Ninachowasifu mimi ni jinsi walivyoshughulikia hayo matatizo yaliyojitokeza bila kuburuzwa na serikali, na pia jinsi wanaodhulumiwa walivyofanya jitihada ya kujaribu kuzuia fujo (ingawa bado zimetokea, nahisi zingekuwa zaidi kama wasingejitahidi). Kwamba kulikuwa na jitihada za wazi za kuiba kura, na hapohapo jitihada za wazi za kupambana na hali hiyo, wanastahili sifa. Maana wangenyamaza tu halafu mwishowe wakasema wameibiwa, tungekuja na msemo wa kiswahili wa "mbaazi kukosa maua na kusingizia jua". Lakini wamepambana kiume, ndio perseverence ninayozungumzia. Tume ya Uchaguzi imewasikiliza wadau na kuridhia hesabu ipitiwe upya usiku huu, hapo ndipo nilipowasifu kwa kuweka maslahi ya taifa mbele, maana tume hiyohiyo inayo madaraka ya kutangaza matokeo iliyoyapata, lakini wametumia busara na kuamua kuachana na ubabe (kama ule ambao huwa unatokea Zanzibar).
Na zaidi ya hayo yaliyotokea katika siku hizi mbili za mwishoni, maandalizi ya uchaguzi huu tokea awali yalikuwa mazuri. Na hata mbinu chafu zilipojaribiwa, wamechukua hatua za kuzishughulikia badala tu ya kutangaza matokeo kibabe. Ndio msingi wa sifa nilizowamiminia wadau wa uchaguzi wa Kenya.