Ikiwa imebaki miezi michache kufikia mwezi Oktoba, mwezi ambao uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 utafanyika nchini, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, Inspekta Jenerali, Simon Sirro, leo Agosti 19, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya siasa, pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
-----
INSPEKTA JENERALI WA POLISI AWASILISHA MADA KATIKA MKUTANO WA TUME YA UCHAGUZI, VYAMA VYA SIASA NA WADAU WA UCHAGUZI NCHINI.
Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Nyakoro Sirro ametoa mada leo tarehe 19.08.2020 kuhusu ulinzi na usalama katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Julius Nyerere Convention Centre (JNICC) jijini Dar es Salaam ikiwa ni mikakati ya kuhakikisha amani na usalama vinatawala wakati wote wa kuchukua fomu kwa Wagombea, urejeshaji wa fomu, kampeni, upigaji kura, kuhesabu kura, kutangaza matokeo na kusherehekea ushindi.
Pia alizungumzia kuhusu hali ya uhalifu nchini, amesema hali ya uhalifu nchini imepungua kwa kiasi kikubwa sana na askari wamejiandaa vizuri sana kusimamia uchaguzi uliopo mbele yetu kwa kubaini makosa hata kabla hayajatokea na kumchukua hatua ikiwa pamoja na kuandaa mashtaka na kuwapeleka watuhumiwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.
Makosa hayo ambayo yamekuwa yanajitokeza ni makosa ya mitandao ya kijamii kama Jamii Forum, Facebook, Instagram, twitter, Blogs na Whatsapp.
Aidha Katika mada hiyo Inspekta Jenerali wa Polisi alihitimisha kwa kusema amani ni muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu hivyo viongozi wa vyama vya siasa kufuata sheria za uchaguzi na tume ya uchaguzi kuweka taratibu zote za uchaguzi mapema ili kuondoa mapungufu yanayoweza kuleta taharuki.
Alisema viongozi wa siasa watapita lakini nchi itabaki kama nchi, pia Hasira huondoa busara na ukitaka kufa tafuta njia nyingine ya kufa na si kutumia siasa.
Mwisho tumejipanga vizuri kutoa ulinzi kwa wahombea na wagombea wenza kwa wagombea wote watakaopitishwa na Tume ya Uchaguzi.