SEASON 03:
A TRUE STORY BY INSIDERMAN
CHAPTER 21
Bila kupoteza muda, nikamnyanyua kwa haraka na kuingia naye chumbani kwa mara nyingine, nikiwa na dhamira ya kumleta Erica katika ulimwengu mpya wa mapenzi.
Nilimlaza kitandani, lakini moyo wangu haukuwa na amani ya kufanya kile kitendo. Japokuwa yeye alikuwa tayari mimi “nikate utepe,” dhamira yangu ilianza kunishtaki na kunihukumu. Kwa haraka nikawaza pale: Erica hajui chochote kuhusu historia yangu, hajui kwamba nina wake wawili. Kuitoa bikra yake bila kumwambia ukweli wa maisha yangu ingekuwa ukatili wa hali ya juu.
Ukweli sikuwa na malengo ya maisha naye, na sababu kubwa ya kumtongoza ilikuwa ni masuala ya kampuni. Kwa wakati ule, niliona ni bora ni-abort mission kuliko kufanya kosa ambalo lingeweza kunitesa baadaye. Erica kufikia umri wa miaka 24 akiwa bado bikra, maana yake alikuwa amekwepa mishale mingi sana ya wanaume.
Nilimtazama machoni, lakini kwa aibu akakwepesha macho. Nikamwambia kwa sauti ya chini,
MIMI: “Erica mama, nenda kaoge nikupeleke nyumbani. Muda umeenda sana sasa.”
Nikashuka kitandani na kuanza kuelekea sebuleni. Mara nikasikia sauti yake ikiniita kwa msisitizo.
ERICA: “Insider! What are you doing?”
MIMI: “Ni saa tatu usiku sahivi, na ulisema uncle wako ni mkali, inabidi uwe nyumbani.”
ERICA: “Mimi siendi nyumbani leo. Nitalala hapa.”
MIMI: “What? Huwezi kulala hapa wakati hukuwa na mpango wa kulala.”
ERICA: “Kwa nini unanifukuza? Kwa nini hutaki nilale kwako?”
MIMI: “Kwa sababu ninajali mahusiano yako na familia yako. Usiporudi nyumbani unafikiri watakuchukuliaje?”
ERICA: “Nilishaaga kwamba sitarudi leo. Nitarudi Jumapili.”
Nilishangaa kusikia hivyo, hakuwa amenieleza kabisa kwamba ana mpango wa kulala kwangu. Sikutaka kubishana naye tena, nikamwambia aoge halafu aje sebuleni tuzungumze kwa kina.
Nikiwa sebuleni, nilikuwa kwenye vita ya nafsi kati ya kumla au nimwache?. Moyo ulikuwa una-nihukumu na ukweli ni kwamba tayari nina wake wawili, wote wana watoto. Niliwaza pale siku akiujua ukweli, angeweza kuniletea matatizo makubwa au hata kunilaani.
“Je nimwambie ukweli kuhusu maisha yangu ili afanye maamuzi sahihi, au ninyamaze?”.
Baada ya kufikiri sana, nikaona bora nisimwambie chochote. Hakukuwa na sababu ya yeye kujua maisha yangu ya ndani. Hata hivyo wazo la kumuacha lilizidi kunigonga kichwani. Niliona ni bora nitafute sababu ya kuachana naye mapema, ili aendelee na maisha yake, mimi ningeishia kumchezea tu.
Simu yangu ikaanza kuita, nilipoangalia, nikakuta ni mama Aria-video call. Nikatoka nje, kibarazani, kupokea simu. Baada ya kuipokea na salamu fupi, alianza kunipasha habari mpya, kuwa ametoka kuzungumza na baba yake kuhusu kampuni tuliyokuwa tunaifuatilia, na mzee amemwambia aachane na mpango huo.
Nilibaki nimepigwa na butwaa baada ya kusikia kauli zile kutoka kwa mama mtoto na ukizingatia hatua kubwa zilikuwa zishaanza kufanyika;
MIMI: “Unafikiri ni kwa nini mzee amesema hivyo?”
