Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema Serikali ikikosa ushauri mzuri ama ikipuuza nchi inaweza kwenda pasipotakiwa kwenda.
Kikwete ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Novemba 22, 2023 alipokuwa akielezea umuhimu wa makongamano na mikutano katika kuishauri Serikali na Rais.
“Ukikosa ushauri mzuri ama ukipata ushauri mzuri ukaupuuza hii nchi itakwenda kusikotakiwa kwenda. Ndio maana makongamano haya ni muhimu sana unachota mawazo,” amesema
Kikwete aliyekuwa Rais wa nne wa Tanzania (2005-2015), amesema hayo kwenye mkutano wa nne wa Maendeleo ya Biashara na Uchumi ulioandaliwa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ambao yeye alikuwa mgeni rasmi.
Amesema unapokuwa Rais hujui kila kitu lakini unatakiwa kushughulika na kila jambo na kwa sababu huwezi kujua kila kitu inakubidi kutegemea ushauri.
“Sasa wenzako wanakuchagua kuwa unafaa kuwa rais, lakini utakuwa hujui kila kitu, taaluma yako ni uchumi…lakini ukiwa Serikali na Rais hujui kila kitu. Kwa sababu huwezi kujua kila jambo, lazima utegemee sana ushauri,” amesema