Tatizo la nchi yetu ni kwamba watu wengi wanadhani kuwa chaguzi zikiwa mbovu, barabara zikiwa duni, au huduma za afya zikiwa hafifu, basi hayo ni matatizo ya Chadema pekee—kana kwamba ni Chadema peke yao wanaoteseka. Ukweli ni kwamba, mfumo mbovu wa taratibu, ikiwemo haki za msingi, unawaathiri Watanzania wengi bila kujali itikadi zao za kisiasa.
Kwa mfano, kuchaguliwa katika uchaguzi ni haki ya kila Mtanzania alimradi anatimiza vigezo vya kisheria. Hata hivyo, wakati huu ambapo Tundu Lissu kupitia Chadema anajaribu kueleza na kupambana na changamoto za sheria na taratibu za uchaguzi, wengi wanadhani ni ajenda ya Chadema pekee. Lakini ukweli ni kwamba, iwapo maboresho yatafanyika, Watanzania wengi watanufaika, hata kama wao wenyewe hawajaingia mstari wa mbele kudai haki hizo.
Ikiwa chaguzi zitakuwa huru, haki, na zenye misingi imara, hata mgombea binafsi asiye na chama atakuwa na nafasi ya kushinda. Lakini kwa hali na sheria zilizopo sasa, mgombea binafsi kushinda jimbo au nafasi yoyote ni sawa na ngamia kupenya kwenye tundu la sindano—yaani, haiwezekani. Lakini je, kuna Watanzania wangapi hawana vyama na wangependa kugombea na kushinda ila wanakwamishwa na mfumo wa sasa wa siasa za vyama? Ni wengi. Hata hivyo, wengi wao hawawezi kutoka hadharani kudai haki zao na pengine wanaamini kuwa hizi reform ni kwa ajili ya Chadema tu.
Nikitafakari, mara nyingine naona kama mfumo wa vyama vingi haujawanufaisha Watanzania ipasavyo. Sheria na miongozo iliyopo ina changamoto zake, lakini hata hizo chache zilizopo hazifuatwi kwa usahihi. Pengine, badala ya mfumo wa vyama vingi au hata wa chama kimoja, tunapaswa kuwa na mfumo wa kati—"hybrid mode"—ambao utazingatia mazingira ya Tanzania na mahitaji halisi ya wananchi. Kwa sababu Watanzania wengi, kama mimi, tunachotaka ni maendeleo na usawa wa kugawana rasilimali za taifa, bila kujali ni mtu gani au chama gani kiko madarakani.
Kwa hivyo, tunahitaji mjadala wa kitaifa unaohusisha makundi yote, si Chadema pekee. Tunapaswa kukaa chini kama taifa na kuangalia katiba yetu, miongozo yetu, sheria zetu, na vyama vyetu, ili tupate suluhisho la matatizo yanayomkabili Mtanzania wa kawaida. Haijachelewa—bado tunaweza kufanya mabadiliko yanayowanufaisha wote.