Changamoto ya Barabara Kijiji cha Kidemeni ni kubwa, inarudisha nyuma mwendo wa maendeleo

Changamoto ya Barabara Kijiji cha Kidemeni ni kubwa, inarudisha nyuma mwendo wa maendeleo

DodomaTZ

Senior Member
Joined
May 20, 2022
Posts
197
Reaction score
233
photo_2026-09-07_09-17-49.jpg
Kidemeni ni miongoni mwa vijiji vinavyopatikana katika Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, wananchi wake wana kilio cha kutokuwepo kwa barabara ya uhakika, hivyo kudai inachangia kudumaza maendeleo yao.

Kwa miaka kadhaa sasa, Zanzibar imeendelea kushuhudia mabadiliko makubwa ya maendeleo kupitia miradi mbalimbali inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wake, chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambayo inaendelea kuweka mkazo katika kuimarisha miundombinu, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa barabara katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.

Barabara zimekuwa sehemu muhimu na kufungua fursa za maendeleo kwa wananchi, kurahisisha usafiri kwa wananchi na usafirishaji wa bidhaa, kuunganisha jamii na kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za maendeleo.
photo_2026-09-07_09-17-56.jpg

photo_2026-09-07_09-17-52.jpg
Hata hivyo, pamoja na hatua hizo bado kuna maeneo ambayo wananchi wake wanaendelea kusubiri kuunganishwa kikamilifu na kasi hiyo ya maendeleo.

Kijiji cha Kidemeni, kilichopo ndani ya Shehia ya Kwale, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, mpaka sasa kina changamoto ya upatikananji wa barabara bora kama zilivyo sehemu nyingine za nchi na hivyo wananchi wake kukosa baadhi ya fursa muhimu.

Kwa msafiri wa kawaida inampasa kuweza kufikiria mara mbili pale anapowaza kufanya safari ya kuelekea kwenye kijiji hicho cha Kidemeni kwani si safari ya kawaida ni mwendo unaomfanya msafiri kuelewa kwa nini wakaazi wa kijiji hicho wamekuwa wakisema barabara ni changamoto kubwa inayowazuia kusonga mbele.

Kutoka Kwale hadi Kidemeni ni mwendo takribani saa mbili hadi tatu kwa mtembea kwa miguu, ni barabara inayopita katika maeneo yenye milima na mabonde imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa mamia ya wananchi wanaotumia barabara hiyo kwenda na kurudi katika shughuli zao za kila siku.
photo_2026-09-07_12-16-50.jpg
Kijiji hicho chenye zaidi ya kaya 150, wakaazi wake wengi wanategemea shughuli za kilimo na uvuvi, ambao wanaendelea kupaza sauti kuhusu hali ya miundombinu ya barabara hiyo inayowaunganisha na maeneo mengine.

Kwa wakazi wa Kidemeni, barabara si suala la urahisi wa safari pekee, ni suala linalogusa maisha yao ya kila siku, uchumi wao na uwezo wao wa kuzifikia huduma mbalimbali.

"Barabara ndiyo jambo la kwanza linalotuzuia maendeleo katika kijiji chetu," anasema Khamis Faki Ibrahim, mmoja wa mzee wa kijiji hicho.

Anasema hali huwa ngumu zaidi wakati wa msimu wa mvua ambapo barabara hiyo huwa katika hali mbaya zaidi, jambo linalowaongezea wananchi changamoto katika shughuli zao.

Kipindi cha Mvua kikianza barabara inakuwa ngumu kupitika na wakati mwingine hata kufikisha mahitaji muhimu inakuwa changamoto, jambo ambalo linawafanya wakaazi wengi wa Kidemeni kupaza sauti zao juu ya suala zima la kupata barabara yenye kupitiaka wakati wote kwa wakaazi wa kijiji hicho.

Bakari Mwalimu ni miongoni mwa wananchi wa kijiji hicho anakiri kuwa mazingira ya Kidemeni yana changamoto kutokana na uwepo wa milima na mabonde, lakini anaamini hali hiyo haipaswi kuwa sababu ya wananchi hao kuachwa nyuma katika safari ya maendeleo.

