JPM alikuwa ni kiongozi mwenye kufanana sana na mahitaji ya nchi yetu. Uonevu ulikuwa umezidi na watu wakijiona ni miungu watu.
Kulikuwa na umafia wa hali ya juu, mitandao ya unyanganyi wa mali za watu ukiongozwa na wafanyakazi wa serikali, hatukuogopana kiasi cha kuoneana huku tukijua yule anayeonewa hana uwezo wa kumfanya chochote muoneaji.
Reli mara ya mwisho kufika Moshi ilikuwa 1995 JPM mwaka jana kaifufua hiyo safari Wachagga wameenda krismasi wakitandika pombe kwenye mabehewa. Hivi sasa kuna wataalam wa masuala ya masuala ya reli 120 wamesomeshwa pale NIT ili wakati SGR ikianza kazi tuwe tayari na wataalam wazalendo.
Ndege hizi kama sio uwezo wa kufuatilia aliokuwa nao RIP zisingenunuliwa. Twiga asingeonekana angani, Mama Samia asingesafiri kwenda Kenya na Uganda akijinafasi.
Hayati alikuwa na udhaifu wake wa hasira na maamuzi yenye kuumiza wengi. Ukitaka tajiri aishi kama shetani maana yake unamuua na njaa mfanyakazi wake. Manji alienda zake Canada, Mo Dewji anaweza kwenda zake South Africa, Bakhresa anaweza kuishi Dubai au New York, tatizo ni yule dereva wake, tatizo ni yule mfanyakazi wa kampuni yake anayesomesha na kulea familia.
Hayati alikuwa na matatizo ya kiafya ambayo ni makubwa, ilikuwa ni vigumu kwake kuwa na amani ya kiakili ikiwa ndani ya moyo kumewekwa kitu cha kumsaidia kupumua. Alikuwa ni mkiwa anayeishi miongoni mwa watu wengi kwa wakati mmoja.
Mungu natumaini amemsamehe madhambi yake kwa kuweza kupata sakramenti ya mwisho siku aliyoaga dunia