Wanabodi,
Hatimaye Tanzania sasa tunaanza kufaidi rasilimali zetu za madini, ambapo leo, donge nono la dola za Marekani milioni 100, zimelipwa kwenye kile kibubu chetu pale kwenye ule mfuko Mkuu wa hazina ya serikali kama advance payment ya kile kishika Uchumba cha dola milioni 300, ambacho baadae tulikigeuza kuwa ndio mahari kamili ya yule binti yetu makinikia.
Kiasi kilichobaki cha dola milioni 200, kitalipwa kwa mikupuo mitano ya dola milioni 40 kila mkupuo ambacho kitalipwa ndani ya miaka 5, kwa kila mkupuo kulipwa ndani ya mwaka mmoja mmoja.
Habari njema hii ni kwa mujibu wa Barrick,
Karibu ujisomee
Barrick Partnership with Tanzanian Government Delivers First Major Outcomes
Japo deni letu la makinikia ya Barrick lilikuwa Dola bilioni 190 ambazo zingetosha kumnunulia Noah kila Mtanzania, tukaahidiwa kishika Uchumba cha dola milioni 300!, lakini kufuatia majadiliano marefu, tulisamehe deni lote, na kile kishika Uchumba cha dola milioni 300, tulikikubali kuwa sasa ndio mahari kamili, hivyo hili donge nono la dola milioni 100, ndio mwanzo wa utekelezaji wa makubaliano na Barrick.
Donge nono hili la dola milioni 100 ni nje ya gawio la hisa asilimia 16% za bure bure, ambayo Tanzania tumepewa kwenye kampuni mpya ya ubia wa Tanzania na Barrick, kampuni ya Twiga, na manufaa makubwa kabisa, manene na manono kabisa yanayosubiriwa kwa hamu, ni mgawo wa 50/50, yaani pasu kwa pasu ya manufaa ya Kiuchumi ya kila kinachopatikana kwenye madini yetu.
Huu ni ukombozi mkubwa sana kwa taifa letu. Hongera sana JPM.
Mungu Ibariki Tanzania
Paskali