Zumbemkuu na wadau wengine wa ujenzi:
Hii mada ya gharama za ujenzi imekuwa inakuja mara kwa mara kwenye ukumbi huu. Nami nimekuwa naifuatilia kwani ni shughuli ninayoipenda na ninajishughulisha nayo kwa muda mrefu.
Mimi ni mhandisi lakini siyo wa ujenzi, japo uchoraji na upigaji wa hesabu ndiyo shughuli yangu ya kila mara. Kwa kipindi kirefu nimekuwa natumia MS Excel kurahisisha makisio ya gharama za ujenzi. Na kwa kweli nimekuwa sichezi mbali sana na gharama halisi kwa kujenga mdogomdogo (yaani kwa kusimamia mwenyewe na mafundi wa mitaani maeneo ya Mwanza na Dar es Salaam.).
Muhimu ninajitahidi kupata ramani kamili ya nyumba ili kupata:
- Urefu wa kuta zote utakaosaidia kupata idadi kamili ya matofali
- Eneo la nyumba-sakafu (ground floor area) ili kupata gharama za sakafu, vigae, ceiling/gypsum board, idadi ya mabati nk.
- Eneo la kuta zote (wall area) ambalo linategemea unanyanyua kozi ngapi za matofali ili kupata idadi ya matofali, gharama za lipu, rangi nk.
Jedwali linasaidia kukokotoa idadi ya vifaa hivyo kirahisi baada ya kuweka vipimo hivyo vichache.
Kwa kutokana sasa na takwimu hizo kwa kutumia formular mbalimbali za civil engineering na uzoefu wa ujenzi, jedwali litakusaidia kupata makisio pia ya gharama kwa "automatic", yaani papo kwa papo. Fine tuning unaweza kuifanya, lakini tayari unakuwa na takwimu za kutosha hata ukimwita fundi muanze kujadiliana idadi ya vifaa vya ujenzi (matofali, ndoo za rangi, maboksi ya vigae, idadi ya mabati, gypsum board, nk) pia gharama za vifaa na gharama za ufundi kwa vile unakuwa una tatwimu zote muhimu na siyo kubishana tu na fundi.
Hili najua ni tatizo kubwa kwa watu wengi hasa wale wanaotaka kujenga nyumba kwa mara ya kwanza. Matokeo yake ni kutishika na kuacha kujenga au kupata mjanja akakuzidi akili na kuishia kununua vifaa vingi usivyohitaji na kama haupo site anaviuza! Aidha matokeo ya mkokotoo wa gharama hizi unaweza kukusaidia kupanga vizuri awamu za ujenzi kwa kulingana na uwezo wako ili ujenge nyumba yako bila taabu.
Nashukuru programu ya BURE ya Sweethome huwa hainiangushi, kwa muda wa nusu saa tu naweza kuchora ramani ya nyumba kubwa inayojitosheleza. Lakini hii ni kwa vile nimefundisha technical drawing na nimejifunza na kuitumia AutoCAD miaka ya nyuma. Hata hivyo ni programu rahisi kwa mtu yeyote kujifunza mwenyewe kama ana uelewa wa ufundi kidogo. Upungufu wake ni kutoweka paa kirahisi. Hivyo huwa nakomea kwenye kuta tu na kukweka furniture halisi kirahisi kabisa nipendavyo ili kupata feeling ya nyumba itakavyokuwa.
Sweet Home 3D - Draw floor plans and arrange furniture freely
Kama una mchoro wa nyumba yako tayari, ingiza urefu wa kuta zote (ndani na nje) kwa utaratibu mzuri bila kukosea. Ni kujumlisha na kutoa tu. Kwa kurahisisha unaweza kujikumbusha hesabu za mzingo pia. Kisha kokotoa eneo la sakafu. Halafu mambo mengine ya kufanya ni kuingiza bei za ufundi/vifaa mbalimbali kulingana na eneo lako kama unaona zangu si sahihi.
Jaribu kubadili takwimu kwenye maeneo MEUPE tu. Ama sivyo kama hujui kutumia Excel utaivuruga!
Nakiri kwamba haya makisio bado si kamili, kwa mfano sijaweka zege la msingi na makisio mengine yanaweza kuendelea kuboreshwa. Lakini kwa sasa nimeona nitoe mchango huu bure kwa jamii - eeh jamiiforums.
Upande wa msingi bado haujakaa vizuri na kwa kweli unategemea sura ya eneo na tabia ya ardhi unapotaka kujenga nyumba yako. Kazi hii hakikisha inafanywa kitaalamu. Kwa hiyo kwa upande wa msingi unaweza kuweka kozi 0 za msingi na hivyo kuondoa kabisa makisio ya msingi. Lakini kama unajenga msingi wa tofali tu, makisio ya matofali yanayohitajika utayapata.
Hapa nimeambatanisha:
- Ramani ya nyumba ikiwa na vipimo (ramani ambayo ilitolewa hapa na Zumbemkuu. Nimetumia ramani hii kugandamizia ili kuchora ramani hii(programu ya Sweet Home 3D inaruhusu jambo hili).
- Jedwali la MS Excel. NB: Jedwali la MS Excel ninalotoa hapa lina formular nyingi na nyingine nitazidi kuziongeza jinsi muda wangu unavyoruhusu, kwa hiyo pitia hapa kupata jedwali jipya au lililoboreshwa baada ya muda fulani.
****Nimeboresha tena awamu ya nne (Version 4)****:
- Ramani: Test house plan Vers3 - 12-2014-combined.pdf
- Jedwali_la_kukadiria_gharama_za_ujenzi_Test-House-Vers4.xlsx