Naam ni aibu iliyoje kwa wasomi wa UDSM au vyama vya upinzani kutoandamana na kukemea ukiukwaji wa demokrasia na mauji ya wananchi wasio kuwa na hatia nchini Kenya.Tuko katika zama za uwazi na ukweli na hivyo vyama vya upinzani na wasomi ni lazima wawe mstari wa mbele kukemea,kufichua,kupinga na kuwakomboa wananchi ambao wengi wao hawana mtu wa kuwasaidia.
Hivyo basi mimi nawaunga mkono wasomi hao wa UDSM kutumia ujuzi wao wa kisheria,hekima na maono yao katika kukemea ufisadi,uvunjaji wa haki za binadamu,mauaji ya raia wasio na hatia, na ukiukwaji wa demokrasia nchini Kenya kwa kufanya maandamano yao Jumamosi ijayo.
Ni lazima waelewe kuwa serikali ya CCM haipendi uozo huo ufunuliwe na ndiyo maana imekaa kimya kama bakuli la maji! pia cha kushangaza kuna watu hadi hapa JF ambao kwa sababu wanazozijua nao wamechukua msimamo huo huo wa serikali ya CCM kushabikia na kuwanyima haki watanzania kufanya maaandamano ya amani kupinga umwagaji damu na maonezi wanayofanyiwa watu wa Kenya.Ni lazima tuelewe kuwa maisha ni haki ya kila mtu na hakuna mtu au chama au kabila linaloweza kunyima mtu kuishi.Hivyo basi tumeona mauaji yametokea nchini Kenya na hakuna hata sehemu moja inayosema kuwa wapinzani wa Kenya ndiyo waliwauwa wananchi hao.Hivyo suala la kuandamana kwa watanzania wakiwemo wasomi wa UDSM ni suala la muhimu katika kuonyesha msimamo wao katika kutetea haki za wanyonge popote pale duniani ikiwemo Kenya.
Hivyo wale wote ambao wamechukua ile propaganda ya serikali ya CCM na polisi wake ya kuwa maandamano ya amani ni ya kumpa support Raila na hivyo kupendelea upande mmoja wasutwe kwa sauti ya juu na fikra zao wenyewe kwa kuwa wameshindwa si tu kukemea maovu na udhalimu bali wanahalalisha mambo haya kutokea tena katika sehemu nyingine Afrika.
Afrika kama bara tumechoshwa na michezo hii ya ubabe ubabe.Waasisi wetu walisimama kidete kupigania haki,usawa na kukemea maovu ambayo watu wetu walikuwa wanafanyiwa na wakoloni, leo hii kuna baadhi miongoni mwetu wanajikweza na kujifanya wao ndiyo wakoloni wa kipindi cha sasa huku wakitumia nguvu za dola na mahakama kukandamiza na kuuwa wananchi wanyonge! na chakushangaza ni pale wale wanaoamua kukemea mambo hayo kwa kufanya maandamano wanaponyimwa haki hiyo na baadhi yetu tunashabikia uamuzi huo wakiwemo wachache hapa JF.Hii siyo sawa na si haki na kama mambo haya yakiendelea basi inabidi tufikirie njia mbadala kama aliyotumia samora machelli na vikundi vingine vya ukombozi katika kutafuta haki.
Na kwa kuanzia hapa hapa JF tuwapinge kwa sauti zote wale wanaondeleza propaganda za CCM na serikali yake katika kuwanyima wananchi haki zao za msingi.
-Wembe
Wapinzani wazimwa Dar
na Happiness Katabazi
JESHI la Polisi jana lilifanikiwa kuzima maandamano yaliyokuwa yawashirikishe wafuasi wa vyama vinne vya upinzani vyenye ushirikiano wa kuunga mkono madai ya kambi ya upinzani nchini Kenya ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Desemba 27.
Tangu saa 12 asubuhi, wakiwa na silaha nzito pamoja na mabomu, polisi walianza kutanda katika vitongoji vya Manzese, Urafiki na eneo la Mahakama ya Ndizi, maeneo ambayo wapinzani walipanga kupita katika maandamano yao.
Wakati polisi wakiwa wametanda katika maeneo hayo, wanachana na wafuasi wa vyama hivyo walianza kuwasili katika maeneo hayo majira ya saa mbili, lakini walipowaona askari walijificha katika nyumba za wakazi wa eneo hilo wakisubiri amri kutoka kwa viongozi wao.
Ilipofika majira saa nne, mmoja wa viongozi wa upinzani aliyesisitiza kuwapo kwa maandamano hayo, Chacha Wangwe alianza kuwasiliana na waandishi wa habari kupitia simu yake ya kiganjani akieleza kuwa yeye pamoja na wafuasi wa upinzani wapatao 100, wako mafichoni eneo hilo, wakipanga mikakati ya kukabiliana na polisi waliokuwa wametanda eneo hilo.
Wangwe alikataa kutaja eneo alilokuwa amejificha pamoja na wafuasi wake kwa kile alichodai kuwa sababu za kiusalama, lakini alisisitiza kuwa wanajiandaa kuvamia eneo hilo ghafla kama mvua.