IRYN: “Sielewi kabisa, amesema anarudi Jumapili tutaongea. But I feel like kuna mchezo unaendelea chini kwa chini, nimeanza kuwa na mashaka.”
MIMI: “Unahisi nini, mke wangu?”
IRYN: “Leo nimegundua ile nyumba anayoishi mama Janeth ni ya baba, alimpa.”
Binafisi nilikuwa nalijua hili kupitia Sumaiya, lakini nikajifanya sijui.
MIMI: “Umejuaje, baby? Haikuwa kwenye list ya mali zake?”
IRYN: “Alisema ameuza, lakini ukweli ni kwamba alimpa mama Janeth. Hata hii kampuni, nahisi atakuwa kapewa yeye.”
MIMI: “Una uhakika?”
IRYN: “Tutazungumza mengi tukionana, ngoja kwanza nihakikishe utafiti wangu.”
Tuliendelea kuzungumza mambo mengine muhimu kisha tukaagana. Niliendelea kukaa pale nje, kwa mbali nikasikia sauti ya Erica ikiniita.
Niliingia ndani na kumkuta jikoni, akipakua chakula kwa utulivu. Tulikaa pamoja mezani na kuanza kula, mazungumzo yakaanza taratibu. Nilichukua nafasi hiyo kuanzisha mada niliyokuwa nimeibeba moyoni, kutaka kufahamu historia yake ya mahusiano na sababu zilizofanya yakome.
Erica alitabasamu kwa upole kabla ya kuanza kunieleza. Alisema tangu shule ya msingi hadi kidato cha sita alisoma katika shule za Dini (Masister), na ametoka katika familia inayoshika sana misingi ya dini. Hivyo maisha yake yalijengwa juu ya nidhamu, maadili na heshima.
Kutokana na malezi hayo, Erica hakuwahi kuharakisha mambo ya mahusiano. Alisema wazi kwamba aliingia kwenye uhusiano wake wa kwanza alipokuwa mwaka wa tatu chuoni. Kabla ya hapo, alijikita zaidi kwenye masomo na kujilinda katika misingi aliyofundishwa.
Alipoanza kufunguka zaidi, aliniambia kwamba katika maisha yake yote ya kimapenzi, amewahi kuwa katika mahusiano na wanaume watatu tu!, na mimi nikiwa kama mwanaume wa tatu.
Mwanaume wa kwanza walikutana chuoni, na ukaribu wao ulianza kama urafiki wa kawaida, wakijadiliana masomo na kushirikiana masuala ya darasani. Kadri muda ulivyokwenda, urafiki huo uligeuka kuwa mapenzi, hasa mwishoni mwa mwaka wa tatu (2022), kipindi ambacho walikuwa wanajiandaa na mitihani ya mwisho (UE).
Baada ya kumaliza mitihani, waliendelea kuwasiliana na kujaribu kuendeleza uhusiano wao hata baada ya mazingira ya chuo kubadilika. Hata hivyo, kadri siku zilivyopita, mawasiliano yakaanza kupungua. Hakukuwa na tukio kubwa la kuvunja uhusiano, ila mapenzi yalizorota taratibu hadi yakapotea kimya kimya.
Kuhusu mwanaume wa pili, Erica alisema walikutana mwezi Februari mwaka huu (2023) baada ya yeye kuajiriwa na tasisi X. Alisema, walikutana kwenye moja ya seminar zilizofanyika katika kumbi za Bunge-Dodoma na kupelekea kubadilishana namba.
Walianzisha mahusiano kwa kasi na shauku kubwa, na mwanaume alionesha kumpenda na kumjali sana. Hata hivyo, mapema kabisa aligundua tofauti kubwa ya mitazamo kati yao. Alisema huyu ndiye mwanaume aliyekuwa akimpa changamoto kubwa zaidi, hasa kwa shinikizo la kutaka kuharakisha sex.
