Nilitegemea wataalam wetu wa afya pamoja na washauri wa Rais waliomshauri kuagiza chanjo ya corona watakuwa mstari wa mbele kujibu hoja za askofu badala yake wamekuwa watu wa kumshambulia yeye binafsi na kumpa vitisho badala ya kujibu hoza zake kitaalam.
Katika hoja ya kwanza, Askofu gwajima ana hoji: Endapo mtu akichanjwa bado ataendelea kuambukiza na kuambukizwa virusi vya corona na kama ndivyo, kuna maana gani ya kuchanja?
Hoja ya pili Askofu anahoji endapo mtu amechanjwa bado atatakiwa kuchukua tahadhari zote ikiwemo kuvaa barakoa ili kujikinga na maambukizi. Askofu anataka kujua, kama kweli chanjo ya corona ni kinga kwanini mtu aliyechanjwa anatakiwa tena kuvaa barakoa?
Askofu anaendelea kuhoji, mataifa makubwa kama vile marekani yote yana chanjo zao. Kwa mfano, marekani wana chanjo ya jonhson&jonhson na moderna, china wana sinovac, uiongereza wana Astrazeneca, germany wana Pfizer, urusi wana ya kwao, Cuba pia wana ya kwao na mataifa mengine yana chanjo zao. Je ni kwanini haya mataifa yenyewe kwa yenyewe yanaogopana kutumia chanjo ya mwingine?
Gwajima ana hoji kwamba katika kipindi cha zaidi ya miezi sita iliyopita wataalam wetu wanaotaka tupambane na corona kwa njia ya chanjo ndio hawa hawa walisema tusiziamini chanjo kwamba zinaweza kuwa na madhara na kwamba tutumie njia za asili ikiwemo kujifukiza wakajenga hadi banda la kujifukizia pale muhimbili wengine wakafanya mahojiano TBC kuonyesha wasi wasi wao juu ya chanjo ya corona, kwanini leo wamebadilika?
Swali la nyongeza: kwenye fomu ya chanjo ya corona kuna kipengele kinasema serikali haitahusika kwa namna yoyote ile endapo mtu aliyechanjwa atapata maudhi ambayo kwa sasa hayafahamiki. Tunataka wataalam wetu watwambie kama hii chanjo wameifanyia utafiti wa kutosha kwanini wanasema tena kwamba mtu aliyechanjwa anaweza kupata maudhi ambayo hayafahamiki?
Napenda sana wataalam wajibu hoja za gwajima kwa sababu vile wanavyomshambulia badala ya kujibu hoja zake ni kudhihirisha kwamba hawana utaalam wa walichosomea kitu ambacho ni hatari kwa uhai na afya za watanzania.
Hoja ya kwanza:
Mtu akipata chanjo anaweza kuambukizwa kwa sababu zifuatazo:
a. Chanjo inachukua muda kuanza kukukinga kwa kikamilifu. Nyingi ni kati ya wiki mbili au tatu. Katika dirisha hili unaweza kuambukizwa.
b. Chanjo sio 100 % katika kuzuia maambukizi. Johnson and Johnson ni kama 80% na Pfizer 90% na Moderna 90%. Ila chanjo zote zinakaribia ubora wa 100% katika kukulinda usiathirike sana. Ndio maana sasa hivi Marekani 95% ya wanaopoteza maisha yao baada ya kuambukizwa ni wale ambao hawajachanjwa.
Hoja ya pili:
Barakoa zinasaidia zaidi kukuzuia kuambukiza kuliko kuambukiza. Ndio maana kama wote mkivaa maambukizi yanapungua sana. Lakini wakiwepo wabishi basi hao wanaweza kuwaambukiza hata waliovaa barakoa. Kwa vile aliyechanjwa anaweza kuambukizwa barakoa inasaidia kumzuia kuambukiza wale ambao hawajachanjwa na kuwaletea matatizo makubwa. Mkichanjwa wengi basi uwezekano wa kuambukizana unapungua sana na hivyo kufanya barakoa kutokua na umuhimu sana. Ila kama wengi hawajachanja basi barakoa ni muhimu hata kwa waliochanja. Mfano ni ingawa tunaoga ili tuwe wasafi lakini haimaanishi kuwa
hamna haja ya kufua taulo ambalo tunatumia kujikausha baada ya kuoga. Hii ni kwa sababu hata uoge vipi kuna uchafu unabaki, kuoga hakukuhakikishii kuwa wewe ni msafi 100 %. Hivyo hivyo kwa kinga.
