Wanajamvi salamu kwanza!
Nimekutana na mjadala mzito mtandaoni kuhusiana na msanii Diamond Platnumz kudaiwa kodi ya shilingi milioni 400 na TRA. Wengi wametoa maoni yao kwa hisia na jinsi ambavyo wanaweza na ni uhuru wao. Hata mimi nimeguswa kama alivyoguswa Profesa J na Mheshimiwa Mtolea (MB). Lakini kuna mambo nadhani kabla hatujajikita zaidi kutetea au hata kuhukumu inabidi tuyajue au tuwe informed nayo kabla hatujatetea au hata kushauri kwenye jambo kama hili.
Kwanza tujue kwamba Diamond anafanya biashara kwenye hii tasnia ya burudani hivyo ni wazi kuwa ni lazima alipe kodi kama wananchi wengine.
Swala linalobaki hapa ni kiasi cha kodi kwani kinaonekana ni kikubwa mno kwa maoni ya waliowengi humu jamvini. Lakini kabla hatujahitimisha hili ni lazima tujue Diamond anaingiza kiasi gani? Je ni aina gani hiyo ya kodi je ni income tax, entertainment tax, VAT etc.
Tukijua kiasi anachoingiza na aina ya kodi anayodaiwa, pia tulinganishe na wasanii wengine kama Ali Kiba, Lady Jaydee, Vanessa Mdee, Lina, Jux, Ben Pol, Mrisho Mpoto nk je wao wamelipa au wanadaiwa kiasi gani kutokana na pesa wanazoingiza tukijua haya tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kujaji kuwa ama Diamond Platnumz anaonewa au anastahili kulipa hiyo kodi.
Mwisho nishauri serikali sasa ni wakati wa serikali kuwekeza nguvu zake kwenye kuboresha na kusaidia kukuza sanaa. Kama msanii mmoja mnaweza kumdai milioni 400 ni wazi sasa kwamba tasnia hii inaweza kuisaidia nchi kuingiza kipato kwa taifa na taifa likanufaika.
Chukulia mfano milioni 400 inaweza kujenga dispensari ngapi kule Kolomije? Je, ni shule ngapi za kata zinaweza kujengwa? Je, kama wasanii hawa walio wengi kama kumbikumbi wakitengenezewa mazingira mazuri yatayowafanya wao pia wanufaike na kazi za mikono yao lakini taifa pia likaingiza pato hatutafika tunakotaka?.
Nishauri serikali sasa kuondokana na mawazo ya kuitazama sanaa na wasanii kama watu fulani wahuni na kuwadharau bali tuwathamini na kuwawezesha tutafika mbali zaidi.
CC; Mwakyembe,
By Zawadi B. Lupelo