Siku ya kwanza alipokwenda nyumbani kwake, hali haikuwa kama alivyotarajia. Jamaa aliomba sex, lakini yeye hakuwa tayari kufanya maana alihitaji muda zaidi wa kumjua jamaa kabla hajafanya maamuzi ya kutoa bikra yake. Erica alisimulia kwa huzuni kwamba alijikuta akilazimishwa kufanya kitu ambacho hakikuwa kwenye mipango yake. Jambo hilo lilizua mabishano makali kati yao, na tangu hapo uhusiano wao haukuwa tena na amani.
Alipofika hapo, Erica alinitazama kwa makini, kiasi kwamba alitaka kuona ninapokeaje simulizi yake. Sauti yake ilikuwa tulivu, lakini ndani yake alionekana kutokuwa na imani na Wanaume. Na alisema kwamba katika mapenzi, si kila anayekuja anaelewa mipaka yako, na si kila anayesema anakupenda yuko tayari kuheshimu maamuzi yako.
Baada ya muda, Erica alikuja kugundua ukweli mchungu kwamba yule jamaa aliyekuwa naye kwenye mahusiano pale Dodoma alikuwa na wanawake wengi. Kumbe kipindi kile mimi naanza harakati zangu Dodoma, nakutana na Erica na kumtongoza, wakati ule alikuwa kwenye mahusiano na huyu boya.
MIMI: “Daah! pole sana, mimi niko tofauti na Wanaume wengine, naomba uwe na amani ukiwa nami.”
Erica alinitazama kwa macho ya aibu, na kutabasamu;
ERICA: “Ile siku tulipokuwa hotelini ukaniambia nije kwako pia nilale, nilijisemea huu ni mtego hapa sichomoki. Lakini nikajiuliza, sasa nitaachana na wanaume wangapi tena?”
Nilishtuka kidogo;
MIMI: “Kwahiyo unamaanisha umekuja nyumbani tayari ulikuwa unajua nini kinaweza kutokea?”
Alivunja ukimya kwa kicheko cha aibu.
ERICA: “Exactly! Uliposema twende chumbani, nikajisemea mambo yameanza sasa…”
MIMI: “Usiwe na wasiwasi, mimi siwezi kukubaka au kukufanyia jambo baya. Ila tambua mimi kama mwanaume Rijali siwezi kukaa na wewe ndani, halafu nikakuangalia tu, ilihali wewe ni mpenzi wangu.”
ERICA: “Insider mimi nimetokea kukuamini, naomba uniheshimu.”
MIMI: “Kukukaribisha nyumbani kwangu, hii ni moja ya heshima kubwa niliyokupa. Na hili suala la wewe kuwa bikra, umenifanya nianze kufikiria mustakabali wetu kwa uzito zaidi. Leo ninaahidi sitakufanya chochote, nataka ujipatie muda zaidi wa kutafakari maamuzi yako.”
Tukiwa deep kwenye maongezi, ghafla mlango ukagongwa.
“Ngo! Ngo! Ngo!”
Kisha nikasikia sauti ikiita, “Insider…!”
Nilitambua mara moja ile ilikuwa sauti ya kaka Bonny. Nikasimama haraka kwenda kufungua mlango.
MIMI: “Kaka, karibu sana ndugu yangu!”
BONNY: “Ahsante bro! Nimeambiwa na wife kuwa ulipita nyumbani kunisalimia. Nikasema siwezi kuacha hivyo, lazima nije nikuone ndugu yangu.”
Nilimkaribisha ndani seblen na alipoingia ndani, macho yake yalitua moja kwa moja kwa Erica ambaye alikuwa amekaa kwenye sofa. Bonny alionesha ile sura ya mtu anayetaka kujua, “Huyu ni nani?”
Sikumpa nafasi ya kubaki na maswali.
MIMI: “Kaka, huyu anaitwa Erica. Ni mpenzi wangu, anaishi hapa hapa Dodoma.”
Bonny akatabasamu kwa upana na kumwangalia vizuri zaidi;
BONNY: “Waoh! Shem, nimefurahi sana kukuona na kukufahamu, karibu sana.”
Erica, kwa tabasamu la heshima, akajibu:
ERICA: “Ahsante sana shem. Karibu tule.”
