Maudhui ya uzi huu ni kwamba Zitto na Chama Chake Cha ACT hawana nia ya dhati ya kuletea wananchi mabadiliko au mageuzi katika maisha yao kisiasa, kiuchumi na kijamii. Badala yake, Zitto na genge lake la ACT ni chama cha watibuaji wa harakati hizo. Zitto na genge lake la ACT kazi yao kubwa ni moja tu, nayo ni kukisaidia CCM kibaki madarakani. Ushahidi juu ya hili upo na umeujadiliwa kwa muda mrefu humu jamvini kwa mfano, kauli za wenzake Zitto huko nyuma (
Kitila Mkumbo na Mwigamba) kwamba lengo la ACT ni kuwa chama kikuu cha upinzani nchini (na sio kuwa chama tawala), huku wakielezea kwa ufasaha kabisa kwamba adui namba moja wa ACT ni Chadema. Hata kauli za viongozi wa sasa wa ngazi ya juu wa ACT Mwenyekiti wa ACT taifa, Anna Mugirwa na Zitto Kabwe ambae
Nguruvi3 amejitahidi kutuelezea jinsi gani kwa nafasi hii, Zitto amejitwalia madaraka ya kuwa a Supreme Leader wa chama cha siasa, viongozi wote hawa wawili wameonyesha wazi na kwa dhati kabisa kwamba adui yao namba moja ni upinzani uliopo sasa na sio chama tawala.
Tuanze na Zitto, hasa jinsi gani asivyokuwa mpenda mageuzi kwa dhati, jinsi gani alivyo mvurugaji na vile vile jinsi gani anatumika kama mpini wa CCM kumaliza upinzani uliopo sasa nchini. Katika mahojiano yake hivi karibuni na kituo cha televisheni cha EATV, Zitto alinukuliwa akijadili kwamba
Chama changu kitapigania kufa na kupona majimbo matatu ya uchaguzi jijini Dar-es-salaam. ZItto akaenda mbali na kuyataja majimbo hayo kwamba ni Kawe, Ubungo na Segerea. Mpenda mabadiliko au mageuzi yeyote atakubaliana nasi kwamba moja ya kazi kubwa inayokabili vyama vya upinzani nchini ni kunyakua majimbo ya uchaguzi yaliyopo DSM na pia kwamba kufanikiwa katika hilo ni hatua muhimu sana katika kuleta mabadiliko ya kweli nchini.
Sote tunajua pia kwamba Dar-es-salaam ina majimbo mengine mengi nje ya matatu anayotaja zitto. Zitto anataja Kawe, Ubungo na Segerea lakini hasemi kwamba yapo mengine ambayo ni Ilala, Kigamboni, Temeke Kinondoni na Ukonga. Hakuna mjadala kwamba majimbo haya bado ni ngome ya Chama cha Mapinduzi, ngome ambayo upinzani unatakiwa kuivunja. Lakini muhimu zaidi ni kwamba ni jambo lisilo na mjadala kwamba majimbo matatu anayolenga Zitto kuweka wagombea wake kutoka chama cha ACT, yani (Kawe, Kinondoni, Ubungo), hizi ni ngome za Chadema ambazo zilipiganiwa kwa juhudi kubwa na chadema pamoja na watafuta mabadiliko. Lakimi cha ajabu ni kwamba, Zitto ananukuliwa akisema kwamba
Chama changu kitafia au kitaimarika kusimamisha wagombea katika majimbo haya kwa gharama zote.
Maswali ya kujiuliza:
1. Je, kama kweli ACT sio Mpini wa Kumaliza upinzani nchini, kwanini Zitto mchana kweupe ataje majimbo ya Kawe, Ubungo na Segerea ambayo ni ngome za Chadema lakini hasemi kwamba ACT inasimamisha wagombea kwenye majimbo mengine ya DSM ambayo ni ngome za CCM kwa maana ya Kinondoni, Temeke, Ilala, Ukonga na Kigamboni?
2. Je, kuna haja gani ya kuondoa wabunge waliopo katika Majimbo ya Ubungo, Kawe na Segerea hivi sasa?
Ubungo ni jimbo linaloshikiliwa na John Mnyika, Kawe ni Jimbo linaloshikiliwa na Halima Mdee, na Segerea ni Jimbo ambalo Chadema ilishinda uchaguzi wa 2010 lakini matokeo yakachukuliwa. Segerea ni jimbo ambalo wapiga kura wake wanasubiri kulikabidhi kwa Chadema na ushahidi juu ya hili upo wazi.
