DODOMA — Serikali ya Uganda imezindua rasmi ujenzi wa Ofisi ya Ubalozi wake katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, ikiwa nchi ya kwanza kuanza ujenzi wa ubalozi wake katika mji huo mkuu wa Tanzania.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali Fred Mwesigye, amesema hatua hiyo ni zaidi ya uwekezaji wa miundombinu, bali ni ishara ya uhusiano wa karibu na wa kihistoria baina ya Uganda na Tanzania. "Hatua hii ni heshima kwa mchango mkubwa wa Tanzania katika historia ya Uganda. Tunafurahi kuwa wa kwanza kuunga mkono uamuzi wa Serikali ya Tanzania kuhamia Dodoma," alisema Mwesigye.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Dennis Londo, aliipongeza Uganda kwa kuweka historia hiyo. "Ni kielelezo cha undugu, ujirani mwema na mshikamano wa dhati baina ya mataifa yetu mawili," alisema.
Londo aliwahimiza mabalozi wengine kufuata mfano huo, akisisitiza kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi jijini Dodoma. Alitaja miundombinu ya huduma bora kama afya, elimu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato kama sehemu ya maandalizi ya kuwakaribisha wanadiplomasia.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, aliahidi kuwa mkoa huo uko tayari kuwahudumia mabalozi wote. "Tunaendelea kuboresha miundombinu yote muhimu kuhakikisha jumuiya ya wanadiplomasia inapata huduma bora na salama," alisema.
Imeandaliwa na Mwandishi Wetu
Zaidi tembelea //www.habarileo.co.tz
#HabariLEOUPDATES