Hii nchi haina usawa. Hii nchi haijapata kiongozi wa kuleta usawa ingalau kwa nusu tu miongoni mwa wananchi.
Tumesikia wimbo huu wa kinafiki kuwa, Rais John Pombe Magufuli ni Rais na kiongozi wa wanyonge, wananchi wa hali ya chini.
Si kweli, no uongo na ni propaganda za kisiasa tu kwa ajili ya wapambe na wanafiki wachache wanaomzunguka huku uhalisia wa mambo ukiwa tofauti.
Mfano wa kuthibitisha hili ni huu;
Bunge limevunjwa juzi tarehe 16/6/2020. Hawa wabunge lililovunjwa juzi wameingia kazini mwaka 2015. Wamefanya kazi yao miaka mitano (5) tu toka mwaka 2015 hadi mwaka huu 2020.
Inasemekana mafao ya kiinua mgongo kwa miaka mitano tu kila mmoja ni zaidi ya Tshs. 250,000,000.
Na inasemekana wakati Rais Magufuli (eti Rais wa wanyonge) anahutubia ndani hiyo juzi kulivunja bunge hilo, tayari mzigo wa fedha wa kila mbunge ulishaingia kwenye Bank Account yake.
Hebu tazama upande wa pili wa wanyonge halisi kinachotokea.
Huko Sengerema (na naamini kwingine kote Tanzania nzima), yupo mwalimu aliyefanya kazi miaka 32 (1988 - 2020) kwa taabu na shida nyingi. Amestaafu tangu mwezi Januari, 2020. Baada ya kukokotolewa kwa mafao yake ya mkupuo atapata kama Tshs. 75,000,0000 hivi.
Kinacholeta shida ni kuwa, tangu huyu mwalimu masikini astaafu kwa mujibu wa sheria mwezi january hadi Juni hii mwaka huu, 2020 (miezi 6 sasa) bado anasotea mafao yake haya kidogo, hajalipwa.
Sasa swali la kujiuliza ni hili;
Kati ya wabunge hawa ambao bunge linavunjwa leo huku mafao yao yakiwa yaneshalipwa jana na huyu mwalimu ambaye kastaafu miezi sita (6) iliyopita na bado hajalipwa vijisenti vyake vya mafao, ni nani hasa mnyonge?
Na huu usawa katika nchi hii uko wapi? Iweje mbunge aliyefanya kazi miaka mitano tu alipwe mafao ya kiinua mgongo kikubwa hivyo kwa takribani mara tano ya mwalimu ama nesi ama daktari aliyefanya kazi kwa miaka 35?
Huyu mtetezi wa wanyonge (Bwana Magufuli) anatetea wanyonge na unyonge upi hasa?
Mimi nasema Tanzania haina kiongozi Rais mtetezi wa wanyonge. Haijapata na hakuna kizuri wala kiongozi mzuri atakayetokana na CCM ili kubadilisha hali hii na kuleta tofauti na usawa.