HERVÉ FALCIANI: MTU ALIYEVUNJA UKIMYA NA KUVUJISHA KWA DUNIA MAJINA YA MAFISADI WANAOFICHA PESA ZAO BENKI YA USWISI

HERVÉ FALCIANI: MTU ALIYEVUNJA UKIMYA NA KUVUJISHA KWA DUNIA MAJINA YA MAFISADI WANAOFICHA PESA ZAO BENKI YA USWISI

Zack Abdul

JF-Expert Member
Joined
Mar 9, 2026
Posts
1,194
Reaction score
911
Usiku wa Desemba 22, 2008, Geneva ilikuwa katika hali yake ya kawaida ya majira ya baridi.

Baridi ilikuwa imetanda. Krismasi ilikuwa karibu. Mji ulikuwa ukijiandaa kwa sikukuu, huku katika majengo ya kifahari ya benki za Uswisi, fedha za matajiri wa dunia zikiwa salama nyuma ya milango iliyofungwa kwa usiri mkubwa.

Lakini ndani ya HSBC Private Bank kulikuwa na jambo ambalo tayari lilikuwa limeanza kuuvuruga utulivu huo.

Jina lake lilikuwa Hervé Falciani.

Alikuwa mtaalamu wa mifumo ya kompyuta aliyefanya kazi katika bank ya HSBC Geneva kuanzia mwaka 2001. Alikuwa mtu wa ndani yani mtu aliyefahamu mifumo, miundombinu ya taarifa na namna data za wateja zilivyohifadhiwa.

Na sasa alikuwa ameshikilia kitu ambacho kingeweza kuvunja moja ya ngome maarufu zaidi za usiri wa kifedha duniani: taarifa za wateja wa benki.

Kwa muda, Falciani alikuwa amekusanya taarifa kutoka kwenye mifumo ya HSBC. Baadaye angeeleza kwamba aliamini alikuwa amegundua mfumo uliokuwa ukirahisisha utoroshaji wa kodi na kwamba alijaribu kuufikisha ujumbe huo kwa mamlaka.

Lakini upande wa pili ulikuwa na simulizi tofauti.

HSBC na mamlaka za Uswisi walimtazama si kama shujaa, bali kama mtu aliyekuwa ameiba siri za benki.

Hapo ndipo hadithi ilipoanza kuwa ya hatari.

Desemba 22, 2008. Geneva, Uswisi.

Polisi walimkamata Hervé Falciani, mfanyakazi wa bank ya HSBC, wakimtuhumu kuchukua taarifa za siri za wateja wa benki hiyo.

Baada ya kuhojiwa, jambo la kushangaza ambalo wengi wangeamini ndio ulikuwa mwisho wa Falcian aliachiliwa na mamlaka kwa muda na alipaswa kuripoti tena kesho yake, lakini badala ya kubaki Uswisi, Falciani alitoroka nchini humo pamoja na familia yake, akavuka mpaka hadi nchini Ufaransa.

Kile alichokuwa amebeba hakikuwa mzigo wa kawaida. Alikuwa na data za siri za wateja wa HSBC, taarifa ambazo baadaye zingetikisa moja ya mifumo mikubwa zaidi ya usiri wa kifedha duniani.

Mwaka 2009, mamlaka za Ufaransa zilianza kuchunguza data hizo. Ndani yake kulikuwa na majina, akaunti na taarifa za kifedha za wateja kutoka nchi mbalimbali.

Miaka kadhaa baadaye, wanahabari wa kimataifa walizifanyia uchunguzi na mwaka 2015 dunia ikaanza kuzifahamu kupitia kashfa iliyokuja kujulikana kama Swiss Leaks.

Taarifa hizo zilihusisha makumi ya maelfu ya wateja wa HSBC Switzerland na zilionyesha jinsi baadhi ya watu matajiri walivyokuwa wakitumia mfumo wa benki za Uswisi na miundo ya offshore kuhifadhi utajiri wao. Baadhi yao walihusishwa na tuhuma za ukwepaji kodi, ingawa kuwa na jina kwenye mafaili hayo hakukumaanisha moja kwa moja kwamba mtu alikuwa amefanya uhalifu.

Kwa mamlaka za Uswisi, Falcian alikuwa mtu aliyeiba siri za benki. Kwa wachunguzi na baadhi ya wanahabari, alikuwa shujaa aliyefichua taarifa ambazo zingesaidia serikali mbalimbali kufuatilia fedha zilizofichwa.

Na hapo ndipo hadithi yake ikawa kubwa kuliko yeye mwenyewe.

MWISHO WA SAFARI

Hervé Falciani hakuwahi kurudishwa Uswisi. Mwaka 2015 alihukumiwa akiwa hayupo kifungo cha miaka mitano, lakini aliendelea kuwa nje ya Uswisi. Alikamatwa tena Hispania mwaka 2018, lakini hakurejeshwa Uswisi.

Leo, Falciani anaishi Ufaransa, akiwa bado huru licha ya hukumu hiyo ya Uswisi.

Kwa Uswisi, alikuwa mwizi wa siri za benki; kwa wengine, alikuwa whistleblower aliyefichua mfumo wa fedha uliofichika nyuma ya usiri wa benki.

Lakini mwisho wa yote, jambo moja lilibaki: Falciani aliondoka Geneva akiwa na siri, na siri hizo zikaja kuutikisa mfumo wa benki duniani.

- MWISHO

✍ Dr. ZACK
HR6jmi7aMAA3pr6.jpg
 
Back
Top Bottom