Mag 3,
Unaandika huku umejawa na ghadhabu.
Katika hali kama hiyo kwa kawaida akili hupoteza umakini.
Umenitukana kwa kuniita mpuuzi na sifa nyingine mbaya na kusema kuwa nipuuzwe.
Mimi si mpuuzi na ndiyo maana wewe umeshindwa kunipuuza umekuwa ukinisoma siku zote.
Mimi si mpuuzi na ndiyo maana unaona nimeweza kuandika vitabu kadhaa na vikachapwa na wachapaji wa sifa kama Oxford University Press.
Unaumizwa kwa jinsi kitabu cha Abdul Sykes kilivyobadili historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika.
Unasema ati Cecil Matola ndiye aliyeanzisha African Association nk. nk.
Lakini huna ushahidi wa hilo.
Nenda Maktaba ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, East Africana kasome Seminar Paper ya mwaka wa 1968 iliyoandikwa na Aisha "Daisy"Sykes, ''Kleist Sykes (1894 - 1949),'' mwanafunzi wa gwiji wa historia ya Tanganyika John Iliffe, inayotokana na mswada wa kitabu alioandika babu yake Kleist Sykes kabla hajafariki mwaka wa 1949.
Humo utapata historia yote ya uasisi wa African Association 1929, kwa majina ya waasisi wake: Cecil Matola (Rais), Kleist Sykes (Secretary), Mzee bin Sudi, Zibe Kidasi, Ibrahim Hamisi, Ali Said Mpima, Suleiman Majisu, Raikes Kusi na Rawson Watts.
Utapata pia historia ya kuasisiwa kwa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika Kleist Sykes 1933 Kleist akiwa Secretary na Mzee bin Sudi akiwa Rais.
Kleist anaeleza pia na utasoma humo kuwa kabla ya kuasisiwa kwa African Association, Waafrika walikuwa wakiwakilishwa na Mzungu Father Gibbons kutoka Pugu Mission na Wakristo wakionywa wasijiingize katika siasa.
Hii ndiyo sababu ya kuona waasisi wa African Association wengi wao ni Waislam.
Haya si maneno yangu bali ni maneno ya Kleist Sykes ndani ya mswada wake ambao sasa ni sura katika kitabu alichohariri John Iliffe (1973).
Isingewezekana kwa hali hii kwa Cecil Matola kuwa kinara wa harakati hili achilia mbali ile hali ya siasa ya Dar es Salaam ya miaka ile ambayo Wakristo walipangiwa hadi maeneo ya kuishi na wakoloni.
Cecil Matola akiishi Mission Quarters sehemu ambako kulikuwa na kanisa pekee Kariakoo.
TANU ilipokuja kuundwa mwaka wa 1954 hali haikubadilika Waislam walikuwa mstari wa mbele.
Umeandika na unasema kuwa mimi nawahalalisha Wazulu, Wanubi na Wamanyema waliongizwa Tanganyika na Wajerumani kama askari mamluki kuja kuwasaidia Wajerumani katika vita yao na wananchi wa Tanganyika waliokuwa wakipigana dhidi ya ukoloni chini ya viongozi wao Mtwa Mkwawa na Bushiri bin Salim Al Harith.
Haya ni matokeo ya ukoloni na mimi nimeeleza historia hii si kwa nia yoyote ya kutukuza dhulma.
Katika hawa mamluki walioingizwa Tanganyika mwishoni mwa miaka ya 1800 alikuwapo babu yangu mkuu, Abdallah Samitungo Muyukwa kutoka Belgian Congo.
Lakini watoto wa hawa askari mamluki ndiyo waliowasha cheche za ukombozi wa Tanganyika.
Historia ya Kleist Sykes na wanae hivi sasa si ngeni katika ukombozi wa Tanganyika.
Babu yangu Salum Abdallah ni mmoja katika wanachama wa TAA na ni muasisi wa TANU Tabora 1954 na mwaka wa 1955 aliasisi Tanganyika Railways African Union (TRAU) akiwa Rais na Kassanga Tumbo Secretary.
Mchango wa babu yangu katika vyama vya wafanyakazi wa Tanganyika ni mkubwa sana ingawa historia bado haijamtambua.
View attachment 1312692
Kushoto ni Salum Abdallah Rais wa TRAU akivishwa mgolole kama ishara ya kiongozi wa mapamabano na wa mwanzo kulia Christopher Kassanga Tumbo Katibu wa TRAU
Salum Abdallah aliongoza migomo mitatu ya wafanyakazi wa reli na migomo hii ikaenea nchi nzima dhidi ya wakoloni 1947, 1949 na 1960, mgomo wa mwaka wa 1960 ukidumu kwa siku 82 rekodi ambayo bado haijavunjwa inawezekana Afrika nzima kwani mgomo mkubwa na mrefu ulikuwa siku 62 ulioongozwa na Makhan Singh, Kenya.
Nina mswada wa Dr. Vedasto Kyaruzi katika Maktaba yangu, ''The Muhaya Doctor.''
Hakuna popote amasema kuwa yeye aliasisi TAA.
TAA hakikuwa chama kipya bali ni ile ilie African Association ilibadilishwa jina mwaka wa 1948 ili kuitofautisha na African Association ya Zanzibar.
Ungependa na kwa hakika nafsi yako na wengi wanatamani kama labda Dr. Kyaruzi angeanzisha TAA kama chama kipya na Nyerere akawa muasisi pekee wa TANU lakini majaaliwa hayakuwa hivi.
Ushahidi wa historia hii unasema vinginevyo.
Historia ya vyama hivi viwili nimeiandika kutokana na Nyaraka za Sykes na sasa imetiwa katika Dictionary of African Biography (DAB) mimi nikiwa mwandishi.
Ikiwa wewe hukubaliani na historia hii itabidi uje na ushahidi kuthibitisha hayo unayoyatamani yawe.
Kunishambulia mimi kama mtu binafsi badala ya kuleta ushahidi wa hiyo historia unayotamani iwe hakutobadilisha ukweli wa historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika.
Sent using
Jamii Forums mobile app