Kama tunavyosema hapa, unaweza kushangazwa sana unapokutana na taasisi kubwa kama TUKI nayo inaboronga Kiswahili.
Wamekosea, hilo si neno sahihi.
Oxford nao wamekosea?
Hapana, wote hawajakosea. Wako sahihi.
Pia, zote, ‘onyesha’ na ‘onesha’ ni sahihi.
Kwa nini zote ni sahihi? Jibu ni lahaja.
Kiswahili kinazungumzwa Afrika Mashariki na Kati.
Hili ni eneo kubwa. Hivyo suala la lahaja za lugha haliepukiki.
Kimvita [Kiswahili cha Mombasa na pwani ya Kenya] kina tofauti za hapa na pale katika matamshi na tahajia za maneno na Kiswahili cha bara.
Mfano, ile mboga uijuayo wewe kama ‘biringanya’, kule Mvita na baadhi ya sehemu za Congo, inaitwa ‘biringani’.
Kuna baadhi ya maeneo namba 0 huitwa ‘sufuri’ na kwingineko huitwa ‘sifuri’.
Hata Kisukuma kina lahaja. Kinyantuzu, Kisukuma cha wenyeji wa Simiyu, kina utofauti na Kisukuma cha wenyeji wa Shinyanga
Mfano, kijiji cha ‘Gambosi’, watu wa nje huwa wanakiita ‘Gamboshi’.
Matamshi yote yanakubalika.
Hata Kiingereza kiko hivyo hivyo.
Mfano, neno ‘schedule’, kwa Marekani hutamkwa tofauti na litamkwavyo Uingereza na kwingineko kutumiako Kiingereza cha Uingereza.
Hata kwenye tahajia, kuna maneno huandikwa tofauti. ‘Center’ na ‘centre’ yote ni sahihi.
‘Defense’ na ‘defence’ yote ni sahihi pia.
Hivyo, ‘onyesha’ na ‘onesha’ nayo yote ni sahihi. Ni suala la lahaja tu.
Na ndo maana yote yapo kwenye kamusi zote za Kiswahili sanifu [ambazo ninazo na ambazo nimewahi kuziona].
Sikuwa na nia ya kujivika ualimu wa isimu matumizi. Ila, wakati mwingine inabidi tu iwe hivyo ili kutoa somo ambalo linaonekana kuwaepa watu wengi.
Kamusi hutungwa na wataalamu wa lugha waliofanya tafiti za kutosha. Sidhani kabisa kama wataalamu wote hao wa Kiswahili, kutoka Afrika Mashariki na Kati, wakakosea kuliweka neno ‘onyesha’ na kutoa fasili yake, katika hizo kamusi za Kiswahili.
Kwenye lugha, neno moja kuwa tofauti katika matamshi na tahajia, ni jambo la kawaida sana, kwa kuzingatia muktadha wa lahaja.