Mabishano makali ya kisheria yameibuka baina ya mawakili wa serikali na upande wa utetezi katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole sabaya na wenzake wawili,baada ya upande wa jamhuri kuiomba mahakama kufanya marekebisho jina la mshtakiwa namba moja Lengai Ole Sabaya lililokuwa limeandikwa Lengai ole Sayaba .
Katika hati ya mashtaka aliyosomewa mshtakiwa sabaya na wenzake Julai 16 mwaka huu jina la Lengai ole Sabaya liliandikwa Lengai ole Sayaba na hivyo wakili mwandamizi wa serikali Abdalah Chavula aliiomba mahakama kufanya marekebisho kwenye hati ya mashtaka.
Wakili wa serikali Abdallah Chavula alieleza kuwa kilichotokea ni makosa ya kiuandishi Lakini mshtakiwa ni Lengai Ole Sabaya na si Lengai ola Sayaba kama hati inavyoonesha
Wakili Chavula aliiomba mahakama kupitia kifungu cha sheria namba 234 Kifungu kidogo cha kwanza cha makosa ya jinai ya mwaka 2019 Sura ya 20 .
Naye wakili mkuu wa serikali Tumaini Kweka aliieleza mahakama kuwa maombi yao yana mashiko na kwa sababu suala hilo liko ndani ya mamlaka ya mahakama kisheria hivyo, wanaomba mahakama iruhusu ombi hilo na kupewa ruhusa ya marekebisho hayo.
Wakili wa upande wa utetezi Mosses Mahuna alipinga ombi hilo na kuieleza mahakama hiyo kwamba upande wa serikali ulipaswa kuleta hoja hiyo mapema wakati shauri hilo likianza kusikilizwa .
Wakili Mahuna alieleza kuwa mshtakiwa Lengai ole Sabaya alisomewa mashtaka na kukutwa na kesi ya kujibu na baadaye mashahidi 11 wa upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao na mshtakiwa kuanza kujitetea in chief lakini upande wanjamhuri hawakuwahi kueleza mapungufu hayo.
Wakili Mahuna alidai kuwa hawapingi mshtakiwa namba moja Lengai Ole sabaya ila wanampinga mshtakiwa aliyeletwa katika hati ya mashtaka ambaye ni Lengai Ole Sayaba.
Hata hivyo Mara baada ya majibizano hayo hakimu mkazi mwandamizi Adira Amworo wa mahakama ya hakimu mkazi Arusha,aliahirisha shauri hilo kwa muda na baadaye alitoa uamuzi wa kutupa pingamizi hilo lililowekwa na upande wa utetezi.
Hakimu Amworo alieleza kwamba kwakuwa majina ya mshtakiwa wa kwanza yalisomwa sawa haiwezi kuathiri mwenendo wa kesi hiyo,hivyo maombi ya Kurekebisha majina kwenye hati ya mashtaka yamekubaliwa.
Washtakiwa kwa pamoja walisomewa upya mashtaka yao wakituhumiwa kutenda makosa matatu likiwemo la unyang'anyi wa kutumia silaha na kupora mali na fedha ambapo wote walikana mashtaka.
Katika kesi hiyo Sabaya na wenzake, Silvester Nyegu na Daniel Mbura wanashitakiwa kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha na kujipatia fedha kiasi cha Sh2.7 milioni mali ya Mohamed Saad.
Kosa la pili ni wizi wa kutumia silaha ambapo Sabaya na wenzake wawili wanatuhumiwa kuiba fedha Sh390,000 mali ya Bakari Msangi, ambaye ni Diwani wa Kata ya Sombetini jijini Arusha.
Kosa lingine Sabaya na wenzake wanatuhumiwa kuiba Sh35,000 pamoja na simu ya mkononi aina ya Tecno mali ya Ramadhani Rashid, ambaye inadaiwa walimtishia kwa silaha kisha kumfunga pingu.
Kesi hiyo inaendelea kwa upande wa sabaya kuhojiwa