UKAMATAJI WA KILO 34.89 ZA HEROIN NA BISKUTI ZILIZOTENGENEZWA KWA
KUTUMIA BANGI
Dar es Salaam, 15 Novemba, 2022
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na
Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, katika kipindi cha mwezi Oktoba na mwanzoni
mwa mwezi Novemba 2022, imefanikiwa kukamata jumla ya kilo 34.89 za dawa za
kulevya aina ya heroin pamoja na biskuti 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa ya
kulevya aina ya bangi kama moja ya malighafi kutokana na operesheni endelevu
zinazofanywa na Mamlaka katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika Operesheni hizo, jumla ya watuhumiwa 11 walikamatwa kati yao watuhumiwa tisa
(09) wanashikiliwa kwa kukutwa na jumla ya kilo 34.89 za heroin. Watuhumiwa hao ni Kambi Zuberi Seifi (40), mkazi wa Oysterbay Jijini Dar es Salaam ambaye ni mfanyabiashara na mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sports Academy kilichopo
Tuangoma - Kigamboni kinachojihusisha na ukuzaji wa vipaji kimichezo na pia ni mmiliki
wa kampuni ya Safia Group of Companies.
Mtuhumiwa wa pili ni Muharami Said Mohamed Sultan (40) mkazi wa Kigamboni ambaye ni kocha wa walinda mlango (goal
keepers) wa timu ya Simba Sports Club.
Watuhumiwa wengine ni Said Abeid Matwiko (41) Fundi Seremala, mkazi wa Magole
‘‘A’’ Kivule; Maulid Mohamed Mzungu almaarufu Mbonde (54) mkulima na mkazi wa Kamegele – Kisemvule; John Andrew John almaarufu Chipanda (40) mfanyabiashara na mkazi wa Magore Kitunda; Rajabu Mohamed Dhahabu (32), mfanyabiashara na mkazi
wa Tabata Segerea; Seleman Matola Said (24) Mkulima na mkazi wa Wailes Temeke;
Hussein Mohamed Pazi (41) mfanyabiashara na mkazi wa Kibugumo Kigamboni;
Ramadhan Rashid Chalamila (27) mfanyabiashara na mkazi wa Mzinga Kongowe.
Watuhumiwa wote tisa watafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria
Aidha, Mamlaka ilimkamata mtuhumiwa Abdulnasir Haruon Kombo (30) mfanyabiashara,
mkazi wa Kaloleni jijini Arusha akiwa na biskuti 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa ya kulevya aina ya bangi akiwa anaziuza katika eneo la Kaloleni jijini Arusha.
Vilevile, Mamlaka ilimkamata Hassan Ismail (25) mkazi wa Olasiti jijini humo anayesadikiwa
kuwa ndiye mtengenezaji wa biskuti hizo zenye dawa za kulevya akiwa pia na dawa za
kulevya aina ya bangi.
Watumiwa hawa wameshafikishwa mahakamani jijini Arusha. Matukio ya uwepo wa bidhaa za vyakula vinavyotengezwa kwa kutumia bangi yameanza kushamiri hapa nchini. Itakumbukwa kuwa, mwaka 2020 na 2021 Mamlaka ilikamata bangi iliyosindikwa mfano wa jam, keki na asali katika matukio tofauti tofauti wakati wa utekelezaji wa operesheni zake.
Hali hii inaonesha kuwa, tatizo hili linaendelea kuongezeka nchini na hasa ikizingatiwa wafanyabiashara hawa wenye nia ovu hutumia vyakula vinavyopendwa na watoto mfano pipi, keki, ice cream na biskuti hivyo,kuwepo na uwezakano wa kuwaingiza watoto kwenye matumizi ya dawa za kulevya bila kujua na
hatimaye kuwa waraibu.
Hivyo basi, wazazi na walezi wanapaswa kufuatilia kwa karibu nyendo za watoto wao.
Mamlaka inawakumbusha wananchi kuwa, kujihusisha kwa namna yoyote ile na dawa
za kulevya ni kosa kisheria.
Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya
{Sura ya 95} inatoa adhabu kali hadi kifungo cha maisha kwa atayethibitika kujihusisha
na kosa hilo.
Hivyo basi, wananchi wanapaswa kushiriki kwa dhati katika kukabiliana na tatizo la matumizi na biashara ya dawa za kulevya kwa kuwafichua wale wote wanaojihusisha na biashara hiyo.
Imetolewa na,
Florence Khambi
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya
Source :
DCEA | Home