Suala lingine muhimu kujadili ni lile la Zitto na UKAWA. Ikumbukwe kwamba Zitto alitamka wazi kwamba UKAWA ni genge la wasaka madaraka na kwamba hawezi kujihusisha nalo. Tafsiri rahisi hapa ni kwamba kwa Zitto, UKAWA ilikuwa ni tishio na sio fursa. Je ni kwanini wakati katika hali ya kawaida, mtafuta mabadiliko yoyote kwake yeye UKAWA ni fursa? Inavyoelekea, upeo wa Zitto juu ya agenda ya UKAWA ilikuwa ni kwamba, UKAWA ulilenga kugawana madaraka ya kisiasa. Kwa maana hii basi, Zitto hakuwa tayari kugawana madaraka na wana UKAWA kwani wangempunja alichokuwa anakitaka. Kama tupo sahihi hadi hapa, basi nadhani tutakubaliana kwamba mtu wa aina hiyo moja kwa moja ni mroho wa madaraka. Isitoshe, ndio maana tayari tumeshaona jinsi gani Zitto alivyoamua kujitwalia madaraka ndani ya ACT kinyume na utaratibu na pia kinyume na utamaduni wa siasa za vyama, suala ambalo
Nguruvi3 kalijadili kwa ufasaha. Wakati wana UKAWA wanaunganishwa na viongozi ambao ni wenyeviti wa vyama vyao, Zitto na ACT yake anakuja na upinzani mpya ambao unaongozwa na Supreme Leader. Hili ni doa kubwa sana kwa demokrasia yetu changa kwani katika uongozi wa kisiasa, dunia imepata uzoefu wa kutosha na supreme leaders wa aina ya Hitler, Musolini, Stalin, North Korea, n.k. Zitto anaelekea kujiunga na orodha hiyo.
Mwisho ni muhimu tukajikumbusha kwamba huko nyuma zitto alinukuliwa mchaka kweupe akisema kwamba:
Siwezi Kujiunga na UKAWA kwa kuwa baadhi ya viongozi wake hawataki muungano. Wamejificha nyuma ya pazia la muundo wa serikali tatu.
Zitto akaendelea kujadili kwamba:
Msimamo wangu siyo kuwa na marais watatu kwa sababu najua msimamo wa marais watatu utavunja nchi. Msimamo wangu ni Rais mmoja wa jamhuri ya muungano, Mkuu wa serikali ya Zanzibar na mkuu wa serikali ya Bara.
Ni wazi kwamba msimamo wa Zitto wa kukataa serikali tatu ni msimamo ambao unapingana na maoni ya wananchi walio wengi waliyoyatoa mbele ya tume ya jaji warioba. Msimamo wa Zitto wa kukataa Serikali tatu ndio msimamo wa CCM ambao umekwamisha mchakato wa Katiba Mpya. Msimamo wa Zitto ambao ndio ule ule wa CCM ulienda sambamba na vitisho kwamba umma ukiridhia mfumo wa serikali tatu, jeshi litapindua serikali.
Kwa kuhitimisha, mtu yeyote ambae ana nia ya dhati ya kuiondoa CCM madarakani atafanya kila linalowezekana kuzuia hujuma dhidi ya Upinzani ulipo sasa (Ukawa). Mtu wa aina hiyo atakaa mbali kabisa na majimbo ambayo yanangara kutokana na uwepo wa wabunge (wa upinzani), wabunge wachapa kazi na waliokuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya taifa letu linalozidi kuteketea. Mtu wa aina hii atakaa mbali kabisa na hujuma dhidi ya UKAWA kuelekea uchaguzi mkuu kwani kitendo cha Zitto na ACT kupinga UKAWA kinalenga kuleta mnyukano baina ya ACT na UKAWA ili iwe rahisi kwa CCM kupenya katikati ya vumbi hilo na kurudi madarakani baada ya uchaguzi mkuu.
Kuna kila sababu ya wananchi waelewa kumkataa zitto na genge lake.