Jeshi la Polisi nchini limesema limebaini kuwepo kwa mipango, matamko na uhamasishaji unaofanywa na baadhi ya viongozi wa dini, wanasiasa na wanaharakati kupitia vikao vya siri na mikutano ya wazi, kwa lengo la kuwashawishi watu kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Kwa mujibu wa Jeshi hilo, vitendo vinavyopangwa ni pamoja na kufanya vurugu, kuharibu miundombinu inayotumika kutoa huduma kwa umma pamoja na kuharibu mali za umma na binafsi.
"Jeshi la Polisi linawahakikishia kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na kwa kutumia taarifa linaloendelea kupokea, linafuatilia kwa karibu sana ikiwa ni pamoja na kuwakamata wahusika wa mipango hiyo kwa hatua zaidi za kisheria," limesema.
Aidha, Jeshi la Polisi limewaonya wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja, likisisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watakaobainika kuhusika na mipango ya kufanya fujo na kuharibu mali.