BONNY: “Ahsante, lakini chakula changu kipo mezani kinapoa. Nimetoroka tu kuja kumsalimia mdogo wangu.”
ERICA: “Shem, hata kidogo tu?”
BONNY: “Unataka nikagombane na shem wako?”
Sote tukacheka kwa pamoja, nikahitimisha kwa utambulisho rasmi zaidi:
MIMI: “Erica, huyu ni kaka yangu Bonny na ndiye kiongozi wetu hapa.”
ERICA: “Nimefurahi sana kukufahamu, shem wangu, karibu tena.”
Baada ya salamu tuliendelea kuzungumza mambo mengine hadi namaliza kula. Baada ya kumaliza kula, alituaga na mimi nikamsindikaza hadi nyumbani kwake nje kibarazani. Tuliendeleza maongezi yetu pale nje, alikuwa akishangaa sana kuona jinsi ambavyo ninabadili wanawake. Kwa utani akasema kuna haja ya kumpa namba ya mganga wangu, tulicheka sana kwa pamoja.
Baadaye mazungumzo yakahamia kwa Michael, yule jamaa aliyeniachia apartment yake. Bonny alisema bado wanawasiliana mara kwa mara, wakati mimi tayari nilikuwa nimepoteza mawasiliano naye kwa muda mrefu. Akanieleza pia kwamba kesho yake angeleta gari yake ofisini kwetu kwa ajili ya service. Nikamwambia awasiliane na kijana wangu mapema ili amuwekee nafasi kwenye ratiba.
Baada ya kuachana na kaka Bonny nilirudi ndani kwa Erica. Alikuwa ametulia, uso wake ukionesha kuwa na furaha na ile amani ya mwanamke aliyeridhika kuwa karibu na mtu anayempenda. Aliniambia kwamba angekaa hapo hadi Jumapili, kisha angerudi kwao. Na alisisitiza kwamba siku zote hizo alijipanga ziwe kwa ajili yangu.
Nilimuuliza kwa tahadhari,
“Je, hilo halitaleta shida nyumbani?”
“Niliaga ninasafiri kikazi. Nitarudi Jumapili kama nilivyosema.”
Kwa upande wangu, nilimweleza ukweli kwamba nilikuwa nishakata tiketi ya kurudi Dar es Salaam Jumamosi, na pia nilikuwa na majukumu ya kikazi yasiyoweza kusubiri, hivyo sikuwa na namna na nilipaswa kuondoka. Nikamhakikishia kuwa anaweza kuendelea kukaa hadi Jumapili, kisha funguo atamkabidhi mdogo wangu Juma, yule niliyempa gheto la nje.
Baada ya mazungumzo hayo, Erica aliaga anaenda kulala. Mimi nikabaki sebuleni, nikiendelea na kazi zangu binafsi hasa kupanga mikakati ya kampuni yangu. Lakini ukweli ni kwamba akili yangu haikuwa pale na mawazo yangu yalikuwa kwa Erica.
Nilijiambia kuwa sina future naye, sina mpango wa kumuoa. Na kama ni hivyo, je, si bora nimwache mapema kabla hajazama zaidi? Kwa mantiki yangu, kumuacha sasa ilikuwa ni kumwokoa. Lakini moyoni nilijua kwamba ataumia sana, ataona nimemtumia. Pia, ataamini nilikuwa naye kwa maslahi yangu binafsi tu! na baada ya kufanikisha nimeamua kuondoka. Nilijisemea “Potelea mbali” kama ataona nilikuwa namtumia kwa maslahi yangu binafsi, lakini ukweli utabaki sijafanya nae chochote.
Jumamosi asubuhi niliamka mapema, nikaoga na kujiandaa haraka, nikapanga begi langu vizuri, nikihakikisha kila kitu kiko sawa kwa ajili ya safari.
Kabla sijaondoka, nilikuwa na mazungumzo mafupi na mpenzi wangu Erica. Nilimwambia ninaondoka na tutawasiliana mara tu nitakapofika Dar es Salaam. Yeye kwa upande wake akasema ataendelea kuwepo hadi kesho ndipo angeondoka. Kulikuwa na utulivu fulani wa kipekee katika mazungumzo yetu, kama vile kila mmoja alijua umuhimu wa muda ule mfupi tulio nao.
