Nataka kumtetea Zitto kidogo. Naamini kwamba hatumiwi na CCM bila kujua. Kwangu mimi, Zitto ameshavuka viwango vya kutumiwa bila kujua. Zitto ni mjanja vya kutosha, kiasi kwamba akiamua kutumika, atafanya hivyo kwa hiari yake.
Kama wanakerwa na vikao vya siri anavyofanya na vigogo kadhaa wa CCM, waseme; na watutajie majina. Kama ni Joseph Sinde Warioba au Dk. Ahmed Salim au Rostam Azizi au Edward Lowassa au Rais Jakaya Kikwete au Lawrence Masha au William Ngeleja; waseme wazi.
Maana kinachozungumzwa sasa ni kwamba mojawapo ya ajenda za Zitto kuutaka uenyekiti ni ahadi aliyopewa na baadhi ya vigogo wa CCM kwamba wanatamani kujiengua na kujiunga na CHADEMA iwapo tu, ataweza kumwangusha Freeman Mbowe katika nafasi ya uenyekiti.
Uongo wanaotumia ni kwamba wakishajimega kutoka CCM wataiwezesha CHADEMA kupata wabunge wengi mwaka 2010, na hata kuipa uwezekano wa kuwa na waziri mkuu kutoka chama cha upinzani.
Lakini hapa kuna mambo mawili. Zitto anajua kuwa mwaka 2005, chama chake kilikuwa na mpango kama huo wa kuwashawishi watu maarufu kutoka CCM wajiunge na CHADEMA kwa malengo hayo hayo.
Na mmoja wa watu waliokuwa wanawindwa katika hatua za awali kabisa ni Jakaya Kikwete na kundi lake, wakati wanamtandao wakiwa hawana uhakika wa mtu wao kupitishwa katika vikao vya CCM kutokana na tuhuma walizojua zinamwandama mtu wao, lakini pia kutokana na hujuma za kisiasa kutoka kwa vigogo kama Philip Mangula, Benjamin Mkapa, John Malecela, Frederick Sumaye na wengine ambao walikuwa wameshikilia chama na serikali; huku pia ukiwapo woga na hofu juu ya Dk. Salim Ahmed Salim.
Wanamtandao walikuwa tayari kuhama kama wangekataliwa CCM, na chama walichotaka kukimbilia ni CHADEMA.
Zitto mwenyewe anakumbuka jitihada zake za kuwanasa wanasiasa wa aina ya Zakia Meghji zilivyoshindikana, hasa baada ya yeye mwenyewe kutoboa siri hiyo kwa vyombo vya habari.
Na kikubwa zaidi, waliweza kutumia vema mbinu zao chafu, wakapenya katika kinyanganyiro na kumpitisha mtu wao. Wakaanza mkakati na wakala yamini kumshughulikia Mbowe kisiasa na kibiashara, wakijua kuwa nguvu yake inategemewa sana kuikuza CHADEMA, na kwamba wakifanikiwa kumdhoofisha Mbowe, CHADEMA itadhoofika pia na kuwapisha kirahisi mwaka 2010.
Zitto amekuwa mmoja wa mashujaa katika vita dhidi ya ufisadi, lakini akiwa mkweli atatuambia bila kificho kuwa watu wale wale waliokuja kufahamika baadaye kuwa mafisadi, ndio waliokuwa wanaomba CHADEMA iwape nafasi walipokuwa hawajaipata CCM.
Ndiyo maana wengi wetu tunatarajia kwamba Zitto angepaswa kuwa mwangalifu sana anapoletewa masharti ya namna hii na vigogo wa CCM wanaomuahidi kujiunga CHADEMA kwa kishindo iwapo atamuondoa Mbowe.
Ndiyo maana Zitto alipojisahau akaanza kutetea ununuzi wa mitambo ya Dowans, akidhani umaarufu wake ungeweza kubadili mjadala wa kitaifa na upepo wa kisiasa, wapambanaji wenzake walimsikitikia sana, na tuhuma za waziwazi zikaanza kurushwa dhidi yake kwamba kuna waliomharibu.
Na katika siku za hivi karibuni, Zitto amesikika akizungumza katika Radio Sauti ya Ujerumani akidai kwamba tofauti ya msingi kati yake na Mbowe katika kinyanganyiro cha uenyekiti ni kwamba Mbowe ni bepari, Zitto ni mjamaa!