EPA kortini Kisutu
na Happiness Katabazi
HATIMAYE watuhumiwa 10 wa wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam chini ya ulinzi mkali wa polisi, kwa tuhuma za wizi huo.
Watuhumiwa hao, walifikishwa mahakamani hapo saa 4:35 asubuhi na kupitishiwa mlango wa nyuma wa mahakama hiyo na kisha kuhifadhiwa kwenye chumba cha waendesha mashitaka kwa ajili ya kuandaliwa mashitaka yao.
Watuhumiwa hao walivuta hisia za wengi na kusababisha wananchi kufurika katika chumba namba moja ambapo kesi mbalimbali za washitakiwa hao zilianza kusomwa saa 7:24, huku, makachero wa polisi wakiwa wametanda kila kona ya mahakama hiyo.
Mshitakiwa wa kwanza kusomewa mashitaka hayo, alikuwa Johnson Mutachukurwa Lukaza na Mwesiga Rutakakyamilwa Lukaza, ambaye hata hivyo mshitakiwa wa pili hakuwepo mahakamani.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Mnyanda, mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Euphemia Mingi, alidai kuwa washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka matano, yakiwemo ya kughushi, wizi na kujipatia ingizo la fedha kwenye akaunti kwa njia ya udanganyifu ambazo ni mali ya BoT.
Wakili Mnyanda alidai kwamba kati ya mwaka 2003 na Desemba saba mwaka 2005, jijini Dar es Salaam, watuhumiwa hao wote kwa pamoja waliiba, sh 6, 300, 402, 224. 64 kwa madai kwamba wao ni wamiliki wa Kampuni ya KERNEL LIMITED ambayo imeteuliwa kukusanya madeni ya Kampuni ya Maruben Corporation ya Japan.
Washitakiwa hawa wanatetewa na wakili wa kujitegemea, Alex Mgongolwa.
Hata hivyo walikana mashitaka yote matano na upande wa mashitaka ulisema dhamana ipo wazi na Hakimu Mingi alitoa dhamana kwa mshitakiwa huyo kwa masharti kwamba kila mshitakiwa, alipe nusu ya fedha anazotuhumiwa kuiba, yaani sh bilioni tatu, wadhamini wawili, ambao watatoa bondi ya sh sh bilioni 150 au kuleta mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Pia mshitakiwa haruhusiwi kutoka nje ya jiji bila ruhusa ya mahakama na kuwasilisha hati yake ya kusafiria mahakamani.
Na upande wa mashitaka ulidai kwamba upelelezi umekamilika hivyo wanaiomba mahakama iwapangie tarehe ya siku ya kutaja ambapo Hakimu Mingi aliahirisha shauri hilo hadi Novemba 18 mwaka huu.
Hata hivyo ilipoitimu saa 12 jioni, mshitakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana, hivyo alipelekwa rumande hadi leo atakapofikishwa mahakamani hapo tena kwa ajili ya kuja kutimiza masharti hayo.
Katika hatua nyingine watuhumiwa wengine wanne wenye asili ya Kiasia Jayantkumar Chandubhai Patel Jeetu Patel, Devendra K. Vinodbhai Patel, Amit Nandy na Ketan Chohan ambao wanakabiliwa na kesi nne tofauti, walipandishwa katika kizimba hicho saa 8:20, wakikabiliwa na kesi za jinai.
Katika kesi ya kwanza ya jinai namba 1153, Mwanasheria wa Serikali Winfrida Koroso, alidai mbele ya Hakimu Neema Chusi kwamba mshitakiwa wa kwanza hadi tatu, wanakabiliwa na mashitaka matano ya wizi, kula njama na kughushi hati za makampuni, kujiingia ingizo la fedha kwenye akaunti kinyume cha sheria na kwamba Agosti 26 na Oktoba 27 mwaka 2005 katika jijini la Dar es Salaam, wote kwa pamoja walighushi hati za makampuni ya Navy Cut Tobacco (T) Ltd na Matsushita Electric Trading Company ya Japan kwamba zimewateua kukusanya madeni ya Kampuni ya Navy Cut Tobacco (T) Limited sh 3,323,974,942.30 na kufanikiwa kupata fedha hizo, mali ya Benki Kuu ya Tanzania.
Washitakiwa hao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea, Mpaya Kamala na Martin Matunda.