Nikatoa simu yangu, nikafungua NMB Mobile App, kisha nikamgeukia.
“Nipe namba ya account yako,” nilimwambia kwa sauti ya upole.
Alinitazama kwa mshangao kidogo.
“Mpenzi, unataka kufanya nini?”
“Nataka nikuinguzie hela ya ahsante kwa kazi kubwa uliyofanya na nyingine ikusaidie kwenye matumizi yako binafsi.”
Alitikisa kichwa taratibu.
“No! Ahsante, niko vizuri. Hata usijali.”
Nilitabasamu.
“Naelewa upo vizuri, lakini linapokuja suala la kufanya majukumu yangu, naomba niachie, wewe weka account yako.”
Baada ya kusita kidogo, aliiweka, nikathibitisha muamala, kisha nikamkaribia na kumbusu shavuni kwa utulivu. Ilikuwa ni ishara ndogo tu ya shukrani na kujali kazi kubwa aliyofanya kwenye kampuni, kisha nikamuaga na kuondoka.
Hatua zangu zilielekea kwa Sanchi kabla ya kwenda airport. Kwa sasa, Sanchi alikuwa tayari ni Secretary wa kampuni, hivyo kulikuwa na mambo muhimu ya kupanga naye kabla sijapaa na kurejea Dar es Salaam.
******
Jumatatu ya asubuhi niliianza kwa safari ya kwenda Mbweni, nilipokwenda kumsalimia Jane na kuzungumzia maendeleo ya biashara yetu ya Kariakoo. Mazungumzo yetu yalikuwa ya kina, tukipanga mikakati ya kuboresha biashara na kupanua wigo wa wateja.
Katika maongezi hayo, tuligusia pia jambo la furaha, siku ya kuzaliwa ya Johson, anayetarajiwa kutimiza mwaka mwanzoni mwa mwezi Novemba. Jane alionekana mwenye hamasa kubwa, tayari alikuwa ameshaanza mipango ya kumfanyia sherehe nyumbani kwake, akiwaalika ndugu, jamaa na marafiki ili kusherehekea siku hiyo maalum.
Baada ya kuagana na Jane, niliendelea na ratiba yangu ya siku kwa kuelekea Masaki ofisini. Nilipofika tu na kuingia ndani, nilimkuta Hilda akiwa kwenye mazungumzo na mama Janeth. Sikutarajia kabisa kumwona mama pale ofisini, hivyo nilimsalimia kwa heshima. Mara moja akaomba nitoke naye nje tuzungumze kwa faragha.
Tukiwa kibarazani, mama alifungua mazungumzo kwa sauti ya utulivu lakini yenye uzito. Hakuwa amefurahishwa na mwenendo wangu wa ofisini, hasa kuchelewa kwa baadhi ya malipo yaliyopaswa kufanyika kwa wakati. Nilimweleza kwa uwazi kuwa nilikuwa nchini Afrika Kusini kwa dharura ya kifamilia- Iryn alikuwa ameugua hadi kulazwa hospitalini pamoja na mtoto.
Habari hizi zilimshangaza sana.
MAMA: “Iryn kaumwa hadi kulazwa? Mbona sina hizi taarifa?”
Alionekana kuguswa na kusikitishwa na kutofahamu kilichokuwa kikiendelea. Nilijaribu kumtuliza kwa kumweleza kuwa mambo yalikuwa ya ghafla, na kwa kuwa naye alikuwa safarini, haikuwa rahisi kupata taarifa kwa wakati.
Mazungumzo yale yaliiacha hewa nzito kidogo, dhahiri mama hakupenda namna alivyoshindwa kupata mawasiliano. Baada ya mazungumzo yale, mama aliingia garini na kuondoka akisema anaelekea ofisini kwake, na kwamba tungekutana baadaye kwa mazungumzo ya kina zaidi.
