BoT yajivua lawama ukomo ajira ya Ballali (Majira)
Na Reuben Kagaruki
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imejisafisha na kusema kuwa haijui ni lini aliyekuwa Gavana wa BoT, Dkt. Daud Ballali, aliandikiwa barua ya kufutwa kazi na kuipokea kwa sababu haihusiki na jambo hilo.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Ikulu kusema kuwa wenye taarifa za lini Dkt. Ballali aliandikiwa barua ya kufutwa kazi na aliipokea lini ni BoT.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndullu, alisema nafasi ya ugavana ni ya kuteuliwa na Rais, hivyo na uamuzi wa kufutwa kazi unatoka huko huko kwake.
"Hii ni nafasi ya kuteuliwa, unajua vyeo vya kuteuliwa unaitwa tu na kuambiwa," alisema Profesa Ndullu na kusisitiza kuwa katika nafasi ya Ugavana Ikulu ndio mwajiri na sio BoT.
Kauli hiyo ya Profesa Ndullu inaonekana kuwachanganya wananchi hasa kutokana na kauli iliyotolewa na Ikulu juzi kuwa BoT ndio wanaojua Dkt. Ballali aliandikiwa lini barua ya kufutwa kazi na aliipokea lini.
Juzi akijibu moja ya maswali ya waandishi wa habari Dar es Salaam lililomtaka aeleze ni lini Dkt. Ballali aliandikiwa barua ya kufutwa kazi na aliipokea lini, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu, Bw. Salva Rweyemamu,alisema wenye jibu hilo ni BoT, lakini katika hali ya kushangaza Benki hiyo nayo imeruka kiunzi hicho ikisema hilo ni suala la Ikulu.
Utata huo unazidi kuibuka huku wananchi wakisema kuwa Dkt. Ballali hajawahi kufukuzwa kazi na kifo chake kimetokea akiwa bado mtumishi wa serikali hivyo iliwajibika kusimamia mazishi yake.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Bw. Augustino Mrema, alikaririwa na gazeti hili hili akisema Dkt. Ballali hajawahi kufukuzwa kazi. Alisema kama aliwahi kufukuzwa kazi basi ioneshe kitabu alichosaini kudhibitisha kupokea barua ya kufukuzwa kazi na Rais ili Watanzania wajiridhishe.
Kama hiyo haitoshi, baada ya kutangaza kumfuta kazi gavana huyo wa zamani, serikali haikujishughulisha kumtafuta na mara zote imekuwa ikisema kwamba haina haja ya kujua hospitali aliyolazwa kwa kuwa ilikuwa bado haijamhitaji.
Profesa Ndullu alipoulizwa leo kama Dkt. Ballali aliweza kukabidhi ofisi wakati anaondoka kwenda kutibiwa, alisema wakati anaenda kutibiwa kuna watu waliokuwa chini yake walioachiwa majukumu.
"Taasisi nyeti kama hii inaendeshwa kwa kumbukumbu, kuna Bodi ya Uendeshaji na kiongozi mmoja peke yake hawezi kuwa mwendeshaji," alisisitiza Profesa Ndullu.
Profesa Ndullu alisema alipoteuliwa kushika nafasi hiyo Septemba mwaka jana na kuanzia kipindi hicho alikuwa na mawasiliano naye mara kwa mara na alikuwa akimpa maelekezo hata pale afya yake ilipozidi kudorora.
My Take:
What on earth is this, King Majuto drama? Yaani muda wote serikali inasema haijui aliko kumbe Ndullu alikuwa na mawasiliano naye ya "mara kwa mara"?