"Ni kweli kijiji chetu kipo katika mabonde na milima, lakini tunaiomba Serikali ituone na itutengenezee barabara yetu, tunahitaji kuunganishwa na maendeleo kama maeneo mengine," anasema.

Kwa wakazi hao, barabara bora ndiyo mwanzo wa mabadiliko wanayoyahitaji, kwani wanaamini kuwepo kwake kutarahisisha shughuli zao za kiuchumi na kupunguza vikwazo vinavyowakabili kwa muda mrefu.

Hata hivyo, nyuma ya kilio hicho kuna simulizi ya jamii ambayo imekuwa ikiishi na changamoto hiyo kwa miaka mingi, ikisubiri siku ambayo barabara yao itakuwa sehemu ya mipango ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Kwa wakazi wa Kidemeni, changamoto ya barabara haijaishia kwenye ugumu wa kutembea pekee, ni tatizo ambalo limekuwa likigusa karibu kila sehemu ya maisha yao ya kila siku kwani wananchi huwa wanafuata huduma muhimu katika mji wa Chake Chake kila uchao, licha ya ubovu huo wa miundombinu ya usafiri wa baara bara.

Katika kijiji hicho kinachotegemea zaidi kilimo na uvuvi, ambapo mazao mengi ya Baharini kama vile Chaza, Kombe, Makome n.k, hutokea maeneo hayo huku wananchi wake wakichukuwa bidhaa hizo kwa kichwa mpaka kufikia barabara kuu yenye masafa kutokana na kukosa usafiri unaosababishwa na ukosefu wa bara bara.

“Mazao yanapopatikana, changamoto kubwa huwa ni kuyafikisha sokoni kwa wakati kwa wavuvi, kwani safari ya kusafirisha bidhaa zetu kwenda maeneo mengine nayo imekuwa na vikwazo kutokana na hali ya Barabara,” wananchi wanasema.

Nurhat Kassim Khamis anaeleza kuwa barabara ndiyo msingi wa maendeleo ya kijiji chao, kwa sababu bila ya uwepo wake hata huduma nyingine zinakuwa ngumu kuwafikia wananchi.

“Barabara ndiyo jambo la mwanzo linalotusumbua. bila barabara maendeleo mengine yanakuwa magumu kufika kwetu," anasema.

Anasema wakati wa mvua hali huwa mbaya zaidi, ambapo baadhi ya maeneo ya huwa hayapitiki kwa urahisi na kuwalazimisha wananchi kutumia nguvu zaidi katika safari zao na wakati mwengine kusitisha safari hata kama ni mgonjwa kutokana na ubovu wa barabara.

Sheha wa shehia ya Kwale Khamis Suleiman Ali ,amekiri kuwepo kwa changmoto hiyo na kusema kuwa jitihada mbali mbali ameshazichukuwa katika kuhakikisha wananchi wa Kidemeni wanaondokana na changamoto wa Barabara ikiwemo kuzungumza na uongozi wa wilaya kwa barua lakini majibu hadi sasa hayajapatikana ya kuondowa kilio hicho.

“Kwa kweli mimi kama sheha naona aibu sasa kila siku naenda kulisemea hili Wilayani lakini naona choyo kuona vijiji vyengine wamenufaika na uwepo wa mendeleo ya DK, Mwinyi lakini sie bado tupo kwenye hali hii hivyo hata mimi nawatakia wanacnhi wangu maslahi naiomba wizara husika kutujengea barabara japo kwa kuiwekea hata fusi kwa hatua za awali ili nijenge imani na wananchi wa shehia yangu”, anaeleza.

Kwa upande wa Afisa Mdhamini Wizara ya Ujenzi na uchukuzi Pemba, Ibrahim Saleh Juma, anakiri kwa kusema serikali inafahamu changamoto za miundombinu zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo maeneo yenye mazingira magumu ya kijiografia kama Kidemeni.