Baada ya mama kuondoka hata mimi pia sikuchelewa. Hivyo, niliwasha gari na kuelekea Kariakoo kukagua mwenendo wa biashara zetu. Nilishinda Kariakoo dukani hadi saa kumi na mbili jioni nikifuatilia hesabu, mauzo na mahitaji ya wateja. Baada ya hapo, niliamua kuelekea Masaki kwa ajili ya kukutana na mama kama tulivyokubaliana asubuhi.
Nikiwa njiani, nilimpigia simu kuthibitisha muda wa kukutana. Hata hivyo, aliniambia ratiba yake imekuwa ngumu kwa siku ya leo na tutaonana kesho yake. Nikabadili mwelekeo na kuanza safari ya kurudi nyumbani, and guess what nilipofika roundabout ya Kawe, simu ya Hilda ikaingia.
Niliacha simu ile ikaita hadi ikakata, akapiga kwa mara nyingine tena, na safari hii nikapokea kwa haraka. Aliniambia yuko ofisini, ananisubiri, na haoni dalili za mimi kurejea. Ndipo nikakumbuka ahadi niliyompa kwamba mara nitakaporudi Dar es Salaam tungeonana. Bila kusita, nilimwambia tukutane TIPS Mikocheni ili tuzungumze.
Niligeuza gari pale roundabout na kurudi nilikotoka. Nilipofika TIPS, nikaagiza kitimoto na ndizi choma huku nikimsubiri. Baada ya kama nusu saa, Hilda aliwasili. Naye akaagiza chakula, na mazungumzo yakaanza mara moja.
HILDA: “Mama amemind sana jinsi ambavyo ulikuwa hupatikani na ofisini huonekani.”
MIMI: “Nilimuona hata mimi, sema tumeyajenga. Nambie bossy wangu.”
HILDA: “Iryn na mtoto wanaendeleaje?”
MIMI: “Nashukuru Mungu, wanaendelea salama kabisa.”
Tuliendelea na maongezi mengine ya kawaida, kisha nikamweleza jambo ambalo lilikuwa moyoni mwangu kwa muda-kwamba mwezi huu natarajia kuanza masomo yangu, na nina mpango wa kuanza kuachia baadhi ya majukumu yangu ofisini.
Hilda alishtuka kidogo, wasiwasi ulionekana wazi usoni mwake. Nilimtuliza kwa kumwambia sitaondoka kabisa ila nitaendelea kufika ofisini kama kawaida, lakini nitapunguza majukumu ili niweze kuzingatia masomo.
Baada ya kuzungumza mambo ya kawaida, hatimaye tuliingia kwenye mada iliyotukutanisha pale kuhusu hatima yetu ya kile kilichotokea.
Nilikuwa nimeshamwelewa Hilda kwa muda mrefu. Hisia zake hazikuhitaji maneno mengi, zilionekana kwenye namna alivyonitazama, alivyojali, na alivyojitahidi kuwa karibu nami. Hata hivyo, nilipompa nafasi ya kuzungumza wazi, alianza kuzunguka, akitafuta maneno bila kufika kwenye kiini cha jambo.
Nilimuuliza direct bila kuficha,
MIMI: “Unataka mahusiano?”
Alishtuka kidogo! Akavuta pumzi ndefu, akatazama pembeni, lakini jibu halikutoka mara moja. Nikaamua kuendelea kuzungumza, nikisema kwa sauti tulivu lakini ya wazi:
“Hilda, natamani sana kuwa kwenye mahusiano na mwanamke mzuri kama wewe. Lakini suala la mahusiano kwetu sisi ni gumu sana kutokana na mazingira yetu. Unajua kabisa nina wake wawili, na wote wana watoto. Zaidi ya hapo, Iryn bado ni boss wetu, fikiria siku akija kugundua kuwa tupo kwenye mahusiano unadhani atatusamehe?”
