MTV,
UCHOCHEZI WA MAKARATASI YA ALLY SYKES KWA WAAFRIKA WA TANGANYIKA: KISA CHA ALLY SYKES NA AMRI KWEYAMBA KACHERO WA SPECIAL BRANCH 1953
Ilikuwa katika miaka ya 1980s wakati huo nafanya utafiti wa kitabu cha Abdul Sykes ni yangu ikiwa kuandika historia ya TANU kupitia Nyaraka za Sykes.
Nimekuta nyaraka iliyokuwa imechapwa kwa ''cyclostyle,'' juu imeandikwa ''Kwa Waafrika Wote wa Tanganyika.''
Ujumbe uliokuwapo ni kuwataka Waafrika wote wa Tanganyika wajiunge na TAA kwani kuna jambo kubwa linakuja.
Nilikuwa naandika katikati ya juma na siku ya Jumamosi ndiyo siku kama nilikuwa na maswali nakwenda ofisini kwa Ally Sykes kupata majibu na maelezo mengine.
Nilipomwonyesha nyaraka ile Ally Sykes nilimuona kachangamka na kafurahi sana.
Akanambia kuwa nyaraka ile ilimletea matatizo makubwa.
Siku hiyo ndiyo aliponihadithia kisa cha yeye kuitwa na kusakwa kama mchochezi.
Ally Sykes anasema baada ya kuwa na uhakika kuwa mwaka wa 1954 kwenye Mkutano Mkuu wa TAA wanaunda TANU yeye alipewa kazi ya kuandika na kusamabaza makaratasi ya kuhamasisha Waafrika kujiunga kwa wingi na TANU ili chama kikiundwa kiwe na wanachama wa kutosha.
Ally Sykes alikuwa na mashine ya kudurufu nyumbani kwake Mtaa wa Kipata.
Mkabala wa nyumba hii alikuwa anaishi baba yangu Said Salum.
Katika baraza hiyo ya nyumba aiyokuwa anaishi baba yangu alikuwa Mzee Kitwana akishona nguo na cherehani yake ya Singer.
Wazee wangu hawa wameona haya yote kwa macho yao mawili.
Ally Sykes akawa sasa anachapa makaratasi haya ya mwito kwa Waafrika kujiunga na TAA kisha anawapa vijana maalum waliokuwa wanafanyakazi katika treni za Reli ya Kati na wao wakawa kwa siri kubwa wanazisambaza kila stesheni kuanzia Morogoro, Dodoma, Tabora hadi Mwanza na Kigoma.
Special Branch wakawa na taarifa kuwa kuna makaratasi ya uchochezi yanasambazwa kwa Waafrika.
Ikawa sasa kuna msako mkubwa wa kutafuta mashine hii na mchapaji wa makaratasi hayo ya uchochezi.
Haukupita muda Special Branch wakajua kuwa mashine ya makaratasi ya uchochezi iko Mtaa wa Kipata nyumbani kwa Ally Sykes na yeye ndiye mchapaji wake.
Ndani ya TAA bila uongozi kufahamu walikuwa na makachero wawili waliokuwa wanapeleka taarifa zote za TAA serikalini - Alexander Thobias na Ali Mwinyi Tambwe.
Kipindi hiki President wa TAA alikuwa Julius Nyerere na Vice President Abdulwahid Sykes, Joseph Kasella Bantu akiwa Secretary General.
Amri Kweyamba akaweka mtego wa kumnasa Ally Sykes.
Mtego ukafyatuka siku moja mchana.
Ndugu yangu MTV,
Hebu niambie unaamini kuwa Ally Sykes alikuwa mchochezi?
Vipi kuhusu Julius Nyerere, Abdul Sykes na Kasella Bantu na wao pia kama viongozi wa TAA tuwaite pia wachochezi?
Mimi natokana na wazee wangu waliounda TANU na naijua vizuri historia ya kupigania haki na madhila yake.
Sishangai kuniona sina busara na "mchochezi."
Kisa ni kuwa natafuta haki na usawa.
Haya yaliwakuta wazee wangu waliopigania uhuru wa Tanganyika kutafuta hayo.
Picha hiyo hapo chini Ally Sykes na mimi ofisini kwake Mtaa wa Makunganya miaka mingi nyuma.