Mh Rais wetu Mstaafu Jakaya Kikwete. Uongozi wa kweli haujengwi juu ya ndoto za kifamilia, bali juu ya msingi wa haki, utu na ujasiri wa kusema ukweli hata pale ambapo ukimya ni salama zaidi. Leo hii Tanzania inalia. Tundu Lissu, aliyenusurika kuuawa kwa risasi akiwa mpinzani mkuu wa serikali, sasa amefungwa kwa tuhuma za kisiasa.
Vyama vya upinzani vinazuiwa, chaguzi zinaibwa mchana kweupe, na watu wanaishi kwa hofu ya kutekwa au kufungwa kwa kusema tu kile wanachoamini. Na wewe Mheshimiwa, unanyamaza. Unanyamaza kana kwamba haya hayakuhusu.
Kama kwamba haki ni jambo la watu wengine si la wale waliowahi kuongoza. Tunajua kuwa huna tena mamlaka ya kisiasa, lakini bado una mamlaka ya kimaadili. Sauti yako inaweza kuamsha dhamira zilizolala. Lakini unapokaa kimya, unaacha hisia kuwa pengine uko tayari kuona taifa likiteketea mradi familia yako ibaki salama pengine na ndoto zako binafsi kama mzazi zisivurugwe.
Hii si hekima. Hii si busara. Hii ni hofu inayojificha ndani ya tabasamu la kisiasa. Na hofu ya mtu mkubwa huzaa mateso kwa watu wadogo.Historia itamkumbuka kila aliyesema hata kama sauti yake itanyamazishwa. Lakini itamhukumu kila aliyenyamaza hasa kama alikuwa na nafasi ya kusema.
Rizwan anaweza kuwa na ndoto ya kuwa Waziri Mkuu. Lakini ni bora awe Waziri Mkuu wa taifa la haki, si la watu walioumizwa kwa ukimya wa baba yake. Uongozi hauwezi kurithiwa kama mali, bali huhesabiwa kwa misingi ya utu na historia ya ujasiri wa familia.
Mh Rais Mstaafu , bado una nafasi ya kuchagua upande wa historia utakaoandika jina lako. Sema. Kemea. Simama upande wa haki. Si kwa ajili ya siasa, bali kwa ajili ya nafsi yako na heshima ya watoto wako mbele ya taifa linaloteseka.Kwa sababu ukimya mwingine ni kosa la maadili ambalo halionekani mara moja lakini halisahauliki.
View attachment 3413045