Hoja ya tatu.
Katika nchi za magharibi chanjo hazitengenezwi na mataifa bali makampuni binafsi yaliyokuwa na uwezo wa kutengeneza. Serikali na watu binafsi wali invest katika haya makampuni ili kuyaongezea uwezo wao. Kwa vile hamna mtu alijua kampuni ipi itafanikiwa kwanza serikali ziliweka oda katika karibu makampuni yote. Umoja wa Ulaya walikubaliana kununua kwa pamoja. Kampuni hizi zilipofanikiwa zilitangulia kuwapa wale walioweka oda zao mapema. Ndio maana Marekani amejikuta ana chanjo nyingi kuliko anazohitaji na ugomvi ulilipuka kati ya EU na Uingereza baada ya Astrazeneca kusema atatimiza kwanza oda ya Uingereza kabla ya EU. Aidha, hizi nchi zote zina taasisi zao za kutoa kibali cha chanjo kutumika. Kibali hiki kinatolewa baada ya mtengenezaji kuomba. Kwa mfano, Astrazeneca haijaomba kibali Marekani kwa hiyo haitumiki Marekani bali inatumika Uingereza na EU ambako waliomba na kupata vibali (EU na Uingereza wanatumia pia za Pfizer na Moderna). Hivyo hivyo kwa chanjo za kichina, kirusi, Cuba n.k. Haziwezi kutumika nchi za magharibi kwa sababu hawawezi kuwaomba kibali adui zao maana wanaweza kuwakatalia ili kuwapakazia tu.
Hoja ya nne.
Hii siwezi kuijibu maana sikuhusika na uamuzi wa awali wa kupinga chanjo.
Hoja ya tano.
Kwa wenzetu fomu ya kibali cha kufanyiwa tiba ni kitu cha kawaida ( hasa Marekani) kwa sababu wenzetu wanatumia vizuri haki yao ya kumshitaki yeyote ambae amemkwaza kwa namna yeyote. Gharama za kutoa huduma yeyote kwa wenzetu zinakuwa juu kwa sababu wataalam wote inabidi wakate bima ( professional indemnity insurance) ambayo itawasaidia kama tatizo lolote litatokea kutokana na kazi walizofanya. Kwa wenzetu ukijikwaa na kuanguka mbele ya duka unaweza kumpeleka mahakamani mwenye duka kuwa hakukausha maji ya mvua mbele ya duka lake na hivyo kukusababishia maumivu makubwa ya kimwili na kisaikolojia kutokana na watu kukucheka ulipoanguka. Tabia hiyo hapa kwetu haipo. Lakini haimzuii mjanja mmoja ambae akijikuta anaharisha baada ya chanjo kumshitaki mtengenezaji katika mahakama za marekani kama pasingekuwa na clause hiyo.
Haya majibu yametolewa sana maana si Gwajima peke yake aliyekuwa na wasiwasi na hizi chanjo. Tofauti yetu ni kuwa hata baada ya kupewa majibu hatutayakubali kwa sababu imani yetu ya asili ( natural instinct) ni kuwaamini waganga na matapeli wanaojifanya ni watu wa Mungu.
Wenzetu wanaendelea kuchanja na kuna uwezekano kuwa hata zile tulizokuwa tunategemea tutapata zikachelewa kwa sababu sasa hivi wanazungumzia chanjo za ku boost hizi za mwanzo.
Mwisho wa siku ni uamuzi wako, hasa kama haujauguliwa au kufiwa na mtu kutokana na janga hili.
Amandla...