Anaeleza kuwa Serikali imeendelea kuweka juhudi katika kuboresha miundombinu ya bara bara ili kuhakikisha wananchi wanapata mazingira bora ya kufikia huduma na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Anasema kuwa miundombinu ya bara bara ni sehemu muhimu ya kuhakikisha wananchi wa maeneo mbalimbali wanashirikishwa katika kasi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali na hivyo inaendelea kuangalia mahitaji ya wananchi katika maeneo mbalimbali na kuchukuwa hatua kulingana na mipango iliyopo.

“Wakazi wa Kidemeni ni kweli kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiri kuona mabadiliko katika bara bara yao ambayo wamekuwa wakiitegemea kwa shughuli zao za kila siku na Serikali bado haijawasahau na muda ukifika watajengewa”, anasema.

Wananchi wameeleza kuwa kuwepo kwa barabara bora kutawapa nafasi kubwa ya kusafirisha mazao yao kwa urahisi, kurahisisha shughuli za kiuchumi na kupunguza vikwazo vinavyotokana na mazingira ya bara bara hiyo.

Changamoto ya kutokuwepo kwa miundombinu ya yabarabara katika shehia ya Kidemani yanaibua pia mjadala mpana kuhusu umuhimu wa kuhakikisha maendeleo yanafika kwa wananchi wote bila kujali maeneo wanayoishi.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar inaweka msisitizo kuhusu usawa wa wananchi na wajibu wa kuhakikisha huduma na fursa za maendeleo zinawafikia wananchi bila ubaguzi hasa katika upatikananji wa hudumu muhimu za msingi katika jamii.

Moja ni suala la Barabara kwani hata wanafunzi nao wamedai itawarahisishia usalama wao tofauti na kukumbana na vichaka, milima na mabonde na sauti za ndege wakati wakielekea kwenye masomo yao ya Skuli ambapo inawagharimu muda wa zaidi ya saa hadi kufika Barabara kuu.

Wanasema hali hiyo inawaogopesha na kuhatarisha usalama wao hivyo hulazimika kutembea kwa makundi ili kujilinda na usalama wao hadi kufika katika maeneo husika.

“Hakuna anaependa kutembea katika vichaka, milima na mabonde bila hata kuona usafiri unapita tunatamani kuona na sisi tunapata Barabara sababu mwendo mrefu tunaotembea na kukutana na sauti tuu ya ndege haitupendezi ni vile ni nyumbani nani mambo ya lazima lakini tunaomba serekali ituangalie kwa hili”. anasema Ali Khamis mwanafunzi wa kidato cha tatu skuli ya Uzalengo ambae ni mkaazi wa Kijiji cha Kidemeni.

Mwajuma Ali anaeleza kuwa kutokana na ubovu na uchakavu wa barabara imekuwa vigumu hata kwa mama mjamzito anapotaka kujifungua kupata ugumu na changamoto mpaka kufikia Barabara kuu, hata wao maendeleo wanadai hawajayashuhudia tangu Mapinduzi matukufu ya mwaka 64 yanatokea zaidi ya kujionea kwa vijiji jirani.

Hata hivyo Wakaazi wa Kidemeni, matarajio yao si kupata upendeleo, bali kuona kijiji chao kikipewa nafasi sawa katika mipango ya maendeleo, ikiwemo bara bara ambayo itawaondolea changamoto inayowafanya wahisi kutengwa na kuwapa uhakika wa kusafiri katika mazingira salama wakati wote wa mwaka.

Kidemeni, inajenga picha iliyobaki haikuwa tu ya barabara yenye mashimo, mawe na miinuko lakini pia ilikua niuhalisia wa wananchi wanaoendelea na maisha yao huku wakisubiri miundombinu itakayowapa nafasi ya kusonga mbele kwa urahisi.

Shauku ya wananchio Kidemeni ni mfano wa namna ambavyo barabara inaweza kuwa zaidi ya miundombinu ya usafiri, inayoweza kuwa daraja la kuunganisha ndoto za wananchi, uchumi wa familia na kasi ya maendeleo ya taifa.

Kwa wakazi wake, ujumbe wao ni mmoja Maendeleo yanapofika katika maeneo mengine, na wao pia wanataka kuona na wao yanawafikia.

BY: FATMA SULEIMAN, PEMBA
 
Back
Top Bottom