Ukimya mzito ulitanda mezani, zaidi ni sauti ya mziki wa taratibu ndio ilikuwa ikisikika muda huu. Hilda alikaa kimya kwa muda, akitafakari. Hatimaye akasema kwa sauti ya chini, yenye hisia kali;
HILDA: “Insider nashindwa kuelewa kwa nini natamani sana kuwa kwenye mahusiano. I don’t know why, najikuta tu niko hivyo.”
Maneno yake yalikuwa ya kweli, lakini ni hisia tu zilizomzidi nguvu.
MIMI: “Naelewa na kuheshimu hisia zako, lakini sipendi kukuingiza kwenye ligi na Iryn. Inaweza kuwa mbaya sana akija kujua kinachoendelea. Huu ndio wasiwasi wangu mkubwa, mimi na wewe tutaendelea kuwa washikaji hata usijali.
Nilichagua kuwa mkweli bila kupaka sukari. Nilijua wazi kuwa mazingira ya kazi yalikuwa magumu. Pia nilijua, kwa namna fulani, Hilda asingeweza kuondoka kazini, hali iliyofanya niwe na jeuri ya kuongea vile.
Baada ya mazungumzo marefu, niliondoka pale Tips Mikocheni nikiwa na mawazo mazito kichwani. Ukweli niliomwambia Hilda haukuwa mwepesi, lakini nilijua ni lazima usemwe tu. Katika mawazo hayo, pia nikakumbuka kwamba sikuwa nimewasiliana na dada yangu kuhusu suala la Iryn, hivyo nikampigia simu.
Nikiwa njiani kurudi home, nilikuwa kwenye mawasiliano marefu na dada yangu hadi nafika nyumbani. Tulizungumza kwa kina kuhusu Iryn maana nilimweleza kila kitu tulichojadili kipindi nikiwa South Africa hasa juu ya hisia zangu, changamoto, na sintofahamu iliyokuwa ikiendelea.
Nilitamani kujua ni hatua gani ameshachukua hadi sasa, lakini aliniambia niwe na subira. Yeye alidai alikuwa na mpango madhubuti anaouandaa, na muda ukifika ningeona matokeo yake.
Nilinyamaza kimya kwa sekunde chache, sikuwa na la kuongeza. Lakini moyoni nilihisi huenda dada yangu anasubiri kwanza ajifungue ndipo aanze kushughulika kwa uzito na suala la Iryn. Mawazo yalinijaa, lakini sikuwa na uhakika wa lolote na hata sikujua mwisho wa jambo hili utakuwaje.
Kesho yake asubuhi, nikiwa tayari nimeketi ofisini na kupitia majukumu ya siku, simu yangu iliita. Ilikuwa ni simu ya mama Janeth na baada ya kuipokea, sauti yake ilikuwa tulivu lakini yenye uzito fulani.
“Naomba upitie ofisini kwangu leo, tuna mazungumzo machache,”
“Sawa mama nitakuja sio muda mrefu.”
Baada ya kumaliza mambo ya haraka mezani kwangu, niliaga na kuelekea kumuona mama, ofisini kwake. Nilidhani tungekaa ofisini kwake kama kawaida, lakini safari hii tulikaa sehemu ya mapumziko iliyo tulivu zaidi. Hapo ndipo nilihisi kuwa mazungumzo yale hayakuwa ya kawaida.
Tulipokaa, hakutaka kupoteza muda, alionekana kuwa na haraka, na baada ya salamu fupi kuhusu maendeleo ya familia na mengine kwa ujumla, straight akaenda kwenye dhumuni la wito ule;
MAMA: “Insider, nakujua wewe ni mmoja wa watu wachapakazi na huwa uko serious na mambo yako. Lakini hatua uliyofikia sasa si nzuri, inaathiri image na utendaji wako na hata kampuni kwa ujumla. Umeanza kuingiza mapenzi kwenye kazi, na hilo si jambo zuri kwa maendeleo yako.”
Alitulia kidogo kisha akaongeza kwa sauti ya upole lakini yenye msisitizo:
“Namheshimu sana Iryn kama binti yangu, na sasa wewe ni kama mkwe wangu. Unapokesea, lazima nikwambie ukweli ili urekebishe.”
