Mungu Baba wa mbinguni, pengine naweza kuwa sistahili mbele zako kuleta maombi haya kwako kutokana na mapungufu yangu, lakini katika hili Baba Mungu nakuomba usiyatizame mapungufu yangu bali ukusikie kuomba kwangu.
Mungu mwenye enzi Mungu mkuu, Tia mkono wako juu ya kiumbe wako huyu Tundu Lissu kama ulivyomuinua mwanao baada ya shetani kushindwa, Mungu baba wafanye mashetani haya yashindwe vile vile kama yalivyoshindwa kwa mwanao mpendwa Yesu Kristu.
Tundu Lissu amekuwa akiifanya kazi yako kwa kuwakemea mafalisayo na wakuu wa sheria bila woga kama alivyofanya mwanao mpendwa, Baba usiruhusu washinde bali uwaoneshe kwamba huyu anaifanya kazi inayokupendeza wewe na kwamba saa yake haijafika ya kumuondoa kwenye kazi yake uliyompa kwa ajili yetu.
Mpe uzima mpe uponyaji wako ili wapate kujua kuwa shetani hana mamlaka juu ya kiumbe wako hata kama wamemmiminia risasi zaidi ya ishirini, umemkinga Baba kwa muujiza wako maana bila hivyo hata hospitali asingefika akiwa hai kama walivyodhamiri hao shetani.
Nakutumaini Mungu maana hujawahi kuniangusha, nisikie na katika hili wapate kutambua kwamba shetani atendaye kinyume na kazi zako daima hatofanikiwa.
Ahsante Mungu Baba kwakuwa umenisikia na umenipa kibali kuyaomba haya kwako. Ni katika njia ya Yesu Kristu ninakushukuru.
Aamina.