Katika Gazeti la Raia Mwema la April 8, 2015 toleo namba 500, Prof. Kitila Mkumbo anajadili dhana ya Kiongozi Mkuu wa Chama, ndani ya ACT. Hii ni kwa sababu, umma umebakia kuduwaa kufuatia Chama chao cha ACT kuja na muundo mpya ambapo ACT itakuwa na Kiongozi mkuu wa chama sambamba na mwenyekiti wa chama Taifa. Kwa mujibu wa
Kitila Mkumbo, maamuzi hayo yamelenga kuepuka kutengeneza chama dola. Kitila anaendelea kujadili kwamba nchi nyingi barani Africa zimekuwa na vyama dola, suala ambalo limeathiri demokrasia. Anaenda mbali zaidi na kuja na mifano ya nchi kama Uingereza na Afrika ya kusini. Kwa mfano, anasema , namnukuu Nchini Uingereza, chama cha Conservatives kina kiongozi mkuu wa sasa, David Cameroon, huku wenyeviti wake wakiwa ni Grant Shapps na Lord Feldman. Vile vile, Kiongozi wa chama cha Liberal Democrats ni Nick Clegg, na Mwenyekiti wake ambaye pia anaitwa Rais ni Sal Brinton. Nchini Afrika ya Kusini, Kiongozi wa chama cha ANC ni Jacob Zuma, huku Mwenyekiti wake akiwa ni Bi. Baleka Mbete, ambae pia ni Spika wa Bunge la Afrika ya Kusini.
Kitila anaendelea kujadili kwamba Chama Tawala Tanzania (CCM)ni mfano wa chama dola,kwani muundo uliopo ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) ni muundo ambao umeshindwa kutenganisha mwenyekiti wake na kiongozi wa serikali, hivyo kufanya CCM kuwa ni chama dola. Hivyo basi, kwa mujibu wa Kitila, muundo mpya wa ACT unalenga kuondoa dhana ya udola katika chama chao cha ACT.
Tujaidili hoja hii ya Prof Mkumbo:
Kwanza: Udola wa chama ni suala la mfumo ambao unatambulika kwa mujibu wa katiba Ya chama husika cha siasa. Inaonekana kana kwamba Kitila hajafanya utafiti vizuri kufahamu ili kuwa chama dola, sio lazima chama husika kiwe kimekamata madaraka ya nchi. Kinaweza kuwa ni chama ambacho hakijawahi kuongoza serikali, lakini pia kinaweza kuwa ni chama kipya kabisa katika anga za kisiasa ndani ya taifa husika, lakini mfumo wake ukakifanya kuwa ni chama dola, kwa mujibu wa katiba ya chama.
Pili, muundo wa chama dola ni muundo ambao uliasisiwa na chama cha mapinduzi nchini Tanzania. Ni muundo huu ndio chama cha ACT aidha kwa kujua au kutojua, kimeamua kuiga. Tukiangalia Katiba za vyama vya CCM na ACT, katiba zote zinataja uchama dola. Kwa mfano, kwenye katiba ya CCM, mwenyekiti wa chama taifa ndiye huyo huyo Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania. Mwenyekiti huyu mwenye kofia ya urais wa nchi ndiye anayeongoza vikao vyote vizito ndani ya chama kwa maana ya vikao vya CC, NEC na Mkutano mkuu wa taifa. Mwenyekiti huyu wa chama ambae pia ni Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuteua viongozi wakuu wa chama ngazi ya taifa kuanzia Katibu mkuu wa chama, manaibu na viongozi wa idara mbalimbali ndani ya chama. Pia ana mamlaka ya kuteua watu anaopenda wawepo katika kamati kuu ya chama (CC)Nguvu hii ni karibia sawa na nguvu ya kifalme kwani nafasi aliyonayo ya uenyekiti kamwe haishindanishwi na kupatikana kwa njia ya demokrasia. Kinachotokea ni kwa wajumbe wa mkutano mkuu kupiga kura ya ndiyo au hapana, basi.
Ukiangalia kwa undani, udola uliopo CCM hauna tofauti yoyote ya msingi na nafasi ya kiongozi mkuu wa chama cha ACT,
Zitto. Kama ilivyo kwa mwenyekiti wa CCM taifa ambae pia ni rais wa wa nchi, Kiongozi mkuu wa ACT Taifa, Zitto ndio kila kitu ndani ya chama na hakuna nguvu wala mamlaka yoyote ile ambayo inaweza kushindana nae. Kama ilivyokuwa kwa CCM, kwa ACT pia, Madaraka na mamlaka yote yamelundikwa mikononi mwa kiongozi mkuu wa Chama Taifa. Hivyo basin i muhimu Kitila akaacha kuadaa umma kwani ACT ni chama dola kwani kama tulivyojadili awali, udola wa chama hautokani na chama hicho kuwa madarakani, Udola wa chama ni suala la kimfumo zaidi kwa mujibu wa katiba ya chama.
Tukija kwenye hoja ya Kitila ambayo inafananisha ACT na vyama vya nchi za wenzetu, pengine Kitila hana taarifa kwamba vyama vya conservatives na liberal democrats kwa upande wa Uingereza na chama cha ANC kwa upande wa Afrika ya kusini, vyama hivi havina title ya uongozi inayoitwa Kiongozi Mkuu Wa Chama, badala yake, vyama hivi vina cheo kinachoitwa Kiongozi wa Chama. Tofauti na wenzetu hawa wa nje, ndani ya katiba ya ACT, hakuna kipengele kinachoeleza jinsi gani nguvu za Kiongozi Mkuu wa chama zinaweza kudhibitiwa. Mamlaka ya aina hiyo haipo ndani ya Katiba ya ACT. Kwa maana hii, mkakati wa akina Kitila Mkumbo, Samson Mwigamba na wenzake uliilenga kumtengenezea Zitto ufalme ndani ya ACT. Mfumo huu uliandaliwa kwa ajili ya mtu mmoja tu, Zitto Kabwe. Chama cha aina hii ni cha kuogopa kama ukoma kwani kinajenga udola hata kikiwa bado hakijapewa ridhaa na wananchi kuongoza nchi.
Wengi bado tunakumbuka vyema jinsi gani Mkumbo, Mwigamba na wenzao walivyokuja na waraka ambao uliwatuhumu viongozi wa chadema kitaifa kwamba ni madikteta. Ukweli unabakia wazi kwamba hadi leo, hakuna kiongozi ndani ya Chadema ambae amewahi kujiundia genge kama la akina Zitto na wenzake. Isitoshe, Katibaya chadema haielekezi kwamba Mwenyekiti au Kiongozi Mkuu wa Chama ndiye atakayegombea urais. Tumeshuhudia kwamba nafasi ya urais inaweza kwenda kwa mwanachama yoyote mwenye sifa. Kwa mfano, Dr. Slaa hajawahi kuwa mwenyekiti au kiongozi mkuu wa Chadema lakini badi ni Kiongozi ambae hadi sasa ndiye anayeaminiwa zaidi katika mbio za urais kwa tiketi ya chadema.
Kwa hiyo anachofanya kitila mkumbo ni upotoshaji wa makusudi kabisa kwani hakuna ukweli wowote kwamba kutenganisha uenyekiti wa chama taifa na nafasi ya kiongozi mkuu wa chama ni kuondoa udola wa chama. Wanachofanya akina kitila ni kupandikiza mbegu ya udikteta. Hatudanganyiki.