Makundi ya kusaka urais 2015 yaanza
*Mawili yanatoka katika mtandao
*Kauli za Nyerere zatumiwa vibaya
* Vigogo wawekeana vigingi kuingia NEC
*Wengi waiga mbinu ya Kikwete
Na Boniphace Makene
HARAKATI za kusaka madaraka ndani ya chama tawala (CCM) katika ngazi tofauti, zimeanza kuchukua sura mpya, huku kukiibuka makundi yenye uchu wa kujaza nafasi mbalimbali, wote wakilenga kujijengea mtaji wa kisiasa hasa katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili, umebaini kuwa makundi yaliyopo yanaiga mtindo alioutumia Rais Jakaya Kikwete, ambaye mpaka alipoukwaa urais katika uchaguzi uliopita, alitumia takribani miaka kumi kujiimarisha katika chama na kujenga mtandao uliomuwezesha kuukwaa uteuzi wa chama.
Rais Kikwete mwenyewe aliwahi kukiri kuwa katika harakati za kusaka urais, alijiandaa kwa takribani miaka kumi, hali ambayo imewafanya wenye dhamira ya kutaka kumrithi amalizapo muda wake, kuanza kujipanga kufuata nyayo hizo.
Hata hivyo kwa mujibu wa kanuni ya 33 (1) ya uchaguzi ya CCM toleo la mwaka 2005, mwanachama yeyote haruhusiwi kuanza kampeni za aina yoyote kabla ya kuteuliwa.
"Wanachama wenye nia ya kugombea hawaruhusiwi kufanya kampeni ya aina yoyote kabla ya majina yao kuteuliwa na kikao kinachohusika," kanuni hiyo inaelekeza.
Hivi sasa kuna habari kwamba tayari yapo makundi mawili yanayotafuta fursa za kuukwaa urais baada ya Kikwete. Makundi haya yalikuwa pia yakimuunga mkono Kikwete katika harakati zake na yanafahamu vema mbinu alizotumia, hali inayowapa fursa ya kuzitumia bila kumezwa na mkondo wa sheria na kanuni za uchaguzi za CCM.
Gazeti hili pia limebaini kuwepo kwa kutofautiana kuhusu nafasi za wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama(NEC). Baadhi ya makada wa CCM walio nje ya serikali wanaitazama NEC kama Bunge la chama, na wamedhamiria kuingia ndani ya chombo hicho ili waweze kutoa changamoto za uhakika kwa serikali.
Kundi hili linaamini kuwa uwakilishi katika NEC unahitaji watu walio nje ya serikali ili waweze kuipangia serikali agenda za kufuata na sio kukubaliana na kila mpango wa serikali.
"Ni vigumu kwa waziri kumueleza ukweli rais wa nchi wakati anafahamu kuwa yuko katika Baraza. Hapa Rais anaingia kama Mwenyekiti na anatakiwa kutokuta wajumbe ambao si mawaziri ili kuweza kujenga mipango mizuri ya kuendesha nchi," alisema kada mmoja wa CCM huku akibainisha pia dhana ya chama legelege kuzaa serikali legelege.
Mkakati huo unaoonekana kuwa umelenga zaidi kuwakwamisha mawaziri na waandamizi wengine wa serikali ili wasiingie katika NEC.
Lakini kundi la mawaziri na viongozi wengine waandamizi ndani ya serikali nao wana lengo mahsusi la kuhakikisha kuwa chama kinafanya yale serikali inayoyapenda na sio vinginevyo. Hawa wanataka ujumbe wa NEC na ule wa Kamati Kuu(CC) kwa ajili ya kuhakikisha kuwa chama katika ngazi hizi muhimu za juu kinashikiliwa na watu wenye utii usio na shaka kwa serikali.
"Huu ni wakati mzuri wa kukirejesha chama nyumbani. Tunataka kuwa na chama kinachotii maamuzi ya serikali hivyo hiki ni kipindi kizuri kwetu kutumia mbinu za aina yoyote kufanikisha hili," waziri mmoja mwenye nia ya kuwania ujumbe wa NEC amelidokeza gazeti hili.
Wakati haya yakiendelea, hali ya kujitangaza na kujipigia chapuo kwa wanachama wa CCM inazidi kuchukua kasi. Wapo baadhi ya wajumbe ambao wametangaza nia na kukutana na ukuta pale walipowafikia vigogo wanaodhani kuwa wanaweza kuwasaidia kupata nafasi wazitakazo.
Mmoja wa mhanga wa hali hii ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Amina Chifupa, ambaye ameweka bayana nia yake ya kutaka kuongoza Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya chama hicho (UVCCM) katika uchaguzi wa mwakani, na hivyo kwenda kumuomba kigogo mmoja wa umoja huo ampigie debe, lakini akagonga mwamba.
Kigogo huyo naye kuonyesha namna alivyo na nafasi muhimu, akatumia kauli ya Mwalimu Julius Nyerere, aliyoitumia wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995. Nyerere alisema; "siwezi kuruhusu mbwa kubweka katika nchi yangu." Kauli hii iliwalenga viongozi dhaifu kutoka kambi ya upinzani waliokuwa wakitaka urais.
