Mkuu hizi nyanya za kiangazi nasikia zina changamoto zake hasa katika madawa,ila ukifanikiwa kuvuna ni kua umepiga bao!ngoja waje kina Malila na Kubota watatoa shule ya uhakika hapa!
Mkuu Nyamburi asante kutambua uwepo wangu, acha nianze kuchangia na wadau wengine wataendeleza nitakapoishia. Kuna thread moja ilianzishwa hapa kuna mdau alikwama kupata wanunuzi wa nyanya (Dakawa) Dumila Morogoro akaandika hapa kuomba msaada wa kuunganishiwa wanunuzi. Kuna mchango mwingi wa mawazo kule kwenye thread hiyo nadhani hapa ni suala linalojirudia.
NI hivi: 1) Nyanya za kiangazi hufanikishwa na kufaidiwa sana na wakulima wenye mitaji mikubwa ambao huwa wanalima kwa maeneo makubwa sana kuweza kujaza FUSO mwenyewe na kusafirisha masoko ya mbali. Ijapokuwa bei ni ndogo lakini kwa kuwa huwa wanamzigo mkubwa na gharama za uzalishaji ni ndogo sana huwa wanaingiza pesa kubwa sana. Kuna wakulima wengi sana aina hii ukifika msimu wa kilimo cha kiangazi huja kwa wingi sana mkoani Morogoro maeneo ya Dumila, Mbigiri na mabonde ya Kilosa na pia eneo la Doma kuelekea Mikumi. Wakulima hawa ni wenye mitaji mikubwa hasa toka Iringa na maeneo mengine, huja msimu wa kiangazi kulima nyanya hizi kwa wingi sana, na wao hata bei ikiwa ndogo husafirisha kupeleka masoko ya mbali ikiwamo Dar! Mkulima mdogo mdogo akilima msimu huu sana sana ndiyo huishia kuwauzia hao wenye uwezo wa kusafirisha na bei ambayo hupewa ni ya kutupa karibu na bure.
2) Kilimo cha nyanya za kiangazi ni kilimo kisichokuwa na changamoto ukilinganisha na nyanya za masika. Majira ya kiangazi kuna ubaridi na hewa kavu magonjwa hayashamiri sana na nyanya huzaa kwa uwezo mkubwa kuliko majira ya mvua. Nyanya huzaa mavuno makubwa sana kiangazi kuliko majira ya mvua ambako huwa kuna joto linalopukutisha maua na matunda.
3)Hata hivyo uzoefu wangu maeneo ya Morogoro kwa ujumla kwa mfano nyanya zisizokuwa na changamoto ni kuanzia mwishoni mwa mvua na kupitia kipindi chote cha baridi nyanya za mwisho zivunwe mwezi wa nane. Kuanzia mwezi wa tisa huwa kuna changamoto ya ukame ambapo umwagiliaji lazima uwe wa karibu karibu zaidi, pia hutokea wadudu ambao ni nuksi sana, wanaitwa red spider mites, ni kama utitiri mwekundu, hawa ni wabaya sana kuanzia majira ya joto kali yanapoanza. Hawa wadudu ndiyo hupausha majani na matunda yanapoiva kuwa kama rangi ya machungwa. Kuanzia mwezi wa kumi hadi kipindi chote cha joto kali mimea ya nyanya hupunguza sana uzaaji kwani maua huwa yanapukutika tu au hayarutubishwi kwa hiyo nyanya zinazozaliwa ni chache. Na pengine ni kipindi hiki nyanya huanza kuadimika na bei huanza kupanda juu.
Kwa hiyo nahitimisha kwa kusema kuwa kupindi cha kiangazi kina awamu mbili, awamu ya kiangazi baridi ambacho huishia mwezi wa nane na ndicho nyanya huzalishwa kwa wingi sana bila changamoto na awamu ya kiangazi joto kinachoanzia mwezi wa tisa hadi mvua zinapoanza, kipindi hiki ni cha wadudu nuksi, ukame mkali na uzaaji duni wa nyanya shauri ya joto kali linaloathiri uchavushaji na urutubishaji maua. Nawasilisha wakuu !!