Mwaka 1982, Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) ilitekwa nyara. Katika Kijiji cha Itunge, kulikuwa na mtu mmoja tu ambaye kila mara alitegea sikio Radio yake aina ya Nation ili kusikia kama kuna taarifa mpya kuhusiana na tukio hilo. Mwanzoni, hakutaka kuieleza familia yake nini kilitokea lakini mtoto wake wa Darasa la Nne ambaye ni mimi alikuwa tayari amesikia katika taarifa ya habari ya Radio Tanzania kuwa Ndege ilikuwa imetekwa nyara.
Mzee alikuwa ametaarifiwa mtoto wake David Mwamakula ambaye alikuwa anafanya kazi na ATC alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa katika Ndege ile. David alikuwa amehitimu masomo yake nchini Zambia na yeye hakutaka kuendelea kuishi Zambia, bali aliamua kurudi ili aje afanye kazi katika nchi yake.
Mwaka 1979, baba alitoa ng'ombe katika zizi akiwemo dume aliyeitwa 'Mwenge' kupeleka kwa watu. Mwenge alikuwa ni kambaku hodari sana katika kulima. Nilipomuuliza baba kuwa ng'ombe wale walikuwa wanakwenda wapi, mama alinijibu kuwa kaka yako aliyekuwa kule 'Kambofi' (Zambia) amerudi na sasa anaoa. Na kwamba ilikuwa ni desturi kwa kuwa ni mke wa kwanza, lazima ng'ombe atoe baba!
Wiki kabla, David alikuwa amekuja akivalia tai huku akiwa mng'aavu na mtanashati. Sikujua kuwa tai iliashiria nini lakini itoshe kusema kaka yangu alikuwa amependeza kuzidi hata walimu wangu. Ndiyo, alikuwa mtanashati hata kumzidi Mwl. Absalomu Kanyama aliyekuwa ni mtanashati sana akitamba na 'raizoni' zake na 'pekosi' yake akiwapiku walimu wote wa Itunge. Jina lingine la 'pekosi' ilikuwa ni 'bugaluu' na jina lingine la 'raizoni' ilikuwa ni 'ngazi mbili' na baadaye zilipochuja, vijana wakaziita 'telemka tuzoze' au 'telemka tuonane'!
Ng'ombe waliswagwa hadi Kijiji cha Lukuyu na huko ndiko kaka alijipatia mke ambaye mimi namkumbuka kwa jina moja la kuzalia watoto la 'Ngolowa'! Sikumbuki majina yote kwa kuwa yeye alifariki muda mrefu lakini pia hata ndoa yake na kaka haikuwa na maisha marefu.
Ilikuwa saa mbili usiku ndipo baba akatueleza kuwa Ndege ya Tanzania imetekwa nyara na kuwa kaka yetu Daudi (David) alikuwemo katika Ndege ile. Ilikuwa ni hofu kubwa kwani wakati ule, Ndege ikitekwa, kilichofuata ni kulipuliwa!
Lakini miaka kwa hiyo.bado vita baridi kati ya Malawi na Tanzania ilikuwa imepamba moto. Rais Nyerere alikuwa amemtuma jirani yetu ili ajifanye 'analima matuta' kama kibarua kumbe lengo ilikuwa ni kukusanya taarifa za Malawi!
Kesho yake, Radio Tanzania ikatangaza kuwa Ndege imepelekwa Uingereza. Baadaye sana ndipo tukasikia kuwa abiria na wafanyakazi wa ATC waliruhusiwa kurejea nyumbani salama. Nilishuhudia mama akianika mpunga mwingi na kupeleka mashine ili kukoboa uuzwe, baba apate nauli ya kwenda Dar es Salaam kumuona mwanae! Lakini, baba tayari alishaondoka na huenda alikopa pesa mahali na hivyo pesa ile ya mpunga ingerudishwa kwa wenyewe.