Kigogo huyo wa UVCCM yeye akamwambia Chifupa kuwa; "siwezi kukuruhusu kuongoza UVCCM labda mauti yanikute." Kigogo huyo alipoulizwa maana ya kutumia kauli hiyo nzito inayofinya haki na uhuru wa demokrasia, alishindwa kutoa sababu za aina yoyote huku akisisitiza tu kuwa Chifupa hana sifa za kuiongoza UVCCM.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Amos Makalla, alikaririwa na vyombo vya habari baadaye akisema kuwa; "anayetamani madaraka sasa ni mtu asiyejiamini." Kauli hii haikutazama wala kulenga kuvunjwa kwa taratibu na kanuni za uchaguzi za CCM, ambazo Chifupa anaonekana tayari kuzivunja na kuzikiuka.
Ngome ya UVCCM inaelezwa ilitumiwa vilivyo na kambi ya Kikwete katika kufanikisha kupata kiti cha urais mwaka 2005. Kuna vigogo wanaotamani nafasi mwaka 2015 ambao wanaitazama UVCCM kama eneo muhimu kabisa linaloweza kumfanikisha mgombea yeyote kupata uteuzi katika chama.
Kwa sasa kuna taarifa kuwa kigogo mmoja kutoka UVCCM ana nia ya kusaka urais 2015 na anachofanya yeye na mtandao wake kwa sasa ni kuhakikisha wanapata warithi ambao watakuwa wagumu kurubuniwa na kuiasi kambi iliyowaingiza madarakani.
Kuonyesha kuwa harakati za kujipanga kwa uongozi ndani ya chama hicho zimeshika hatamu, hivi karibuni Kamati Kuu ya CCM iliwasimamisha makada watano wa chama hicho na kuwaweka katika uangalizi kwa miezi 18 kwa madai kuwa wamekiuka kanuni kwa kuanza kampeni kabla ya wakati.
Mjumbe mmoja wa NEC alipoulizwa mazingira ya kutolewa kwa adhabu kama hizo alisema ingawa zipo mara kwa mara, lakini mara nyingi zinawalenga watu ambao hawatakiwi katika chama au mfumo wa kipindi hicho.
"Kilichopo hapa kuna mambo kama kulipa visasi na pia suala hili la makundi kudumu hata baada ya chaguzi. Ni wazi wengi sasa wanafanya kampeni kupitia mikutano ya serikali na shughuli nyingine za kijamii lakini hatujaona wakiadhibiwa," kilieleza chanzo hicho.
Kitendo cha Kamati Kuu kutoa adhabu kinatoa picha tu ya namna kulivyo na papara za kusaka madaraka kwa makundi kadhaa huku kampeni za kuvunjana nguvu zikishika kasi chini kwa chini. Kila kundi lina nia na malengo yake lakini kubwa ni kutofautiana kulikoambatana na harakati za urais 2005.
Kuna makundi yanayotaka kurejesha heshima baada ya kuonekana yanabaguliwa katika shughuli za chama na serikali, huku kundi la mtandao likijivunia kutumia nguvu zake kubakia serikalini na pia kukiweka mkononi chama.
Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Phillip Mangula, alipoulizwa na Mwananchi Jumapili katika mahojiano maalum yaliyofanyika katikati ya wiki alisema; "chama kinatoa adhabu pale anapopatikana mtu wa kutoa shtaka na kisha kufuatiwa na uchunguzi. Huenda kuna matukio yamefanyika lakini hakukuwa na mtu wa kushtaki au ushahidi kukosekana."
Kauli hiyo ya Mangula ilitokana na swali lililotaka kujua nini kilifanya kambi mojawapo ifanye kampeni kwa zaidi ya miaka kumi bila kugundulika huku ikiwa imevunja utaratibu wa kanuni za uchaguzi namba 33 hasa vifungu vya 1, 4 na 7.
Vifungu hivyo kwa ujumla wake vinaelezea, mwiko wa kuundwa vikundi visivyo rasmi ndani ya chama na kushiriki katika kampeni za kichinichini, kutumia jumuiya ya chama ili kumjenga mgombea mmoja na kubomoa wengine na kuanza kampeni kabla ya wakati.
Ni jambo lililo wazi sasa kuwa kundi la mtandao lililomuunga mkono Kikwete bado lipo huku kukiwa na taarifa zinazoeleza kugawanyika kwa kundi hilo kuwa mawili yaani mtandao maslahi na mtandao matumaini.
Wachunguzi wa mambo ya siasa wanaeleza pia kuwa, hata makundi yanayotamani urais mwaka 2015 yanatoka katika kundi hili huku sifa zilizotumika kuangusha wagombea wenye umri mkubwa sasa zikibadilishwa kufuatia kuwepo makundi yanayotofautiana kiumri.
"Mtu yeyote anaweza kugombea la msingi ni umri wa kuanzia ambao ni miaka 40. Unaweza kuongoza hata ukiwa na miaka 80 japokuwa mimi naona ni muda mzuri wa kupumzika badala ya kung'ang'ania kuwa madarakani," anasema Mangula ambaye sasa kaamua kuwa mkulima baada ya kutumikia CCM kama Katibu Mkuu kwa miaka 10, kipindi kirefu kuliko Katibu yeyote mwingine aliyewahi kuratibu kazi za chama hicho.
CCM inafanya uchaguzi wake mkuu mwaka huu kuanzia ngazi za shina hadi taifa. Uchaguzi huo utaendelea mwakani ambapo jumuiya mbalimbali zilizomo katika CCM zitafanya chaguzi zake kuanzia ngazi za chini kabisa hadi taifa.
SOURCE:
http://www.mwananchi.co.tz/habari/habari0.asp