MAHAKAMA Kuu Kanda ya Kigoma, imewaachia huru washtakiwa 11 waliokuwa wakikabiliwa na kosa la kuua kwa kukusudia askari wawili wa Jeshi la Polisi na kukata sehemu za siri za mmoja wa askari hao katika mapigano yaliyotokea wakati wa kuwaondoa wananchi waliovamia eneo la Hifadhi ya Ranchi za Taifa (NARCO), wilayani Uvinza.
Hukumu hiyo ilisomwa Ijumaa (Agosti 14), na kesi hiyo ilihusu tukio lililotokea Oktoba, mwaka 2018, wakati wananchi karibu 1,000 walipojiunga kupambana na askari wakiwa na silaha za jadi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Ilvi Mgeta, alisema sababu za kuwaachia huru ni ushahidi alioutoa daktari wa Kituo cha Afya cha Lugufu, aliye wahudumia baadhi ya washtakiwa na kueleza kuwa risasi walizopigwa zilipita juu ya ngozi wakati washtakiwa wana makovu makubwa yanayoonyesha risasi zilipita upande mmoja na kutokea mwingine tofauti na shahidi ulivyoeleza.
“Tunashindwa kuelewa kwa nini shahidi huyu alitoa ushahidi wenye nia ya kuidanganya mahakama wakati akiwa anajua ukweli ni ushahidi wa askari walioeleza kuwapo katika mapigano hayo.”
Ushahidi mwingine ulioelezwa kuwa dhaifu ni wa askari walioeleza kushiriki operesheni hiyo kuwa walipambana na wananchi hao uso kwa uso na kufanikiwa kuwapiga risasi wakati wa mapigano, wakati makovu ya risasi hizo kwa watu 10 kati ya 11 walioshtakiwa, yakionyesha kuwa walipigwa upande wa nyuma na kutokea mbele hivyo wapigaji wa risasi hizo hawakuweza kuwaona uso kwa uso washtakiwa.
Pia, Jaji alisema gwaride la utambuzi halikufuata misingi ya sheria kwa kuwa mmoja wa washtakiwa alieleza kuwekwa kwenye mstari akiwa peku na wengine wakiwa na nguo zilizo jaa damu kutokana na majeraha ya risasi, hivyo kurahisisha kutajwa kuwa walihusika na mauaji hayo.
Kadhalika, alisema ushahidi wa aliyeshuhudia gwaride la utambuzi kuiambia mahakama kuwa hakuwaona washtakiwa hao katika gwaride la utambuzi pamoja na maelezo ya onyo yaliyoelezwa kuandikwa na washtakiwa, ambayo wote waliyakana mahakamani kuwa sio yao pamoja na kukamatwa eneo tofauti na tukio lilipotokea katika maeneo tofauti.
Baada ya Jaji Mgeta kupitia uchambuzi wa hoja za pande zote mbili za upande wa Jamhuri uliowakilishwa na Happyness Mayunga, Shaban Masanja na Riziki Matitu na upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Sadick Aliki, Kagashe Rweyumamu na Eliuta Kiviylo, alisema kwa kuzingatia uhalisia wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo kuonyesha kuwa na taarifa zinazopingana, ushahidi huo ni dhaifu na hauwezi kuwatia hatiani washtakiwa hao na mahakama hiyo imeamua kuwaachia huru washtakiwa wote 11.
Askari waliopoteza maisha kwenye tukio hilo ni Inspekta Ramadhani Mdimu na Koplo Mohamed Nzengohuku. Washtakiwa 11 waliochiwa huru ni Gelya Gisega, Jumanne Jackson, Nkono Mwandu, Shishi George, Masanja John, Hamis Masalu, Walwa Malongo, Makenzi Lukelesha, Masalu Inambali, Petro Bucheyeki na Charles Maduhu.
NIPASHE