Wakati huo haikuwa sawa na Leo ni Bora yeye umalaya wake ulitupatia uhuru
Bandari zinapambaniwa Sh trilioni 2.7
*Kampuni za familia huvuna milioni 400 kila mwezi, zinalinda ICD zisifungwe
*Mombasa kontena husafirishwa kwa dola 1,300; Dar es Salaam ni dola 3,500
*Wakubwa wamejijengea mfumo unaowahakikishia dola 1,200 kila kontena
*Wanapambana mrija usikatwe, DP World kupewa mkataba kama wa TICTS
Na Mwandishi Wetu
Siri zimeanza kufichuka baada ya baadhi ya watumishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Kupakua na Kupakia Makontena Bandarini (TICTS) kujitokeza na kusema kuwa wao na taifa la Tanzania wamenyonywa kwa muda mrefu.
Wanasema mrija wa unyonyaji huo ambao unaelekea tamati, ndio unafanya baadhi ya watu wapige kelele baada ya mkataba wa TICTS kwisha.
Wamelieleza JAMHURI kuwa TICTS ambayo inamilikiwa na kampuni mbili zenye ubia; Hutchison Ports ya China yenye asilimia 75, na Tanzania Harbours Investment yenye asilimia 25, ziliisajili kama kampuni ya Kitanzania kwa jina la TICTS.
“Kwa kweli tunawaangalia watu wanasema hadi wanatokwa mishipa, ila leo tukasema acha na sisi tupate nafasi ya kueleza upande wa pili, pengine watatuelewa machungu yaliyotupata na nchi ilivyopoteza mapato kwa muda mrefu. Sisi katika makubaliano ya kuundwa kwa TICTS ilikuwa wafanyakazi tupewe asilimia 5 ya hisa za kampuni hiyo kupitia DOWUTA.
“DOWUTA ambacho ni Chama cha Wafanyakazi wa Shuguli za Meli na Bandari Tanzania, TICTS ilimilikishwa hisa kupitia TICTS Employees Trust kwa kutupatia asilimia 5 ya hisa kwenye kampuni hiyo.
“Ajabu sisi wafanyakazi wote tuliishia kuwa tunapewa dola 300,000 kwa mwaka bila kujali kampuni imepata faida kiasi gani. Hii ni tofauti na Spain, Indonesia au Uingereza ambako Kampuni ya Hutchison Ports imefanya uwekezaji kama hapa kwetu. Kule inatoa hadi dola milioni 2 (tarkiban Sh bilioni 5) kwa mwezi kwa wafanyakazi kulingana na faida iliyopatikana,” amesema mtoa taarifa.
Mfanyakazi mwingine ameliambia JAMHURI kuwa mgogoro wote wanaouona wananchi, wala si uzuri wa TICTS au ubaya wa DP World, bali kuna familia inayopigania uchumi wa familia kama familia.
“Hapo bandarini TICTS wanahudumia karibu kontena 79,000 kwa mwezi. Hapa ndipo ulipolala mchezo kati ya wenye meli, TICTS na wamiliki wa Bandari Kavu (ICD) zinazoongeza gharama ya kusafirisha kontena kuja Tanzania.
“Meli zinapopakia kontena kwenda Mombasa, Kenya kutoka China zinatoza dola 1,300 kwa kila kontena. Sisi hapa wanasema watalipishwa wharfage kubwa kutokana na meli kuchelewa kushusha mzigo kwa hadi siku 20. Hizi meli hata ukienda hapo baharini tunaziona zimetia nanga muda mrefu bila kuingia bandarini. Wakati mwingine si kwamba hakuna uwezekano wa kontena kutolewa ndani ya siku tatu, bali wakifanya hivyo ICDs zitakosa biashara.
“Kila kontena likienda kwenye ICD linatozwa dola 1,200, achilia mbali zile dola 80 na tozo nyingine ndogo ndogo wanazotoza. Ukichukua kontena 79,000 mara dola 1,200 tayari inakuwa dola 94,800,000. Kiasi hiki cha fedha ukizidisha mara Sh 2,400 ambao ndio wastani wa kubadili fedha ya dola kwa shilingi ya Tanzania kwa sasa, unakuta wanapata jumla ya Sh bilioni 227 kila mwezi sawa na Sh trilioni 2.73 kwa mwaka. Hawa kwa vyovyote vile baada ya kupata kiasi hiki cha fedha kila mwaka kwa miaka 22, hawawezi kukubali kuachia kirahisi,” amesema mfanyakazi mwingine.
JAMHURI limeonyeshwa taarifa za kampuni ya uwakili, kampuni ya kukopesha, kampuni ya usafirishaji, benki moja ambayo mmiliki wake ana ubia kwenye TICTS, moja ya ICD kubwa iliyokuwa inamilikiwa na Bandari ikiwa imekodishwa kwa TICS ambayo miaka yote haikulipa pango ila baada ya kupewa mwekezaji mwingine imeishatoa dola milioni 2.5 ndani ya muda mfupi na nyingine nyingi.
Ipo kampuni ya familia iliyokuwa inafanya kazi ya kupakia shaba, hii imekuwa ikilipwa dola 80,000 kila mwezi sawa na Sh milioni 192 au Sh bilioni 2.3 kwa mwaka. Ipo kampuni ya usafirishaji yenye jina la ‘Ndege Anayeruka’, ambayo kwa mwezi inapata wastani wa Sh milioni 160 kama gharama za kusafirisha wafanyakazi kila mwezi sawa na Sh bilioni 1.92 kwa mwaka.
