.Balozi wa Tanzania Washington DC kuhudhuria
MWANDISHI WETU
Dar es Salaam
MAZISHI ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Marehemu Dk. Daud Timoth Said Ballali (65) aliyefariki Ijumaa iliyopita nchini Marekani yanafanyika leo na kuhudhuriwa na wageni waalikwa pekee.
Habari kutoka Washington DC, nchini Marekani yanakofanyika mazishi hayo zimeeleza kwamba familia ya Dk. Ballali imeamua mazishi hayo kushirikisha waalikwa pekee.
Kwa mujibu wa tovuti ya KLH News inayoratibiwa na Watanzania wanaoishi nchini Marekani, mwili wa marehemu Ballali umehifadhiwa katika Nyumba ya Maziko ya De Vol iliyoko Washington DC, kabla ya kuzikwa leo.
Kuna mwaliko katika mazishi hayo na hivyo sina hakika kama nitakwenda maana hadi sasa sijapata mwaliko, alisema Mtanzania mmoja anayeishi Washington DC, jana alipoulizwa na KULIKONI kama atahudhuria mazishi hayo kutokana na kuwahi kufanya kazi na Ballali.
Taratibu za mazishi zinaeleza kwamba Gavana Balali aliyefariki Mei 16, 2008, Washington DC atazikwa leo baada ya ibada itakayofanyika katika Kanisa Katoliki la Mt. Stephen Shahidi mjini Washington DC. Kanisa hilo lipo 2436 Pennsylvania Ave, NW Washington, DC 20037.
Ibada hiyo ya mazishi itaenda sambamba na kuuona mwili wa marehemu kuanzia saa nne asubuhi. Hata hivyo shughuli hiyo nzima ni kwa ndugu, jamaa, na marafiki wa karibu na si kwa hadhara ya kila mtu atakaye kushiriki, inaeleza taarifa ya tovuti hiyo ya KLHN.
Imeelezwa kwamba marehemu Ballali anatarajiwa kuzikwa katika makaburi ya Wakatoliki ya Gate of Heaven eneo la Silver Spring, MD.
Miongoni mwa watu mashuhuri walioalikwa mazishi hayo ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani Ombeni Sefue, watumishi wa idara mbalimbali alizowahi kuzitumikia ikiwemo Shirika la Fedha Duniani (IMF), ndugu zake ambao wamewasili siku chache zilizopita, na baadhi ya Watanzania kadhaa waishio maeneo ya Washington DC na miji jirani.
Hata hivyo, taarifa za tovuti hiyo zimegusia kitu ambacho sio cha kawaida kwa mila na desturi za Waafrika kwamba upo uwezekano wa mwili huo kuteketezwa kwa moto kwani makaburi hayo pia hutoa huduma hiyo.
Kama ulikuwa ni wosia wake kuteketezwa, basi kwa kanuni za Kanisa Katoliki zitafanyika mara tu baada ya ibada. Kwa kanuni za Kanisa Katoliki mwili uliolazwa kwa njia ya kuteketezwa kwa moto mabaki yake (majivu) hawapewi familia, kusambazwa au kugawanywa katika mafungu madogo madogo na badala yake ni lazima yawekwe ardhini au kwenye sehemu maalumu inayotumika kwa maziko ya namna hiyo, inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ya KLH.
Ballali ambaye amefariki akiwa amezungukwa na wingu kubwa la kashfa dhidi yake na dhidi ya taasisi aliyoiongoza inasemekana aliacha wosia uliotaka atakapofariki basi azikwe Marekani.
Hata hivyo, pamoja na kashfa nyingi zilizoandikwa na vyombo mbalimbali, hasa magazeti na kutangazwa majukwaani, Ballali hakuwahi kushtakiwa rasmi pamoja na kuwapo taarifa kwamba aliwahi kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Ballali ambaye ameacha mke na familia, amekuwa akitamka wazi kwamba hajawahi kuiba hata senti moja ya umma katika kipindi chote akiwa BoT na kuwashutumu watu aliowakwamisha kuwa chanzo cha kuandamwa kwake na tuhuma mbalimbali kabla ya kukataliwa kujiuzulu na hatimaye kufukuzwa na Rais Jakaya Kikwete.
Kifo cha Ballali kimetokea katika mazingira na wakati nchi ikiwa katika wimbi kubwa la tuhuma za ufisadi na misukosuko ya kisiasa, hali ambayo inazidisha utata wa kifo hicho kutokana na baadhi ya mambo kumgusa moja kwa moja marehemu.
Hali hiyo imesababisha watu wengi wakiwamo watu mashuhuri kuhoji uhalisia wa kifo hicho na kupendekeza kufanyika kwa uchunguzi huru na makini kuthibitisha kifo cha Ballali kabla ya kuzikwa kwake.
Marehemu Ballali alijiunga na Benki kama Gavana Julai 14 1998 hadi Januari 8, 2008.
Ballali ambaye alikwenda ghafla nchini Marekani mwishoni mwa mwaka jana akiwa na nia ya kurejea nchini, alikwama huko baada ya kubainika na matatizo makubwa tumboni kabla ya kulazwa hospitali na kufanyiwa upasuaji mkubwa.
Kwa mujibu wa habari hizo za awali, Ballali aliieleza familia yake kwamba alikuwa akihofia kula kitu chenye madhara makubwa hasa baada ya madaktari wa Marekani kumfanyia uchunguzi mara tu alipowasili nchini humo.
Wakati akiendelea na matibabu, Ballali aliandika barua kuelezea nia yake ya kuomba kujiuzulu kutokana na kuendelea kuzorota kwa afya yake huku akiwa bado na majukumu mazito ya kusimamia uchumi wa Taifa.
Hata hivyo, hakukuwa na taarifa zozote za upande wa serikali kuthibitisha kupokea barua ya kujiuzulu kwa Ballali siku kadhaa kabla ya serikali kutangaza matokeo ya ukaguzi wa kampuni ya nje iliyopewa kazi ya kukagua hesabu za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Ni baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza kupitia ripoti ya wakaguzi hao, ndipo alipotamka kumfuta kazi Ballali bila kuzungumzia lolote kuhusu kujiuzulu kwake.
Hata hivyo baadhi ya watumishi ndani ya BoT, walieleza wazi kwamba kabla hata ya taarifa za kujiuzulu na hatimaye kufutwa kazi kwake, Ballali aliondoka nchini akijua kwamba hatorejea tena nchini hasa baada ya serikali kuteua Manaibu Gavana wawili, Juma Reli aliyekuwapo na Profesa Prof. Benno Ndulu (ambaye aliteuliwa kuwa Gavana mpya).
Ballali amekuwa Gavana wa Benki Kuu kwa miaka saba na alielezwa kupatiwa matibabu katika hospitali moja mjini Boston, huko Marekani, lakini kabla ya kuanza tiba alikuwa nchini akipambana na shutuma nzito za ufisadi dhidi yake na taasisi ya umma anayoongoza.
Katika mkutano na waandishi wa habari makao makuu wa Benki Kuu Julai mwaka jana, Ballali alisema hawezi kujiuzulu na kwamba tuhuma dhidi yake ni za uzushi na uongo mtupu.
Pamoja na kukanusha kwake, Ballali alipata kuhojiwa na Takukuru kabla hajaondoka nchini, mahojiano ambayo yalielezwa kumkera kiongozi mmoja wa juu serikalini. Kiongozi huyo hayupo madarakani kwa sasa baada ya kujiuzulu kwa kashfa ya ufisadi.
KULIKONI-Ijumaa 23 Mei, 2008