Ilikuwa ni furaha iliyoje kuona kaka yetu Daudi (David) alikuwa salama. Mwaka huo huo, dada yangu naye (Lusia) aliaga kuwa anakwenda Dar kumsalimia kaka Daudi, ikawa 'katumu' - yeye hakurudi tena Itunge! Alilowea! Zamu yangu ya kuja Dar es Salaam ilikuwa Agosti 1985. Ajabu, nilikuja kuishi Kipawa, pembezoni na Uwanja wa Ndege. Nikakumbuka tukio la kutekwa kwa kaka yangu David.
Desemba 1988 nilihamia rasmi kwa kaka David eneo la Temeke Wailesi, na hapo ndipo nikawa na fursa ya kumuuliza juu ya tukio la utekaji. Lakini yeye hakuwa anapenda sana kusimulia habari ile zaidi ya kutaja watekaji kwa majina. Lakini alikuwa pia anapenda kuwataja rafiki zake ambao alikuwa nao ATC kama Captain Kasimbazi, Captain Mahimbo, na Etutu! Hao niliwafahamu hata kwa sura pia ingawa sijui kama na wao walikuwa ni miongoni mwa waliokuwa wametekwa nyara mwaka 1982.
Siku moja mwaka 1990, kaka David alinipatia maelekezo ya kipekee. Alinieleza nimfulie mapema nguo zake na nihakikishe nazipiga pasi vizuri sana kwani kesho yake anakwenda Ikulu! Alinieleza kuwa wameitwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kupewa nishani za ushujaa! Kwamba tukio la kutekwa nyara lilikumbukwa na Serikali na kuwa Rais atawavisha nishani. Nilitamani na mimi nijihudhurishe Ikulu, lakini, 'mawe'!
Aliporudi, nikajisemea moyoni kuwa kumbe na sisi kwenye familia na ukoo wetu tumetunikiwa nishani! Mwe! Lakini sikuona kama waliepwa pesa labda kama walipewa, kaka alichikichia na huenda haikua pesa nyingi. Tangu wakati ule ninawaza kuwa nishani za ushujaa ziwe na pesa 'mingi' isiwe sifa tu! Mwe!
Leo, nilipokuwa napekua kumbukumbu zangu nikakutana na picha ambayo Rais Ali Hassan Mwinyi alipiga pamoja na watunukiwa hao Ikulu mwaka 1990. Nikamuona kaka yangu David Mwamakula akiwa kushoto kabisa akiwa amevalia vyeo vya wana anga! Usiniulize kwa sasa kuwa yuko wapi! David Mwamakula au 'Kulaman' kama wenzake walivyozoea kumuita alifarakana na maisha haya mwaka 2002.
Sikuwepo wakati anarejea baada ya kutekwa nyara (nilikuwa kinda), sikuwepo Ikulu wakati anapewa nishani (nilikuwa napiga kitabu au nilikuwa 'nabundi' pale Azania) na sikuwepo wakati anafariki (nilikuwa masomoni nje). Yeye alizoea kuniita kama mama (RIP), baba (RIP) na dada Lusia walivyokuwa wananiita.
Simulizi binafsi ni mafiga muhimu sana katika maisha ya viongozi. Viongozi wengi wa Afrika hawataki mambo binafsi kuhusu maisha na pia mapito au makuzi yao yajulikane hadharani. Mimi najitahidi kuweka simulizi binafsi kuhusu maisha yangu.
Kama simulizi hii imekuboa, basi nenda katika ukurasa wa Yericko Nyerere kasome kuhusu tuzo yake, nenda ukurasa wa Ikulu Mawasiliano kasome juu ya uteuzi au nenda twita kasome ntiiti za Shangazi wale wawili. Vinginevyo, kula 'kobisi', 'kula yabisi', 'minya' au potezea kabisa jifanye hujaona!
Je, nini kimekushangaza? Je, nini maoni yako?
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula
Dar es Salaam, 11 Desemba 2023; 10:28 jioni
Sent using
Jamii Forums mobile app