Nilikaa kimya maana maneno yake yalikuwa mazito. Kabla hata sijapata cha kujibu, aliendelea kuongea;
“Iryn ni Managing Director wa kampuni hii, lakini ni lazima uheshimu ofisi, hata kama ni mke wako. Mimi ni HR na pia Director, lakini kila ninaposafiri huwa natuma taarifa rasmi kwa email. Wewe unaondoka kimyakimya, hutoi tarifa na sio mara moja-imekuwa ni tabia yako, unajisahau sana, na hilo si zuri.”
Nilinyamaza kwa muda kabla sijaamua kuzungumza;
MIMI: “Mama, unachosema ni sahihi. Safari nyingi hutokea ghafla bila mipango ya muda mrefu, lakini huwa najitahidi kutoa taarifa kwa Hilda au Lucy. Naomba samahani kama haijawa kwa utaratibu unaotakiwa. Na hili halitajirudia. Pia naomba usifikiri Iryn ndiye chanzo cha haya yote, hapana mama.”
MAMA: “Mimi niko kukuongoza na kukuambia pale ninapoona unakosea. Ukifanya vizuri nakusifu, lakini kwa sasa umekuwa too much, Insider. Mapenzi yamekukolea hadi unasahau majukumu yako.”
Katika mazungumzo haya, mimi nilikuwa kimya tu, ni mara chache sana niliweza kuongea. Mazungumzo yangu na mama hayakuchukua muda mrefu. Tulipomaliza, alinisisitiza nisijisikie vibaya kwa aliyoyasema, kisha tukaagana kwa utulivu.
Njiani nikirudi ofisini, mawazo yalinijia kwa wingi sana, nilikuwa nikijiuliza kwa nini mama aliamua kusema hayo leo? Moyoni nilihisi huenda amekuwa akibeba jambo hili kwa muda mrefu, na hatimaye akaona leo ni wakati sahihi wa kulitoa.
Kwa muda nilifikiria kumshirikisha Iryn, lakini nikajizuia. Ukweli mama alizungumza si tu kama mzazi, bali pia kama mtu mwenye wajibu na uzoefu wa kazi kama Director na HR. Niliona mantiki ya msimamo wake, hivyo nikaamua kunyamaza na kuendelea na siku yangu.
Nilirudi ofisini, nikajitumbukiza kwenye majukumu ya mchana. Baadaye nikapokea simu kutoka kwa rafiki yangu Manuel aliyeko Switzerland. Kwa sauti yenye furaha, alinijulisha kwamba wiki ijayo anatarajia kutua Tanzania, na lazima tukutane. Habari hiyo ilinijaza bashasha na nikamkaribisha kwa moyo mkunjufu.
Ilikuwa saa tano za usiku nikiwa nyumbani nilipopigiwa simu na shemeji yangu-mume wa dada yangu. Kwa sauti ya furaha alinipa taarifa kwamba dada yangu amejifungua salama, na wamebahatika kupata mtoto wa kike.
Baada ya kunipa taarifa hiyo, shemeji alikata simu. Nikabaki nikiwa nimezama mawazoni: imekuwaje ghafla hivi? Jana tu niliongea na dada yangu, na hakutaja kabisa dalili zozote za kujifungua.
Wakati napokea taarifa hizo nilikuwa kitandani pamoja na mke wangu, na alikuwa amesikia kila neno tulilozungumza. Baada ya simu kukatika, alisogea karibu nami na tukaanza kujadili habari ile njema. Tukapanga kwamba kesho tungesafiri wote kwenda Arusha, halafu yeye angebaki huko kwa siku chache kisha angerudi Dar es Salaam.
Tulipokuwa bado tunazungumza, simu yangu ikaanza kuita tena pale kitandani. Mke wangu akaichukua na kunipa. Nilipotazama kwenye screen, nikaona ni Erica anayepiga.
Muda wote huo mke wangu alikuwa amenikazia macho, akifuatilia kila hatua nitakayochukua. Hatimaye akavunja ukimya:
“Baba Junior… kwa nini hupokei hiyo simu?”