View attachment 1440056
Aliwayewahi kuwa Mbunge wa Ubungo na Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Dkt.
Masumbuko Lamwai amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Mei 05, 2020.
Dkt. Lamwai atakumbukwa kama Mwanasiasa machachari, Mwanasheria nguli na Mkufunzi Mwandamizi (senior lecturer) wa Tumaini University.
Akiwa NCCR-Mageuzi, alikuwa na wanasiasa wengine wakongwe kama Mabere Marando, Marehemu Dk Sengondo Mvungi (RIP), Augustine Mrema, Makongoro Nyerere, Prince Bagenda, Ndimara Tegambwage, Stephen Wassira na wengine wengi.
Katika Uchaguzi Mkuu wa Vyama Vingi wa 1995, NCCR-Mageuzi walitetemesha na kutingisha nchi mpaka Mwl Nyerere akaingilia kati baada kusimama majukwaani CCM.
Baadae alijivua uanachama wa NCCR na kuhamia CCM.
Mwenyezi Mungu amjalie pumziko la amani.
MDOGO WA MAREHEMU DKT. LAMWAI, MH. JOSEPH SELASINI AZUNGUMZIA KIFO CHA KAKA YAKE
Kupitia mahojiano yake na kituo cha East Africa Radio asubuhi ya leo, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini ameeleza hivi:
Dk Lamwai ni kaka yangu. Ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia ya Mzee Roman Selasini na Mama Katarina Roman.
Na kama kiongozi wa familia ametuongoza kwa hekima na busara mpaka mwisho wa uhai wake. Kama mtoto wa kwanza, ametutengenezea misingi mizuri katika familia.
Alikuwa ni mwanasheria aliyebobea katika mwenendo wa mashitaka pamoja na ushahidi (evidence and civil procedures)
MBUNGE PEKEE WA UPINZANI
Katika maisha yake ya kisiasa alipata kuwa diwani wa Manzese mwaka 1995 na baadaye alikuwa ni mbunge wa Ubungo na alikuwa mbunge pekee wa upinzani. Nakumbuka mwaka 1995 Tume ya Uchaguzi ilipofuta uchaguzi wa Mkoa wa Dar es Salaam yeye hakuafiki akaendelea na kumshinda marehemu Venance Ngula wakati huo. Alidumu kwa miaka miwili na baadaye mahakama ikatengua ubunge wake.
Kipindi kilichofuata Mh. Benjamin Mkapa alimteua kuwa Mbunge wa kuteuliwa na Rais. Hiyo ilikuwa baada ya kurejea CCM kutokea NCCR-Mageuzi. Amefariki akiwa ni mwanachama wa Chama cha Mapinduzi.
ALIKUWA HODARI, MWENYE MSIMAMO NA USHIRIKIANO
Namfahamu kama mtu hodari, mtu aliyekuwa na misimamo. Mtu ambaye alikuwa akikusudia jambo lake anapambana nalo mpaka ahakikishe limefika mwisho. Ni mtu alikuwa determined kwaakweli.
Alikuwa anashirikiana na watu kufanya jambo. Hata sisi wadogo zake alikuwa akituagiza hasubirii mrejesho, bali munakwenda wote.
Tumepata pengo kubwa katika familia. Tulipotelewa na wazazi na yeye alibaki kuwa kiongozi wetu na sasa ameondoka. Ni pengo ambalo halizibiki.
ALIPENDA KAZI YA UALIMU
Alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alianzisha kampuni yake ya Uwakili inayoitwa Lamwai Advocates. Amefanikiwa kuwasomesha watoto wake wote wanne (4) ambao ni mawakili na wanashughulika na hiyo ofisi yake.
Baada ya kutoka Chuo Kikuu alikuwa ni mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Tumaini - Dar es Salaam. Aliendelea na kazi hizo mbili: Kuendesha kampuni yake pamoja na hiyo ya Uhadhiri.
Kazi ya ualimu aliipenda sana. Ni kazi ya familia. Familia yetu ina wanasiasa wengi sana na walimu wengi. Kwahiyo alipenda sana kusomesha mpaka mwisho wa uhai wake.
AFYA KUDHOOFU NA UMAUTI
Afya yake ilidhoofu katika kipindi cha wiki mbili tatu zilizopita. Lakini pamoja na kudhoofu huko, alipigwa na malaria kali ambayo alikuwa anaendelea kupata dawa.
Hata Jumapili alikaa na watoto wake wakaongea sana ni vile tu hauwezi kujua Mungu amepanga nini. Jana usiku akazidiwa na katika safari ya kumpeleka hospitali, akafia njiani.
Kwa sasa mwili umehifadhiwa Hospitali ya jeshi Lugalo jijini Dar es salaam.
=====
SOMA: BAADHI YA KESI ALIZOWAHI KUSIMAMIA
Jinsi mbunge Ramadhan Kihiyo alivyojiuzulu baada ya kashfa ya kufoji vyeti - JamiiForums
Mbunge wa Longido Onesmo Nangole (CHADEMA) huenda akavuliwa ubunge kwa kufoji elimu - JamiiForums
Sarah Simbaulanga: Mwanamke wa kwanza kuiba pesa ndefu katika historia ya benki zote nchini - JamiiForums