Baadaye Wangwe aliwasiliana tena na waandishi na kuwaeleza kuwa kutokana na udhibiti wa polisi katika eneo hilo, wamebadilisha sehemu ya kuanzia maandamano hayo na kuwataka waandishi wakashuhudie wanavyoibuka wakitokea eneo la Tandale Uzuri Darajani.
Waandishi waliwahi katika eneo hilo lakini hadi saa saba mchana, waandamanaji hao hawakuwa wamejitokeza katika eneo hilo huku polisi wakiendelea na doria kali.
Wangwe aliwasiliana tena na waandishi wa habari na kuwataka waondoke eneo hilo kwa sababu nalo halikuwa salama, warudi Manzese. Muda mfupi baadaye alipiga tena simu na kueleza kuwa amepata wazo jipya na kuwataka waende eneo la Mkwajuni, Masai Pub ambako alisema angelipua bomu.
Baada ya waandishi wa habari kufika eneo hilo walipokewa na mtu ambaye hawakumfahamu mara moja, aliyewaelekeza waende karibu na msikiti uliokuwa eneo hilo ambako walizungushwa hadi nyumba ambayo haikufahamika pia mmiliki wake ni nani, wakakalishwa chini ya mti.
Wangwe aliungana na waandishi hao dakika chache baadaye na kukiri kuwa wapinzani wameshindwa kuandamana kutokana na nguvu kubwa iliyotumiwa na serikali kuzuia maandamano yao.
Alidai kuwa licha na maandamano hayo kutofanyika, serikali inapaswa itambue kuwa wapinzani wanajua kuwa Serikali ya Tanzania ilishiriki kuiba kura katika uchaguzi wa Kenya uliofanyika hivi karibuni.
Huku akiongea kwa wasiwasi, Wangwe alidai anao ushahidi kuwa Serikali ya Tanzania ilishiriki katika hujuma zilizofanyika kwenye uchaguzi mkuu wa Kenya, kutokana na ziara ya bingwa wa propaganda wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale- Mwiru, nchini Kenya wakati wa uchaguzi huo.
Serikali yetu kupitia Kingunge imeshiriki kuiba kura za Wakenya na ndiyo maana hadi sasa haijatoa tamko la kulaani yanayotokea kwa jirani zetu, kwani nayo ni miongoni mwa walioshiriki kuharibu uchaguzi ule, na ndiyo maana leo (jana) wametumia nguvu kubwa ya dola kutuzuia sisi tusiandamane. alisema Wakati akiendelea kueleza hayo, askari wawili wa upelelezi walipita eneo hilo na mara Wangwe alipowaona alinyamaza ghafla na kuwataka waandishi wakutane naye Masai Pub, hatua chache kutoka alipokuwa akizungumzia.
Baada ya kuyasema hayo aliondoka haraka eneo hilo akitumia gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T 865 AMR, na haikueleweka alielekea wapi baada ya waandishi kumkosa Masai Pub.
Baadaye ilielezwa kuwa Wangwe alikuwa amekimbilia makao makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) huko Kinondoni na waandishi walipofika eneo hilo walimkuta na alieleza kuwa alikuwa akiwasubiri waandamanaji waliokuwa na mabango ili maandamano yaanzie hapo.
Dakika chache baadaye aliwaita waandishi wa habari ndani ya ofisi za CHADEMA na kuwaambia kuwa maandamano hayo yamesitishwa lakini yatafanyika siku nyingine kwa nchi nzima, hata hivyo hakutaja siku ya kufanyika maandamano hayo.
Naye Mkuu wa Idara ya Habari wa CHADEMA, Erasto Tumbo, alitaka Kenya itolewe kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki iwapo Rais Kibaki hatajiuzulu, kwa vile ameingia madarakani kwa wizi wa kura.
Kwa ujumla mwenendo mzima wa pilika pilika hizo za jana ambazo zilikuwa kama sinema, zilivuta hisia za watu wengi huku baadhi ya wafanyabiashara wa eneo la Manzese wakiogopa kufanya shughuli zao.
Polisi waliokuwa wakiwafuata waandishi hatua kwa hatua, walisikika wakieleza kuwa iwapo kuna mpinzani atakayeonekana anaandamana barabarani, basi kila hatua yake moja itafuatia rungu la polisi moja.
Baadhi ya wafuasi wa upinzani nao walidai kuwa walichokuwa wakikifanya jana ni kulitikisa na kulihangaisha Jeshi la Polisi ili liendelee kufanya doria siku nzima ya jana chini ya Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni, Damas Kasabi.
Nako katika ofisi za Ubalozi wa Kenya zilizo Mtaa wa Mafinga, Kinondoni na katika baadhi ya mitaa ya Jiji la Dar es Salaam, hali ya ulinzi iliimarishwa, huku magari ya polisi ya kurusha maji kwa ajili ya kuwatawanya waandamanaji yakiwa yameegeshwa Kituo cha Polisi Magomeni na Urafiki, yakiwa tayari kuwakabili waandamanaji.
Maandamano hayo yalipigwa marufuku juzi na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Alfred Tibaigana, kwa maelezo kuwa hali ya usalama hapa nchini kwa sasa si shwari.