Mdogo wangu, acha nikishauri kidogo.
1. Ndoa sio suala la kutafutia ushauri
Hapa naona vijana wengi wanaingia mkenge kwa kudhani kuwa kuoa na kuolewa ni suala la National Assembly yaani ushauri na majadiliano. Ndoa ni yako, maisha ni yako. Ukifika muda wa kuoa na ukajiona kuwa upo tayari kuoa na ukiwa umepevuka namaanisha ''matured'' huna haja ya kutafuta ushauri wa lini uoe wala umuoe nani.
2. Suala la kuoa mwanamke mwenye mtoto
Labda nikuulize, mwanamke akishazaa huwa anapungukiwa nini mwilini mwake? Kuzaa kwa mwanamke inamaanisha tu kuwa aliwahi kuwa na mahusiano na mtu, akapata ujauzito na hatimaye akazaa. Hilo tu.
Kinachowatofautisha wanawake waliozaa na wasio na watoto ni jambo moja tu; hawa wenye watoto wana ushahidi wa mahusiano yaliyopita na kubeba mimba ambazo walizitunza na hatimaye kuzaa.
Nikueleze tu; wanawake wengi ambao hawana watoto, waliwahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi kabla ya kukutana na wewe, wengine waliamua kutumia njia za uzazi wa mpango ili wasipate mimba, wengine walipata mimba na kuitoa ili kutunza unafiki wa kuonekana kuwa hawajapata mimba nje ya ndoa.
Sasa basi, kama kuna mwanamke unaona kabisa anafaa kuwa mke na ana mtoto, tatizo ni nini?
Najua hofu ya vijana ''eti atakuwa na mahusiano na baba mtoto''; kwanini huwa mnafikia tamati kuwa lazima wataendeleza mahusiano?
Wapo ambao wameamua kuachana na wakiingia kwenye ndoa wanabaki kuwa waaminifu kabisa.
Nikuulize swali, unafahamu ndoa ngapi ambazo wanawake na wanaume wanaendeleza mahusiano yao ya kimapenzi ya zamani na hawana watoto?
3. Akili za kuambiwa changanya na za kwako
Hapa kuna mtego unauingia bila sababu, kwanini unatafuta ushauri juu ya aina ya mwanamke wa kumuoa? Huyu mwanamke unaoelea familia ama ni kwa ajili yako?
Embu nikuulize; mpaka hapo ulipofika hujawahi kuwa na mahusiano na wanawake wengine? Hao wanawake wapo wapi kwa sasa? Huko walipo hawana mahusiano na wanaume wengine?
Jambo la muhimu katika ndoa ni uaminifu, heshima na kuthaminiana.
Nikuambie tu kuwa kwa mwanamke kutokuwa na mtoto sio kigezo cha yeye kuwa mke bora, hali kadhalika mwanamke kuwa na mtoto sio kigezo cha yeye kushindwa kuwa mke bora na kujenga familia.