Upande wa mashitaka walidai kwamba hawana pingamizi na dhamana na hakimu Chusi aliamuru kila mshitakiwa kutoa nusu ya fedha taslimu wanazotuhumiwa kuiba na wadhamini wawili watakaotoa bondi ya sh bilioni moja na kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika.
Wakati wakihangaikia kupata dhamana, washitakiwa hao walipandishwa tena kizimbani kwa kesi ya pili.
Katika kesi ya pili ya jinai namba 1155 ya mwaka huu, mshitakiwa Devernra Patel, Jakayantkumar Patel, Amit Nandy ambao wanakabiliwa na makosa matano yanafanana na ya kesi ya kwanza.
Mwanasheria wa serikali, Fredrick Manyanda, alidai kuwa katika tarehe tofauti Desemba 2005 jijini Dar es Salaam, walijipatia sh 4,924,494,477.03 kutoka BoT ambapo walighushi na kujifanya wamiliki wa kampuni hewa ya Maltan Mining Ltd na kwamba wameteuliwa kukusanya madeni ya Kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan.
Hata hivyo kwenye kesi hii ya pili, hakimu alisema hawezi kutoa uamuzi wa dhamana kwa sababu ya muda wa kazi, na badala yake, uamuzi huo utatolewa leo.
Aidha, katika kesi ya tatu ya jinai namba 1154 ya mwaka huu inayomkabili Jeetu Patel Devendra Patel na Amit Nandy ambapo wanakabiliwa na mashitaka manane yakiwemo ya kughushi nyaraka, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Ilidaiwa kuwa katika tarehe tofauti, Septemba 2005, washitakiwa walijipatia sh 2,599,944,456.12 na sh 7,962,978,372.48 toka BoT kwa kisingizio kwamba wameteuliwa na kumpuni zaidi ya tatu hewa, kudai madeni ya kampuni ya Marubeni Corporation.
Katika kesi ya nne ya jinai namba 1157 ya mwaka huu, washtakiwa wote wanakabiliwa na makosa matano ya aina hiyo na walighushi hati za makampuni hewa ya C. ITOH & Company Ltd ya Japan na Bina Resorts Ltd yaliyokuwa yanaonyesha Bina Resort Ltd imewapatia jukumu la kukusanya deni sh bilioni 3,924,992,009,25 la C. ITOH Company Ltd, katika Benki Kuu ya Tanzania. Walikana shitaka hilo.
Wakati huo huo, watu watano akiwemo mume na mke walipandisha mahakamani hapo kwa kesi ya jinai ambapo wanakabiliwa na mashitaka 14, likiwemo la kughushi nyaraka mbalimbali ambazo zinaonyesha wao ni watumishi wa kampuni hewa ya Changanyikeni na kufanikiwa kuchukua fedha BoT.
Washtakiwa hao ni Bahati Mahenge, Manase Makale, Davis Kamungu, Godfrey Mosha na mwanamke mmoja Eda Makale ambaye ni mke wa mshitakiwa wa pili, wote wanadaiwa kuiba sh 2,887,267,249.65 ndani ya BoT.
Hata hivyo upande wa serikali upelelezi umekamilika na kwamba dhamana ipo wazi kwa maelezo kwamba kila mmoja wao anapaswa kulipa nusu ya kiasi fedha taslimu ambazo zikijumlisha kwa pamoja zitafikia kiwango hicho cha fedha wanazotuhumiwa kuiba na kuahirisha kesi hiyo hadi kesho kutwa.
Washitakiwa walishindwa masharti ya dhamana, hivyo ilipofika saa 12:13 jioni walipakizwa kwenye magari mawili aina ya Defender, yenye namba za usajili T220 AMV na T 210 AMV na kupelekwa gereza la Segerea.
Msafara wa watuhumiwa hao, ulikuwa chini ya ulinzi mkali na ukiongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Mkumbo.
Leo Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Eliezer Feleshi, anatarajia kuwasilisha mashitaka ya watuhumiwa wengine wa wizi wa fedha za EPA.
Ijuma iliyopita Rais Jakaya Kikwete alimuagiza DPP, Feleshi kuanda mashtaka dhidi ya watuhumiwa ambao wamekaidi agizo lake alilolitoa bungeni Agosti 31 mwaka huu, kwamba ifikapo Oktoba 31 mwaka huu, wawe wamerejesha fedha walizoiba.