Profesa Mkumbo ni miongoni mwa maprofesa wenye umri mdogo nchini, ambaye ni chapakazi na mpiganaji kielimu na kimaisha aliyeanza kazi mwaka 2001 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) akiwa Ofisa Tawala na pia alikuwa mwanafunzi wa shahada ya pili ya Saikolojia chuoni hapo.
Safari ya maisha ya Profesa Mkumbo ilipitia mambo mengi, ikiwa ni pamoja na malezi yasiyo na wazazi. Juni 21, mwaka 1971, ndiyo siku aliyozaliwa huko kijijini Mgela, Iramba mkoani Singida."Kwa bahati mbaya wazazi wangu walitengana mapema na kuondoka nyumbani nikiwa bado mdogo chini ya umri wa miaka mitatu, hivyo nililelewa na bibi na mjomba wangu," anasimulia Profesa Mkumbo.
Pamoja na changamoto hiyo, walezi wake walijitahidi kumlea ambapo alianza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mgela na alipokuwa darasa la nne ndipo alipomfahamu mamaye, ila mamaye huyo alifariki muda mfupi baada ya kumfahamu.
Jambo hilo likawa tatizo kwake, kwani aliendelea kuishi na walezi wake na kwamba katika familia yake walizaliwa wawili. Yeye na dada yake ambaye hivi sasa ameolewa na anaishi na familia yakehuko Mombasa, Kenya.
Anasema kwa kuwa alizoea kuishi na bibi na mjomba, maisha yaliendelea na yeye alijitahidi kwenye masomo kwa kuwa aliamini mkombozi wake ni elimu.
Jitihadazake za masomo zikazaa matunda, kwani alipomaliza elimu ya msingi alichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Mwenge, alikosoma kidato cha kwanza hadi cha nne."Nilisomeshwa na walezi wangu kwa msaada pia wa wasamaria, kwani sikumfahamu baba yangu wakati huo na wakati nimemfahamu mama, naye akafariki muda mfupi tangu nimjue," ni kauli ya Profesa Mkumbo.
Jambo hilo likaendelea kumpa nguvu Mkumbo na kuongeza juhudi kwenye masomo ambapo baada ya kumaliza kidato cha nne alifaulu na kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Pugu kwa masomo ya sayansi."Hapo nikapata furaha, nilifahamu mwanzo wa safari ya mafanikio imewadia, nilifurahi sana na nikaendelea kusaidiwa na wasamaria na walezi wangunikaenda shuleni Pugu", anasisitiza Profesa Mkumbo.
Juhudi zake zikawa zile zile kwani aliamini kusoma kwa malengo ndiko kutakakomkomboa kimaisha na hapo akaongeza juhudi iliyomfanya afaulukidato cha sita na kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomaShahada ya Sayansi kwenye Elimu na kuhitimu mwaka 1999.
Hakuishia hapo, mwaka 2001 alipoajiriwa chuoni hapo alikutana na mkewe huyo na kufunga ndoa mwaka huo huo. Mkewe ambaye ni Ofisa Tawala chuoni hapo, amekuwa msaada mkubwa kwa Profesa Mkumbo, ambaye kila wakati anamsifia kwa kumfanikishia na kusisitiza kwamba nguvu kuu ya mafanikio ni huyu mkewe.
"Kwa kweli mke wangu ndio mafanikio yangu, nampenda sana, yeye ndiye aliyefanikisha nikafika hapa na leo nimepata uprofesa, yote ni kwa ajili ya juhudi na msaada wake mkubwa katika familia yetu", alisema Profesa Mkumbo.
Akiwa msomi na pia mmoja wa waanzilishi wa Chama kipya cha Siasa chaACT-Tanzania baada ya kuenguliwa Chadema, Profesa Mkumbo amepitia mambo mengi na changamoto mbalimbalikatika maisha.Baada ya kuajiriwa chuoni hapo kama Ofisa Tawala, wakati huo alikuwa anasoma shahada ya pili ya Saikolojia chuoni hapo na alihitimu mwaka 2002.
