Kipekee sana nimekuwa na heshma kubwa na ukatoliki. Kama ilivyo kwa wakristo wengi, wengi wetu, kwa kiasi kikubwa malezi ya utotoni tumeyapatia katika kanisa katoliki, baadaye baadhi yetu kwasababu mbalimbali tumejikuta ni wakristo wa madhehebu mengine.
Mbali na malezi ya kiroho kwa wakristo walio wengi; ukiacha serikali, kanisa katoliki ndiyo taasisi yenye shule nyingi za msingi, sekondari, vyuo na vyuo vikuu ambayo vimelea na kuzalisha nguvu kazi kubwa kwa Taifa letu.
Nimeanza na hayo ili kujenga msingi wa ukubwa wa ushawishi wa kanisa katoliki katika jumuiya ya wakristo, wasomi wa nchi yetu na wananchi kwa ujumla.
Kwa muktadha huo na kwakuzingatia mwenendo wa matamko ya Baba yetu Padre Kitima, nimejikuta nawaza kwa sauti; Je, ni kweli kuwa serikali yetu haishauriki kwa kiasi hiki, au na yeye anafanya siasa?
Katika maisha yetu ya kawaida, tunajua ushauri kupokelewa au kutokupokelewa haitegemei tu kuwa ushauri huo ni mzuri kiasi gani bali pia njia zilizotumika kuutoa ushauri wenyewe. Ushauri mzuri ukitolewa katika njia inayowatweza viongozi ni wazi kuwa watauona kama shambulio la kisiasa. Hali kama hii inaleta hisia za kujihami na kujilinda ambazo kwakweli zinachochea mpasuko na uhasama.
Najaribu kufikiri tofauti, vipi kama Baba yetu Padre Kitima, kwa nafasi yake kama katibu wa Balaza la Maaskofu angeomba kumuona Rais wetu ili kumshauri mambo yote anayodhani kuwa hayopo sawa, katika mazingira yasiyoutweza utu wa Rais wetu, Je, asingepewa nafasi hiyo?
Wasiwasi wangu ni kuwa kama ushauri mzuri unaotolewa na walezi na wazazi wetu wa kiroho hautatolewa katika mazingira yanayoepusha hisia za ubaguzi na kutwezwa kwa viongozi, jamii nzima ya watanzania itayakosa matunda mazuri ya ushauri huo.
Mwisho ningependa kutoa tahadhari, Rais wetu ni mzanzibari, na ni Muislam! Tusipokuwa waangalifu, ni rahisi sana harakati za kanisa kudhaniwa kuwa zinafanyika kwa misingi ya chuki na ubaguzi. Kama tukifika hapo, jitihada hizi nzuri zitakuwa sio baraka tena bali balaa.