Dkt. Evaline Munisi: Ughaibuni Loan ni hatua ya kujenga imani mpya kati ya Serikali na vijana wa Kitanzania

Dkt. Evaline Munisi: Ughaibuni Loan ni hatua ya kujenga imani mpya kati ya Serikali na vijana wa Kitanzania

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
5,352
Reaction score
15,876
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Wilbard Munisi amesema uzinduzi wa Ughaibuni Loan si uzinduzi wa mkopo pekee, bali ni hatua ya kujenga imani mpya kati ya Serikali na vijana wa Kitanzania, hasa vijana wenye ujuzi wanaotamani kutumia fursa za ajira nje ya nchi lakini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kifedha katika kuanza safari yao.

Amesema Serikali, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mazingira ya kuziba pengo hilo kwa kuwawezesha vijana kupata fursa za ajira katika soko la kimataifa. Kwa mujibu wa takwimu alizozitoa, Watanzania 14,613 wameajiriwa nje ya nchi tangu mwaka 2022, huku 8,408 wakiwa wamepata ajira katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, jambo linaloonyesha kasi ya ongezeko la fursa za ajira za kimataifa kwa Watanzania.

Dkt. Munisi amesema Tanzania sasa inalenga kujijenga kama nchi inayotoa nguvu kazi iliyoandaliwa, salama na inayowajibika, badala ya kuwa chanzo cha nguvu kazi isiyo na mfumo. Amesisitiza kuwa hatua hiyo inaenda sambamba na nafasi ya Tanzania katika uongozi wa Jukwaa la Mawaziri wa Kazi la Ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, pamoja na maandalizi ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa Afrika na nchi za Ghuba utakaofanyika Dar es Salaam mwezi Oktoba kujadili mustakabali wa ajira duniani.

Aidha, ametoa msisitizo kuhusu usalama wa Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi, akionya dhidi ya watu wanaoweza kutumia fursa hiyo kuwatoza vijana gharama kubwa zisizo halali au kuwaingiza katika njia za magendo. Amesema ulinzi wa Mtanzania popote alipo ni wajibu wa Serikali, hivyo mifumo ya ajira za kimataifa inapaswa kwenda sambamba na usalama, uadilifu na uwajibikaji.

Kwa mtazamo wa Dkt. Munisi, Ughaibuni Loan inapaswa kutazamwa kama zaidi ya msaada wa kifedha; ni mlango wa fursa unaolenga kuwasaidia vijana wenye uwezo kuingia katika soko la ajira la kimataifa. Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imechukua hatua ya kufungua mlango huo, huku vijana wenyewe wakibeba jukumu la kuutumia kwa uadilifu na kuhakikisha fursa hiyo inaleta matokeo chanya kwao, familia zao na Taifa kwa ujumla.
 
Back
Top Bottom