Ilipita mwaka mmoja tu tangu amalize masomo yake hayo na yeye akahamishiwa kwenye Idara ya Taaluma akiwa Mhadhiri Msaidizi.Kupenda kwake masomo kulimfanya aende kusoma tena Shahada ya Falsafa ya Udaktari (PhD) ya Saikolojia katika Chuo cha Southampton, Uingereza.
Anasema kipindi hicho akisoma Uingereza, ndipo baba yake mzazi alirejeanyumbani mwaka 2005 na alifariki muda mfupi wakati huo yeye alikuwa masomoni.
"Baba yangu mzazi alirudi nyumbani, ila wakati huo mimi nilikuwa masomoni Uingereza mwaka 2005, na alifariki muda mfupi, hapo ukawa mwisho wa uhai kwa wazazi wangu wote," alisemaProfesa Mkumbo.
Tukio hilo halikukatiza masomo yake, kwani alifanikiwa kumaliza masomo yake mwaka 2008 na kurejea nchini kuendelea na kazi chuoni UDSM, ambapo alipanda cheo na kuwa Mhadhiri Mwandamizi mwaka 2011.
Maisha yake na siasa Wakati huo akiendelea na taaluma yake, pia alipendasiasa na kwamba alishawahi kuwa mwanachama cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) hadi mwaka 2005. Mapenzi yake kwenye siasa yakahamia Chadema, ambako alidumu kwa miaka kadhaa hadi mwaka 2013 alipofukuzwa uanachama akiwa Mjumbe muhimu wa Kamati Kuu yachama hicho.
"Nimekuwa nikifanya siasa kama sehemu ya harakati, niliwahi kuwa CCM, na nilihamia Chadema sio kwa sababu ni chama bora kuliko CCM, la hasha! Niliamini kujiunga kwangu huko kuna fursa ya kujenga chama, na tulifanikiwa kweli na kuifanya Chadema kuwa mstari wa mbele kiitikadi na kisera," alisema.
Na kwamba kwa bahati mbaya ile nia yaoya kuibadilisha Chadema kiuongozi ilishindwa na hivyo akaishia kufukuzwa uanachama. Profesa Mkumbo aliwahi kuwa Mkuu wa Idara chuoni hapo mwaka 2009 hadi 2011, pia kuwa Mkuu wa Kitivo cha Elimu katika Shule Kuu ya Elimu Dar es Salaam (DUCE), Julai 2012 hadi Novemba 2013 alipojiuzulu.
Kuhusu ACT-Tanzania Akizungumzia kuhusu chama kipya cha ACT-Tanzania, ambacho kimeanzishwa hivi karibuni, Profesa Mkumbo anasema yeye ni miongoni mwa waanzilishi na kwamba Watanzania watarajie mengi mazuri, kiuongozi, kiitikadi, kisera na hata kifalsafa.
Anabainisha kuwa wanatengeneza chamakitakachobadilisha na kuondosha dhana ya kwamba vyama vingi ni ubabaishaji, uhuni, upatukaji na uropokaji.
"Tunajenga chama chenye nidhamu, kiuongozi, kisera, kiitikadi na kimtazamo, wananchi wataona na kushuhudia hayo na hivyo tuna imani tutaendelea kupata wanachama wengi zaidi", anasema Profesa Mkumbo.
Kuhusu kupata ngazi hiyo ya uprofesa, Mkumbo anasema anashukuru kwa Baraza la Wasomi chuoni hapo kuona kazizake na kutambua mchango wake katika jamii, hivyo kumpandisha ngazi hiyo kutoka udaktari hadi uprofesa.
Kupanda kwake ngazi kulitangazwa Agosti11, mwaka huu na baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kwamba Makamu Mkuu wa UDSM (Taaluma), Profesa Makenya Maboko alisema Dk Mkumbo nawenzake wamepata hadhi hiyo.
Hata hivyo, taarifa kamili itatolewa wiki inayoanza kesho kuhusu kazi alizofanya na alama alizopata hadi akafanikiwa kupanda ngazi hiyo. Profesa Mkumbo ni baba wa watoto watatu, wa kiume wawili mmoja mwenye umri wa miaka 11, na mwingine miaka minane na wa kike.