Licha ya kwamba Profesa Safari ametaja sababu za kugombea Umakamu Mwenyekiti, nadhani huyu msomi hakutafakari kwa umakini na kwa kina, eti anataka kukomesha Ukanda, Udini, Ubaguzi wa rangi au Ukabila na Kijinsia, Umaskini na Ujinga pamoja na Ubadhirifu.
Kwanza kuhusu Ukanda, CHADEMA kilianzishwa na Mtei wa Kanda ya Kaskazini, lakini kwa juhudi kubwa za huyu Muasisi, akisaidiwa na waliomrithi na wanachama wengine, kimeenea nchi nzima: Kigoma, Kagera, Mwanza, Mara, Mbeya, Iringa, Ruvuma, Mtwara, Lindi na mikoa yote ya Pwani, Kati na Kaskazini kwao Mtei.
Kuhusu Udini, yeye mwenyewe Muislamu, na mgombea uenyekiti taifa ni Mkristo. Anataka nini cha zaidi ya
kushirikisha dini zote? Labda CHADEMA washirikishe wasio na dini (atheists) zaidi?
Ukabila na Rangi haviko Chadema. Hata sijui kabila la Prof. Safari, na nikiwa mpiga kura katika jimbo lake, namhakikishia kura yangu. Ubaguzi wa kijinsia hauko kabisa CHADEMA. Uliza wakina mama wa Chama.
Umaskini, Ujinga na Maradhi vinatushinda sisibsote, kutokana na ufinyu wa fedha na zana za kukabiliana navyo. Hilo ni tatizo la kitaifa kwa chama chochote cha siasa, hata CCM chama tawala, licha ya kwamba Ubadhirifu na Rushwa vikitokomezwa tutamudu zaidi majukumu hayo.
Kwa hiyo kwa jumla, Profesa ni vema ujue matatizo na kiini chake. Nina hakika uongozi wa sasa wa CHADEMA utanufaika, endapo juhudi zako za kujiunga nao kama Makamu Mwenyekiti, zitafanikiwa. Kila la kheri.