View attachment 3425524
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelaani tukio la kusukumwa kwa mwenyekiti wake, Tundu Lissu na askari wa Magereza baada ya kesi ya uhaini inayomkabili kuahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kistu Dar es Salaam.
Video za tukio hilo zilizosambaa mitandaoni Agosti 13, 2025 zilimwonyesha Lissu akiwapungia mkono wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamehudhuria mahakamani hapo na ndipo askari Magereza waliokuwa wamemzunguka walimwondoa na kumsukuma.
Video:
Askari Magereza wamsukuma Lissu kidogo aanguke Kizimbani wakati akiaga Mahakamani
Taarifa iliyotolewa leo Julai 31 na Mkurugenzi wa Mawasiiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia imesema kitendo hicho ni cha kinyama na kisicho cha kibinadamu kilichotekelezwa na askari wa Magereza, ambaye alimshambulia kwa kumsukuma kwa nguvu na kumuangusha.
“Hili si tukio la kawaida. Ni tukio la kikatili, la kushtua, na linalodhalilisha utu wa binadamu. Ni hatari zaidi kwa kuwa limefanywa na mtu ambaye, kisheria, anapaswa kuwa mlinzi wa sheria, haki, ulinzi, na usalama wa raia wakiwemo wale wanaokabiliwa na kesi mahakamani ambao bado wanastahili kuonekana kuwa hawana hatia hadi itakapothibitishwa vinginevyo na vyombo vya sharia.
“Ni muhimu kuwakumbusha Watanzania wote kwamba Mwenyekiti, Mheshimiwa Tundu Lissu, bado anaendelea kuishi na ulemavu wa kudumu uliotokana na kupigwa risasi 16 katika jaribio la mauaji la Septemba 7, 2017. Kwa msingi huo, aina yoyote ya ukatili dhidi yake si tu kwamba ni kinyume cha sheria, bali pia ni tishio la moja kwa moja kwa maisha yake,” imesema taarifa hiyo.
Chama hicho kimeitaka Mahakama ya Tanzania kulichunguza tukio hilo na kuwachukulia hatua waliohusika.
View attachment 3425536