Wakuu heshima kwenu kwa michango hapa nami nachangia kuhusu Aina za nyanya tu kidogo kadri ninavyozifahamu ili kuongezea akiba ya taarifa.
Money maker: Hii ni aina ya siku nyingi sana ni nyaya za kusimikia mti unabakiza shina moja au mawili mara nyingi zikifikia mikungu 5 au 6 unatakiwa ukate juu. Zinatabia ya kupasuka matunda zikipata maji mengi hasa wakati wa mvua shauri ya ganda laini, hazikai muda mrefu na hazistahimili misukosuko ya safari ndefu!
Roma: Ni nyaya zinazaa sana na ni aina ya mbegu ya enzi na enzi, zinangozi laini, hivyo hazikai muda mrefu mezani kwa mfanyabiashara na zinapondeka kirahisi zinaposafirishwa mbali. Roma ni nyanya tamu sana kwa kachumbari na zina mchuzi mzito lakini zinatabia ya kukauka kitako chake kirahisi sana zinapokabiriwa na ukame au udongo wenye chumvi.
Marglobe: Hii inahitaji kusimamishiwa kwa kufunga kwenye kijiti na mara nyingi hupunguziwa na kuachwa shina moja tu, matunda yake ni makubwa sana na machache nayo inangozi laini haistaimili misukosuko ya kusafirisha.
Tengeru (97?): Hii ni aina ya mbegu zilizozalishwa na watafiti wa kitanzania, inahitaji kusimamishiwa kwa kufunga kwenye kijiti na mara nyingi hupunguziwa na kuachwa shina moja, matunda yake ni makubwa sana na machache hii aina nyanya zake zinaganda gumu hustahimili kusafirishwa na huvumilia magonjwa ya mnyauko, mavuno yake makubwa.
Tanya: Hii ni aina ya mbegu zilizozalishwa na watafiti wa kitanzania, nikifupi cha Tanzania Nyanya. Aina hii haipunguziwi matawi. Ni nyanya nzuri sana zinazokidhi matakwa ya soko inaweza kusafirishwa mbali na inakaa muda mrefu mezani iwapo sokoni. Umbo lake ni matunda marefurefu mfano wa yai isipokuwa ncha zake ni bapa kidogo si mchongoko kama yai.
Ukibahatika kupata mbegu Original ya aina hii utaifurahia kwani matunda yake ni mengi, makubwa na yanavutia sana umbo lake! Angalizo ni kwamba makampuni mengi yanauza mbegu ya Tanya iliyochanganyika kiasi kwamba imefanya wakulima wengi kuichukia mbegu hii! Nimewahi kuilima ilipofikia mavuno nilichoona sikuamini! Ilikuwa ni mchangayiko wa Roma, Marglobe, vigorori na mtepeto, yaani wateja wangu walinikimbia! Ni mbegu nilizonunua kwenye makopo yaliyopakiwa na East African Seed Company, ndugu zangu muwe makini, makampuni ya kibongo yakiishiwa mbegu hukusanya nyanya kwa wakulima na kuzikamua tu! Kuweni macho ikibidi tunzeni mbegu zenu. Mbegu za makampuni ya Kikwetu ninaziogopa sana, utapeli ni mwingi tu na wenye pesa wako above the law!
Cal J: Aina hii haihitaji kupunguziwa matawi, inazaa sana. Ina ngozi ngumu na kwa kweli hustahimili hekaheka za usafirishaji yaani ni mawe, wengine huziita dumudumu, kuna wakati matunda pia hupasuka mvua ikizidi. Hii ni aina maarufu maeneo maarufu ya kilimo cha nyanya.
Rio Grande: Hii ni aina mpya ambayo imekuja kuuwa umaarufu wa Tanya huachwa kutambaa haihitaji kupunguziwa matawi. Aina hii ni aina ya kisasa zaidi inayojibu mahitaji ya soko kwa kuweza kustahimili kusafirishwa masafa na kukaa muda mrefu mezani sokoni (shelf life). Hii ni aina nzuri sana ya nyanya zenye umbo la yai, aina hii humwaga maua na matunda bila kelele, hutoa majani kiasi na inapokunya matunda shambani utaona shambani yanaonekana matunda tupu! Kama ningelima leo ningechangua mbegu hii.
Ornyx: Hii ni aina mpya ambayo imekuja kuuwa umaarufu wa Tanya. Aina hii haihitaji kupunguziwa matawi. Aina hii ni aina ya kisasa zaidi inayojibu mahitaji ya soko kwa kuweza kustahimili kusafirishwa masafa na kukaa muda mrefu mezani sokoni (shelf life).
Aina hii ina matunda makubwa na mengi kuliko Tanya. Matunda yake umbo ni mfano wa yai. Inafanana sana kama Rio Grande, ingawa haifikii uzazi wa Rio Grande. Kwa uzoefu wangu shambani Rio Grande iko juu zaidi ya Orynx.
Nimewahi kuona mbegu za Mkulima Seed Company kopo limewekewa label iliyosomeka 'Rio Grande (Orynx)' ! Inashangaza sana kwa vile hizo ni aina 2 tofauti! Nadhani ni kumpa picha mkulima aliezoea aina mojawapo aone ni ile ile! Yaani aliyezoea Oryx anunue na aliyezoea Rio Grande anunue, lakini huo ni wizi, ni utapeli hizo ni aina tofauti kabisa za nyanya japo zinafanana muonekano wa matunda yake!
Anna F1: Hii ni aina chotara, shina tawi moja au mawili husimamishwa kwa miti, hurefuka urefu zaidi ya mita tano, shina moja huzaa kuanzia kilo 25, ni aina maalum kwa green house ingawa huzalishwa pia nje, unavuna miezi zaidi ya 6, mbegu zake ni ghari sana. (Msifikiri ni hadithi nyingine ya machungwa 4000 kwa mti nina Hand book yake ukipenda niPM nikugawie).
NB: Kusimamishia miti!
Wakati wa masika au umwagiliaji ni lazima kusimamishia miti aina yoyote ya nyanya maana zinapogusana na udongo wenye unyevunyevu huoza.
Unapochagua aina ya nyanya za kupanda angalia soko lako linapenda aina gani ya nyanya ingawa huwa zikiadimika nyanya ni nyanya tu hakunaga kuchagua!
Samahani mimi nami sijuagi kuandika maelezo mafupi msinichoke mwee enh jamani!!