Na Tundu Lissu usiku huu:
Waheshimiwa habari za usiku huu. Naomba kutoa updates juu ya kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chama Mh. Freeman Mbowe. Mimi na Katibu Mkuu Dkt. Vincent Mashinji tumeshuhudia sehemu ya sachi iliyofanyika nyumbani kwa Mwenyekiti kati ya saa tatu unusu na saa sita usiku huu. Kama nilivyosema kwenye ujumbe wangu wa awali, hii sio vita dhidi ya wafanya biashara ya madawa haramu bali ni vita ya kisiasa dhidi ya sisi wapinzani wa CCM na Rais Magufuli. Kwa uthibitisho wa kauli yangu naomba niwapatie orodha ya vitu walivyokamata polisi nyumbani kwa Mwenyekiti Mbowe. Vitu hivyo vimeorodheshwa kwenye fomu na. DCEA 003 inayoitwa 'Hati ya Ukamataji' iliyotolewa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kama ifuatavyo:
(1) Hati moja ya CHADEMA CHASO kwenda kwa Mwenyekiti ya tarehe 16/7/2013
(2) Picha mbali mbali nane za matukio ya uhalifu - picha za wahalifu wanaoharibu mali
(3) Hati moja ya Rasimu ya Kwanza ya CHADEMA kuhusu uundwaji wa Red Brigade
(4) Hati moja ya kurasa 13 inayoongelea mambo ya Muungano.
Hivi ndivyo vielelezo vilivyokamatwa nyumbani kwa Mwenyekiti vinavyothibitisha kwamba yeye ni muuza unga!!! Kama isingekuwa ukweli kwamba hivi ninavyoandika Mwenyekiti wangu yuko mahabusu Central, hiki kingekuwa kichekesho cha mwaka. Lakini Mwenyekiti anasota mahabusu usiku huu. Huu ndio ushahidi ambao Kamanda Sirro na polisi wake wamekuwa wanamtafutia Mwenyekiti wetu kwa amri ya Paul Makonda. Hatuna budi, katika hali hii, kuomboleza - kama alivyofanya Mwalimu katika kitabu chake 'Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania' - juu ya mahali ilikofikishwa nchi hii yetu. Nitawatumia picha ya orodha hiyo shortly.
Update: Mwenyekiti Mbowe aachiwa
Kama tulivyowajuza kwamba iwapo itatokea jambo lolote la umuhimu kujuzana kabla ya asubuhi tutafanya hivyo, tunapenda kuwatangazia wanachama wetu,wadau,wapenzi, na wapenda haki,amani na demokrasia ya kwamba Mwenyekiti Freeman Mbowe ameachiwa huru punde tu mnamo majira ya SAA saba na robo usiku huu.
Tunawashukuri wote kwa sala,maombi na subira na hivyo kuhitimisha salama SAA KUMI za Mwenyekiti wetu kuwa chini ya Jeshi la Polisi nchini katika kituo kikuu cha Polisi jijini Dar es salaam.
Taarifa za ziada juu ya jambo hili zitatolewa kesho.
Salum Mwalim
Naibu Katibu Mkuu
Chadema