tu ndizo zilikwenda Wilayani kuimarisha chama.
MAJIBU YANAYOHITAJIKA:
Kwanza kama ni kweli Chadema inapokea milioni 66 kwa mwezi basi kiwango kilichotakiwa kuwa kimepatikana kwa miezi sita ya mwanzo ni milioni 396 na siyo 374 (isipokuwa kama kuna makato ambayo mimi sijayaingiza).
Katika hili cha kwanza kinachohitajika ni kujulikana kwanza kwa muda wa miezi sita ya mwanzo Chadema ilipata kiasi gani kama ruzuku. Na pili kati ya kiasi hicho ilitumia kiasi gani makao makuu na kwa vitu gani na kiasi gani kilitumika nje ya makao makuu. Tatizo siyo tu la kutumika kiasi hicho lakini hasa ni kuhalalisha matumizi hayo. Kama ni kweli zimetumika milioni 350 makao makuu ni wazi Chadema wanaweza kuonesha kitu hicho kilichostahil matumizi hayo. Kinyume chake pia ni kweli, kiwango chochote kilichotumika makao makuu lazima kioane na huduma au bidhaa iliyolipiwa kiasi hicho.
DAI LA TATU LA WARAKA:
Kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Mhe. MBOWE alitufahamisha wanachama kuwa alikuwa anakidai chama US $ 181,949.00 sawa na Tshs. 218,338,546. Mpaka sasa chama kimekwisha mlipa Tshs. 175,000,000/=
MAJIBU YANAHOHITAJIKA:
Hapa ni rahisi kwani ni swali la "kitu ni cheupe au cheusi"? Je Mbowe aliikopesha Chadema kiasi chochote cha fedha kwa mkataba gani? Hivyo kuna swali alikopesha au hakukupesha? Kama alikopesha ilikuwa ni kiasi gani na kwa mkataba gani?
Hili siyo gumu kulielewa na halina matatizo kwa sababu kama wanavyosema wenzetu "the devil is in the detail". Ni vizuri kuona mkataba huo (kama upo) na masharti yake. Endapo mashart hayo (kama riba n.k) ni kubwa mno basi kuna haja ya Chadema au Mbowe kuelezea ni kwanini waliingia mkataba wa aina hiyo ambao kimsingi unafanya Chadema kuwa na mzigo.
DAI LA NNE
Na kwa kuwa hata baada ya kuwa Mhe. MBOWE amekwisha lipwa zaidi ya nusu ya deni alilodai kuikopehsa CHADEMA, vifaa vyote yakiwemo magari, vipaza sauti na kadhalika vimebakia kuwa mali yake binafsi,
Hili nalo ni swali la "cheupe au cheusi"? Je vifaa vyote vikiwemo magari, vipaza sauti "n.k" vimebakia mali yake binafsi? Ni rahisi kulikanusha dai hili au kulithibitisha kwani vitu vina mmiliki na mali za Chadema zimeorodheshwa na mkaguzi. Chadema wanaweza kuliengua dai hili kwa kuonesha orodha ya mali zao.
DAI LA TANO
...ukweli wa suala hili hauna mjadala. Kwamba Mhe. MBOWE na wafuasi wake walighushi orodha ya majina ya viti Maalum badala ya kupeleka yaliyopendekezwa na Kamati Kuu sio siri. Naamini hata Mhe. MBOWE anakubaliana nami kuwa suala hili si moja ya siri anazodai nimevujisha!...
Yamesemwa mengi juu ya mtafaruku uliojitokeza kuhusu viti maalum hadi baadhi ya waasisi wa chama wakataka kujitoa na hivyo kumlazimisha Mwenyekiti Taifa ( FREEMN MBOWE) na Katibu Mkuu (DR WILBROAD SLAA) kukiomba radhi kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kwa kukiuka katiba, kanuni na maadili ya chama katika suala hili la kugushi viti maalum.
MAJIBU YANAYOTAKIWA:
Kwanza hapa kuna kitu tunachokiita kama 'pseudo-obviousness". Kwamba, ni ukweli usiopingika na kila mtu anajua ukweli huo. Sasa Chadema au Mbowe na wenyewe waseme kama ukweli huu ni readily available kuwa "walighushi orodha ya majina ya viti maalumu". Kama ni kweli basi wakiri ni ukweli kwani tumeambiwa na waraka kuwa hili halina "mjadala".
Zaidi ya yote kuwa Mbowe na Dr. Slaa waliomba radhi kwa "kughushi" na "kuvunja Katiba" ni madai mazito kwani yanakiri kufanya makosa yaliyotajwa. Je ni kweli radhi hiyo iliombwa na kwa kosa hilo la kughushi?
MADAI YA SITA - Ubabe
Mathalan kumzuia Martin Mungongo Mkurugenzi aliyechaguliwa kwa kura kutofanya kazi zake ndani ya chama, madai ya kupigana na watendaji wa chama ndani ya baa na vitendo vingine vya aina hiyo ni ushahidi tosha wa hulka hii. Hadi sasa Mhe. MBOWE amefanikiwa kukizuia chama hiki kisifanye kazi ya siasa mkoa wa Dar es salaam kwa miaka minne.
MAJIBU YANAYOHITAJIKA
Je ni kweli huyo mtu yupo? na je ni kweli alichaguliwa na ni kweli hafanya kazi yake? Lakini kubwa ni je hafanya kazi hiyo kwa sababu ya Mbowe? Na je ni kweli Chadema haifanyi kazi ya siasa mkoani Dar kwa miaka minne?
MADAI YA SABA: VYAMA DADA SHIRIKI
Vyama dada hivi vyote vinaulalamikia uongozi wa CHADEMA kwa kufuja fedha ya misaada na kuwasilisha kwao risiti za kugushi, kama ilivyofanyiwa Conservative Party baada ya kutoa msaada wa Tshs. 78,000,000 kwa ajili ya ununuzi wa baiskeli na pikipiki ambazo hazikununuliwa.
MAJIBU YANAYOHITAJIKA.
Hapa napo ni rahisi pia; je ni kweli vyama hivyo rafiki vinaulalamikia uongozi wa Chadema? Je ni kweli walitoa msaada wa Shs milioni 78 kwa ununuzi wa baskeli na pikipiki na vitu hivyo havijanunuliwa hadi sasa. Majibu yake ni rahisi kwani ni ndiyo au hapana na maeleezo kidogo.
MWISHO:
Utaona kuwa nimeyaacha madai yoyote ambayo yanadai mang'amuzi binafsi kwani kwanza hatujui mwandishi wa waraka huu ni nani hasa ingawa unataja kuwa ni wa "Wangwe". Hadi Polisi waseme kuwa kuna nyaraka za Wangwe ambazo zimepatikana na wanathibitisha kuwa ni za wangwe (through chain of custody) ni vigumu kukubali kuwa ni wa Wangwe. Lakini pia kwa sababu, masuala yanayohusu vionjo, hisia, mitazamo na mang'amuzi binafsi ni vigumu kluyahoji kwani ni vitu ambavyo vya kibinafsi sana. Lakini zaidi ni kwa sababu kama kweli ni waraka wa Wangwe kuna maswali ambayo yeye pekee angeweza kuulizwa.