Ndugu zangu, nafsi yangu imenisukuma kuandika jambo wakati huu tunapoomboleza msiba wa rais wetu mstaafu "Mzee Ruksa" kama ifuatavyo;-
Aliuza Loliondo kwa waarabu pamoja na kelele nyingi zilizopigwa.
Alileta ada kwa vyuo vyote vya serikali IFM, Mzumbe, UDSM, n.k wakati wa Mwalimu vyuo vyote ilikuwa hulipi chochote ni sifa tu za kujiunga zinakupeleka.
Alianzisha utaratibu wa kulipia matibabu katika hospitali za serikali, kabla ya hapo matibabu yalikuwa bure hadi Muhimbili. Maana yake ni kwamba serikali iligharamia.
Alianzisha utaratibu wa kulipia ada katika shule za sekondari za serikali, kabla ya hapo ilikuwa bure kabisa.
Alivunja miiko ya viongozi. Sasa, viongozi wakawa hawana miiko tena, hapa ndipo ufisadi wa viongozi ulipoanzia.
Alianzisha upendeleo wa waziwazi kwa watu wake hata kama wamefanya makosa kiasi gani aliwakingia kifua na kuwasamehe...mfano Ruban Aziz aliyefungwa kwa kutorosha madini alimsamehe kwa madai "eti" mama Aziz alienda Ikulu kumlilia.
Yeye ndiye muasisi wa viongozi kuanza kujimilikisha mali za umma.
Yeye ndiye alianza kuuza viwanda vya umma kwa matajiri.
Yeye ndiye alisitisha ajira za moja kwa moja toka vyuoni, baada ya kukosa ubunifu wa kupanua wigo wa ajira kwa kuanza kuua viwanda, mashirika n.k vya umma.
Ndiye alianza kuogopa midahalo katika vyuo vikuu...alisisitiza vyuoni kumefuatwa vyeti tu siyo siasa. Hapo ndipo tatizo lilipoanzia anguko la wasomi wa nchi hii kuwa na vyeti vizuri lkn hawana "akili" kabisa.
Heshima ya taifa ilianza kushuka sana, majirani hata mataifa ya nje yaliyokuwa yanatuheshimu yalianza kutudharau kwakuwa kiongozi wetu hakuwa makini sana kwenye mambo ya msingi, mfano alitoa amri ikawa sheria sikukuu yoyote ikiangukia jumamosi au jumapili ilikuwa inalipiziwa kwa watu kupumzika siku za kazi juma linalofuata, ulikuwa ujinga fulani hivi na ulitushushia hadhi sana kama taifa kwa wenzetu.
Alianzisha utaratibu wa kusafiri na "kijiji" akienda nje ya nchi. Lengo lilikuwa kwenda kula maisha na marafiki zake. Safari ya mwisho ilikuwa ya Copenhagen...vyombo (hasa magazeti) yaliandika na kulalamika sana kuhusu hili.
Aliondoa udhibiti kisheria wa bei za bidhaa mbalimbali. Bidhaa zilikuwepo lkn mfumuko wa bei ukawa juu, wafanyabiashara wakaneemeka sana wananchi wa kawaida wakazidi kuwa masikini.
Aliongeza pengo kati ya tajiri na masikini, nchi ilianza kuwa ya matabaka ya matajiri na masikini wakati wake. Kabla yake ilikuwa kawaida mtoto wa mkulima wa jembe la mkono na mtoto wa rais, waziri n.k kusoma shule moja, lkn alipokuja "akawatenga" nchi hii sasa hawa watu wanakutana wakati wa uchaguzi tu hohehahe wanapo ombwa kura.
****
Ninapenda nimalizie hivi ndugu zangu.
Nimeamua nimkumbuke mzee wetu kwa baadhi ya mambo hayo ambayo naamini ni muhimu kizazi ambacho hakikuwepo wakati wa utawala wake kikayafahamu au hata waliokuwepo wanaweza kuwa wamesahau.
Lengo la hayo hapo juu siyo kubeza, kuchafua, ama nia yeyote mbaya, la si hivyo. Lengo ni kwetu tuliobaki, kila tutendalo kwa watu liwe jema ktk macho yao au baya litakumbukwa siku tutakapo "fumba macho".