“Ipo kampuni ya vibarua inayolipwa dola 70,000 kila mwezi (sawa na Sh milioni 168 kwa mwezi au Sh bilioni 2 kwa mwaka). Wanawakodishia wafanyakazi wageni 10 magari ya VX kwa gharama ya dola 300 kwa siku (sawa na Sh 720,000 au Sh milioni 21.6 kwa mwezi kwa mtu mmoja au Sh milioni 259.2 kwa wafanyakazi wote 10 kwa mwaka).
“Hawa wanayo kampuni ya matairi inalipwa dola 80,000 kila mwezi sawa na Sh milioni 192 au bilioni 2.3 kwa mwaka, huku kampuni nyingine mbili za vibarua zikilipwa dola 340,000 kila mwezi kwa ujumla wake sawa na Sh milioni 816 kwa mwezi au Sh bilioni 9.79 kwa mwaka. Kampuni ya ulinzi waliyo na vinasaba nayo inalipwa dola 180,000 kwa mwezi sawa na Sh milioni 432 kwa mwezi au Sh bilioni 5.18 kwa mwaka,” amesema mfanyakazi huyo.
Mfanyakazi mwingine anasema: “Tangu Januari 2023 walipoingia TPA na kuanza kuendesha kitengo cha kontena, wafanyakazi tumelipwa bonasi hadi tukashangaa. Kati ya Januari hadi sasa kila mwezi tunapokea bonasi. Ilianza tukalipwa dola 475,000 sawa na Sh bilioni 1.14 hadi Mei, 2023 tumepata bonasi ya dola 800,000 sawa na Sh bilioni 1.92. Hii bonasi inagawanywa kwa usawa kwa wafanyakazi wote 650 wa TICTS - kuna mtu anapata bonasi ya Sh milioni 2, ambayo ni zaidi ya mshahara wake. Wakati wa TICS bonasi ilikuwa ni dola 110,000, mara moja tu ndipo tulipewa dola 310,000.”
Muda wote wafanyakazi wa TICTS walilazimishwa kuchukua mkopo kwenye taasisi moja tu ambayo iliwakopesha kwa riba isiyowapa uhuru wa kuchagua. Hata bima ya afya walielekezwa kwenye kampuni moja tu, ambayo ina uhusiano na mmoja wa wawekezaji.
Mwanasheria mmoja aliyesema yeye hataki kuingia kwenye vita ya maneno, ameliambia JAMHURI: “Hapa wanachoelezwa Watanzania kuwa Bandari inauzwa ni tofauti na uhalisia. Wanachofanya wanaosema hivyo wanalenga kuwachochea Watanzania wapandishe hasira, kumbe wanatetea kitumbua chao.
“Hao wanaopinga mkataba kwa vitisho, ukiangalia historia zao ziko wazi juu ya nani aliwasomesha, wamekuwa wakipata nini kutoka TICTS kupitia mlango wa nyuma, na sasa wanataka nini kiendelee.
“Kuna mawaziri na baadhi ya vigogo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika hili hutakaa usikie kauli yao. Hawa ni wasaidizi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, lakini ni wanufaika wakubwa wa ICDs. Wanatumia nguvu kubwa kuikataa DP World, maana wanafahamu kuwa biashara ya kupata dola 1,200 kila kontena inakwenda kufa.
“Wanafahamu kuwa gharama ya kusafirisha kontena inakwenda kushuka chini ya DP World wakiishawekeza katika teknolojia, mteja ataweza kulipia gharama za kontena lake na itafikia hatua ya kontena kutoka kwenye meli na kupakiwa kwenye treni au lori la mteja kwenda dukani kwake moja kwa moja. Hapa mrija wa ICD utakuwa umekatika. Tena hawa wenye ICDs ndio wabaya zaidi, maana hawaonekani popote angalau kama ilivyo TICTS.”
Juhudi za kuwapata TICTS kuzungumzia suala hili hazikuzaa matunda baada ya ofisa mwandamizi aliyekataa kutajwa jina gazetini kusema: “Sisi TICTS hatuna mgogoro na serikali. Mkataba wetu ulikwisha, amepatikana au atapatikana mwekezaji mwingine, hatuna la kusema. Nafahamu watu wanasema sisi ndio tunachochea kelele zinazoendelea juu ya mkataba wa Bandari, ila uhalisia hatutaki hata kutajwa kwenye vyombo vya habari.”
Serikali ya Tanzania Oktoba mwaka jana iliingia makubaliano (IGA) na Serikali ya Dubai kwa ajili ya kuendeleza Bandari ya Dar es Salaam na maeneo mengine ya kiuchumi. Makubaliano hayo yanaelekeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Bandari la Dubai la DP World wazungumze na waingie Mkataba wa Nchi Mwenyeji (HGA) na mikataba ya uendeshaji itakayosimamia utekelezaji wa makubaliano hayo kwa kuweka muda na masharti ya utekelezaji wa mikataba itakayoingiwa.
Hata hivyo, kumekuwapo mjadala mkubwa nchini kuwa DP World imepewa mamlaka makubwa kupitia Mkataba wa IGA; jambo ambalo limefafanuliwa na serikali mara nyingi kuwa mkataba wenyewe haujaingiwa, bali kilichosainiwa ni makubaliano yanayotoa mwongozo wa maeneo ya ushirikiano katika mikataba itakayoingiwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wiki iliyopita amekaririwa akisema DP World watapewa mkataba unaofanana na waliokuwa nao TICTS kwa nia ya kuongeza ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam, kukuza ajira na kuongeza mapato ya nchi yatokanayo na Bandari.
Ends…