Nikupongeze Mnyika kwa imani uliyopewa. Hujapewa ukuu bali utumishi. Hujapewa starehe bali mateso kutoka kwa wadhulumaji. Hujapewa sherehe bali huzuni ya mateso yako na wale utakaowaongoza. Hujapewa utajiri bali kufukarishwa na wenye roho ya ibilisi. Hujapewa utukufu bali udhalilisho unaofanywa na mbweha waliovaa ngozi za kondoo kuwahadaa Watanzania.
Mnyika unayajua hayo, umeyapokea hayo na umekubali kuyabeba. Hakika najua utasimama katika ukweli kama wale mitume waliokuwa wakisimama mbele ya watawala ibilisi wakitakiwa waikane imani yao ili wawe huru ili wapate starehe, lakini wakayakataa ya ibilisi, wakasimama katika ukweli kwa sababu walijua dhamira wanazozitumikia walipewa na zipo chini ya mwenye mamlaka makuu, mamlaka ya juu kabisa katika ukuu. Mtumikie aliye mkuu, japo mbwa kichaa hutisha maana anaweza kukung'ata na kukujeruhi. Lakini ujuacho ni kuwa mbwa kichaa pamoja na kuwa na uwezo wa kung'ata bado yeye ni mbwa kichaa. Watu wote walio wazima wanajua mbwa kichaa ni hatari kwa kila mmoja hata kwa mfugaji. Mbwa kichaa haishi milele, hata asipofanywa chochote, ukichaa unaomfanya ajeruhi watu ndio huo huo humwangamiza na yeye.
Mnyika simama katika ukweli, uuishi ukweli, uupiganie ukweli maana ukweli hauchangamanishwi na ulaghai au unafiki. Utambue hakuna kupigania haki kama hakuna mdhulumaji, hakuna kupigania uhuru kama hakuna mkoloni, hakuna kupigania ukombozi kama hakuna mtesaji, hakuna kupigania demokrasia kama hakuna dikteta. Basi ni mtu mwovu ndiye humtangaza yeye aliye mpambanaji dhidi ya dhuluma.
Tupo katika utawala ambao unafanya kazi ya kuwainua wapigania haki, wapigania uhuru na demokrasia. Hii ni fursa iliyo njema ya kuyainua majina makuu ambayo bila dhuluma, yasingeweza kujulikana. Fahamuni, tajiri hawezi kuwa maarufu kama hakuna maskini. Mpigania demokrasia hawezi kuwepo kama hakuna dikteta.
Mungu akubariki Mnyika, ukasimame kataka uimara.